Nav bar

Jumamosi, 1 Mei 2021

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUPIMA AFYA ZAO MARA KWA MARA

 Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo),  Prof. Hezron Nonga, ametoa wito kwa  watumishi wa umma kupima afya zao mara kwa mara ili kutambua afya zao kama ambavyo muongozo wa kudhibiti virusi vya ukimwi (VVU), Ukimwi na magonjwa sugu yasiyo ambukiza mahala pa kazi unavyowataka.

 

Prof. Nonga, aliyasema hayo  wakati akifungua mafunzo pamoja na upimaji wa afya kwa watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi yaliyofanyika Jijini Dodoma Aprili 30, 2021.

 

Alisema kuwa upimaji wa afya kwa watumishi wa umma kwa mujibu wa muongozo huo wa mwaka 2014 ni jambo la lazima siyo hiyari.

 

“Kupima afya ni jambo la lazima na muhimu sana kwa mtumishi kwani itasaidia hata kuongeza tija katika taasisi baada ya kutambua afya yake” amesema Prof.Nonga.

 

Aidha amesema kuwa kwa kutambua afya za wafanyakazi kutamwezesha  mwajiri kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa jukumu mbalimbali.

 

“Kama mtumishi atakuwa na afya njema basi atasaidia kuongeza uzalishaji katika taasisi hivyo wafanyakazi wanatakiwa kupima afya zao kwa mujibu wa muongozo huo wa kudhibiti vvu, ukimwi, pamoja na magonjwa sugu yasiyoambukiza” alisisitiza Prof. Nonga.

 

Aliongeza  kuwa, kwa mtumishi ambaye atabainika mara baada ya vipimo kuwa ana maambukizi ya virusi vya ukimwi taratibu zinamtaka mwajiri wake kumpatia kiasi cha Sh. 100,000 kila mwezi.

 

Alisema kuwa mafunzo hayo kwa wafanyakazi, watapatiwa mada mbalimbali kutoka kwa watalaam wa masula ya afya.

 

“Wafanyakazi wanatakiwa pia kufanya mazoezi ili kuondokana na tatizo la uzito uliopitiliza pamoja na msongo wa mawazo” alisema.

 

Kwa upande wake mtoa mada katika mafunzo hayo Daktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Garvin Kweka, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongea na watumishi ili kuwasaidia kujenga tabia ya kutambua afya zao mara kwa mara.

 

“Leo nimekuja kuzungumza na watumishi hawa kwani tumekuwa tukipoteza nguvu kazi nyingi kutokana na magonjwa, asilimia 60 ya watumishi inaonyesha wana tatizo la uzito kupindukia pamoja na msongo wa mawazo kwa hiyo mafunzo haya yatawasaidia kutambua nini wafanye na kipi wasifanye ili kuwa na afya njema, ili kuendelea kuleta tija katika maeneo yao ya kazi”alisema Dk.Kweka.

 

Naye Mratibu wa Ukimwi, Vvu na magonjwa sungu yasiyoambukiza mahala pa kazi Sekta ya Mifugo Rachel Maliselo, amesema kuwa lengo la zoezi hilo ni kutoa fursa kwa wafanyakazi kupima afya zao kwa mujibu wa muongozo huo.

 

Alisema wafanyakazi wamefurahi sana kupata fursa hii kwani inawapa nafasi ya kutambua afya zao na kufanya kazi  kwa bidii na kuongeza tija katika maeneo yao ya  kazi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Hezron Nonga akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo (hawapo pichani) wakati akifungua mafunzo pamoja na upimaji wa afya yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma Aprili 30, 2021.


Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Mifugo) walioshiriki mafunzo pamoja na upimaji  afya yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma. Aprili 30, 2021.


Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimali watu, Bw. Fraksed Mushi, akimkaribisha Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Hezron Nonga (hayupo pichani) kufungua mafunzo pamoja na upimaji wa afya yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma 31.04.2021.


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Hezron Nonga akiongoza watumishi wa Wizara hiyo (hawapo pichani) kwenye zoezi la upimaji afya mtumba jijini Dodoma Aprili 30, 2021.


Daktari Bingwa wa magonjwa yasiyo ambukiza kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Garvin Kweka akieleza lengo la kutoa mafunzo  ikiwa ni pamoja na kuwasaidia watumishi  kujenga tabia  ya  kupima na kutambua afya zao mara kwa mara mtumba jijini Dodoma. Aprili 30, 2021.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni