Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka utaratibu wa kuvua kambamiti kwa wavuvi wakubwa na wadogo ili kufanya kambamiti waweze kuzaliana na kukua.
Hayo yamebainishwa leo bungeni na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kibiti Mhe. Twaha Ally Mpembenwe, ambaye alitaka kufahamu ni lini serikali itatoa uamuzi wa kuwaruhusu wavuvi wa kambamiti kuvua kuanzia mwezi Desemba hadi Julai kila Mwaka.
Alisema, utaratibu huo wa kuvua kambamiti umewekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo unaruhusiwa kufanyika kuanzia mwezi Machi hadi Septemba kila mwaka kwa ukanda wa Kaskazini unaohusisha Wilaya za Bagamoyo, Pangani na Chalinze na kuanzia mwezi Aprili hadi Agosti kila mwaka kwa Ukanda wa Kusini unaohusisha Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Kilwa.
Aliongezea kuwa, kipindi kilichobaki kimeachwa ili kambamiti waweze kuzaliana na kukua.
Maamuzi haya yamefanyika baada ya taarifa za utafiti wa kisayansi na kuzingatia uendelevu wa Rasilimali hii.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2009 na Marekebisho yake ya mwaka 2020; Serikali haijawahi kuzuia uvuvi wa kambamiti” Alisema Mhe. Ulega
Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Twaha Mpembenwe, ambaye alitaka kufahamu siku serikali itaruhusu uvuvi wa kambamiti kuanzia mwezi Desemba hadi Mei kila mwaka, Mhe. Ulega alisema serikali inatambua kuwa shughuli kuu ya wananchi katika baadhi ya maeneo ya Kibiti na Mkuranga wanatengemea uvuvi hasa wa kambamiti.
Alisema, katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa suala hili Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na Idara ya Uvuvi kwa kushirikiana na wavuvi itafanya tena utafiti katika maeneo ya uvuvi kwa kambamiti ili kupata mwafaka wa pamoja wa suala hili.
“Serikali imejipanga kuwezesha wavuvi kuweza kunufaika na rasilimali za uvuvi katika maeneo yao, samaki wanakulia maeneo ya kibiti na baadhi kuelekea maeneo ya Bahari Kuu ambako wavuvi wengi wanashindwa kufika kwa ajili ya kuvua “ Alisema Mhe. Ulega.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ilala, Mhe. Mussa Zungu aliyetaka kufahamu ni kwa nini wavuvi katika soko la feri jijini Dar es Salaam wanashindwa kusajili vyombo vya uvuvi hasa katika zone na. 8 kunakosababishwa na kuwepo kwa vitendo vya rushwa, Mhe. Ulega alisema kuwa mwenye mamlaka ya kutoa leseni kwa vyombo vya uvuvi katika wilaya ni Mkurugenzi wa Halmashauri kupitia Idara yake ya uvuvi ama afisa mwingine aliyeidhinishwa.
“Mhe. Mwenyekiti ikiwa kama feri, soko ambalo linamilikiwa na Manispaa ya Ilala kuna vitendo visivyokuwa vya nidhamu vya uvunjifu wa sheria, kama ulivyosema watu wanatoa rushwa natoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala na mamlaka zote pale ilala zishughulikie jambo hili na hao wanaofanya vitendo hivi tumepata taarifa za awali na vyombo vyetu vya dola vinafanyia kazi, hiyo ni kinyume cha sheria, vyombo vyetu vitachukua hatua stahiki na jambo hilo liachwe mara moja.” Alisema Mhe. Ulega
Mhe. Ulega alihitimisha majibu yake kwa kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Mtama Mhe. Nape Nnauye aliyetaka kufahamu ni lini serikali itatekeleza ahadi ya kuwasaidia wavuvi ukanda wa Pwani kupata injini za boti ambapo amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itapeleka mashine za boti kwa wavuvi katika jimbo la Lindi mjini na Mtama kama ilivyoahidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni