Naibu Waziri wa mifugo na uvuvi Mhe. Abdalla Ulega amesema Wizara hiyo ina mkakati wa miaka mitatu (2020/2021 – 2022/2023) ambao umelenga kuendeleza mashamba kwa kuongeza ng’ombe wazazi na kuimarisha huduma za uhimilishaji ili kupata ngombe bora na wenye tija.
Ulega aliyasema hayo bungeni Mei 24, 2021 wakati akijibu swali la Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Sanga ambaye alitaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuendeleza Shamba la Mifugo la Kitulo.
Mhe. Ulega alisema kuwa katika kutekeleza Mkakati huo Wizara kupitia bajeti ya mwaka 2021/2022 imenunua madume matano (5) ya ng’ombe wazazi kutoka shamba la Shafa Farm lililopo mkoani Iringa, kilo 400 za mbegu za malisho kutoka Marekani na nyingine 100 kutoka Kenya kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa malisho.
Alisema, shughuli nyingine ni uhimilishaji ambapo ng’ombe 135 wamehimilishwa na ununuzi wa tenki la kupoozea maziwa lenye ujazo wa lita 3,000 ambapo utaratibu wa manunuzi unakamilishwa.
“Shamba la Kitulo linahitaji uwekezaji wa kiasi cha shilingi bil. 6.6 ili kufikia kiwango cha juu cha uzalishaji, na uwekezaji huu utaendela kufanywa na Serikali kadri ya upatikanaji wa fedha kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo.” Alisema Ulega
Aidha akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Sanga aliyetaka kufahamu iwapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo tayari kushirikiana na benki ya maendeleo ya kilimo (TADB) ili kuendesha shamba ilo kwa tija zaidi na kujua siku ambayo maslahi ya wafanyakazi yatalipwa na vifaa kununuliwa, Mhe. Ulega alisema juu ya uwekezaji wapo tayari na milango yetu ipo wazi, karibuni tuweze kujadili jambo hilo, na jambo la kuboresha maslahi na kununua vifaa ni sehemu ya pesa zilizopangwa kutumika kwenye bajeti hii, hivyo hilo tunalielekea pia.
Kwa upande wake Mbunge wa Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete alitaka kufahamu siku Serikali itapima eneo la mifugo la Ruvu na kulikabidhi kwa Halmashauri ya Chalinze ambapo Mhe. Ulega alisema Serikali imeshapima na kutoa kipande cha ardhi chenye ukubwa wa hekta 2,208 kutoka Ranchi ya Ruvu kwa ajili ya matumizi ya wananchi.
Aliongeza kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ilikatiwa hekta 1,488 kwa ajili ya vijiji sita ambavyo ni; kijiji cha Ruvu Darajani hekta 200; kijiji cha Kidogozero hekta 200; kijiji cha Kitonga hekta 480; kijiji cha Magulumatali hekta 200; kijiji cha Vigwaza hekta 8 na kijiji cha Milo-Kitongoji cha Kengeni hekta 400.
Aidha, Serikali imepima na kutoa kipande cha ardhi chenye ukubwa wa hekta 120 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa ajili ya vijiji vitatu vya Kidomole hekta 40; Fukayosi hekta 40 na Mkenge hekta 40. Pia, Serikali imepima na kutoa ardhi yenye ukubwa wa hekta 600 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha vijijini kwa ajili ya kijiji cha Mperamumbi Kitongoji cha Waya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni