Serikali imewataka wadau wa uwekezaji nchini kugeukia Sekta ya Mifugo hasa katika kutumia fursa ya changamoto ya uhaba wa mbegu za malisho ambayo mahitaji yake ni zaidi ya tani milioni 7 kulinganisha uzalishaji wa sasa wa tani 127 pekee.
Rai hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akifungua warsha maalum ya wadau wa uzalishaji mbegu za malisho hapa nchini Mkoani Morogoro 12, Mei 2021.
Alisema kuwa takwimu zinaonyesha kiwango cha uzalishaji wa mbegu ni mdogo ukilinganisha na mahitaji yake na kwamba kama wawekezaji wakigeuza changamoto hiyo kuwa fursa inasadia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji.
“Mahitaji ya mbegu za malisho Tanzania ni tani milioni 7 lakini kiwango cha mbegu kilichozalishwa kwa mwaka 2019/20 ni tani 127 maana yake ni kwamba kuna uhaba mkubwa sana ivyo changamoto hiyo tuichukulie kama fursa ya uwekezaji katika sekta hiyo” alisema Prof Gabriel.
Kadharika alisema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, makampuni na watu binafsi wenye nia ya kuzalisha mbegu bora za malisho, kufanya kazi hii kibiashara kwa kuwapa mwongozo unaostahili.
Alibainisha kuwa lengo ni kufanikisha juhudi hizi za Serikali hasa kujiletea faida za kiuchumi kupitia uwepo wa fursa ya wingi wa mifugo nchini na hata kuuza malisho katika mataifa mengine.
“Hii si tu kwamba itainua uchumi wa mtu binafsi bali italipatia Taifa fedha za kigeni, hasa tukizingatia kuwa wananchi wanaweza kutumia fursa ya ardhi iliyopo kuzalisha malisho kibiashara kama wanavyo zalisha mazao ya chakula”. alisema Prof. Gabriel
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Utafiti Mafunzo na huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa alisema lengo la warsha hiyo ni kuhakikisha tafiti zilizofanyika kubaini mbegu bora za malisho zinawafikia wafugaji wadogo kwenye mashamba yao.
Alisema zipo mbegu ambazo zimekuwa rahisi kuwafikia wafugaji kama mbegu aina ya Nyasi, mikunde inayotaambaa na mikunde jamii ya miti malisho ambazo zipo katika makundu tofauti ambazo pia mahitaji ya msingi katika mashamba ya malisho.
“Tunaona kuna fursa kubwa ya uzalishaji wa mbegu endelevu na hapa tunazungumzia mbegu mafungu matatu ambazo hizo tunaangalia ni namna gani tunaongeza uzalishaji hapa nchini” alisema Dkt. Mwilawa.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof.
Elisante Ole Gabriel akifungua warsha ya wadau wa uzalishaji wa mbegu za
malisho kwenye ukumbi wa Cate hotel Mkoani Morogoro (12.05.2021)
Mkurugenzi wa Utafiti Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Angello Mwilawa akimkaribisha Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani), kufungua warsha ya
uzalishaji wa mbegu za malisho kwenye ukumbi wa Cate hotel Mkoani Morogoro.
(12.05.2021)
Mhadhiri mstaafu chuo kikuu cha Sokoine na Mwenyekiti mstaafu
wa chama cha nyanda za malisho Tanzania, Prof. Ephraim Mtengeti akimshukuru
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel
(hayupo pichani) kwa kuweza kushiriki nao na kufungua warsha ya uzalishaji wa
mbegu za malisho kwenye ukumbi wa Cate hotel Mkoani Morogoro 12.05.2021
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (waliokaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau walioudhuria warsha ya uzalishaji wa mbegu za malisho mara baada ya kufungua warsha hiyo kwenye ukumbi wa Cate hotel Mkoani Morogoro. (12.05.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni