Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesisitiza upatikanaji wa taarifa sahihi za uvuvi mdogo nchini kwa kuangaza taarifa za wavuvi wadogo zilizofichika ili ziweze kutumika kwa mipango ya maendeleo endelevu kwa lengo la kukuza Uchumi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa warsha ya wadau wa sekta ya uvuvi ya kupitia matokeo ya utafiti wa mchango wa Uvuvi mdogo iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (DRTE) Dkt. Erastus Mosha mjini Morogoro (21.5.2021).
Akisoma hotuba hiyo, Mkurugenzi amewakumbusha wadau kuwa Uvuvi ni sayansi, hivyo usimamizi wa rasilimali hiyo ni muhimu na unahitaji taarifa za kutosha za kitafiti ili kufikia malengo ya kuwa na Uvuvi endelevu nchini.
Alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya Uvuvi kwa muda mrefu kuwa ni kukosekana kwa taarifa sahihi za mavuvi, zana haramu, idadi ya wavuvi, vyombo vya Uvuvi na nyinginezo.
Pia alisema ana matumaini makubwa kuwa matokeo ya utafiti huo wa kuangaza taarifa za uvuvi zilizofichika yatasaidia kuboresha mipango ya sekta ya Uvuvi nchini kuendana na kasi ya maendeleo ya viwanda na kuongeza mchango wa sekta kwenye pato la Taifa kutoka asilimia 1.7 hadi asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025.
Aidha katika hotuba yake mgeni rasmi aliwafahamisha wadau kuwa,mwaka 2016 Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliingia makubaliano na Shirika la Kilimo na Chakula (FAO) ili kutekeleza mradi wa kuwezesha utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Mdogo unakuwa Endelevu katika Muktadha wa Uhakika wa Chakula na Kuondoa umasikini.
Aliongeza kuwa matokeo mazuri yanayoendelea kutokea yanatokana na Mradi wa kutekeleza Mwongozo wa Wavuvi Wadogo (SSF Guidelines),ambapo Wizara kwa mara nyingine tena ilisaini makubaliano ya kutekeleza Mradi huo wa kuimarisha mchango wa Uvuvi Mdogo kwa usalama wa Chakula na Maisha Endelevu.
Kwa upande wake kiongozi wa timu ya utafiti Dkt. Paul Onyango kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam anasema utafiti huo uliofadhiliwa na FAO ulianza Mwaka 2018, na umefanyika kwenye takribani nchi 40 Duniani.
Akigusia matokeo ya utafiti huo, Dkt. Onyango anasema kuwa kuna taarifa nyingi zilizofichika ambazo zinasababisha thamani ya mchango wa uvuvi mdogo kiuchumi kuonekana ndogo sana tofauti na uhalisia wenyewe.
Dkt. Onyango anabainisha mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hiyo kuwa ni vyema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) kuwa na bajeti maalum ya ukusanyaji takwimu za wavuvi wadogo, kuongeza wakusanya takwimu wenye weledi wa kazi hiyo na pia kutoa elimu kwa wavuvi kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa sahihi kwa Serikali.
Mvuvi mdogo Bw. Peter Sumuni kutoka ziwa Nyasa akizungumzia sababu ya wao wavuvi kutokutoa takwimu sahihi kwa maafisa Uvuvi wa maeneo yao, anasema kuwa hawana elimu ya kutosha ya umuhimu wa takwimu hizo pia ushirikiano wao na maafisa Uvuvi hauridhishi.
Aidha Bi.Sijali Hemedi kutoka Kilwa ambaye ni mkusanya takwimu ameelezea kuwa changamoto ni uchache wa wakusanyaji wa takwimu pamoja na uwezeshwaji wa rasilimali Fedha kwa ajili ya kazi hiyo.
Ili kufanikisha lengo la kuwa na Uvuvi Endelevu kwa ajili ya kukuza uchumi, Bw. Yusuph Semuguruka kutoka ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anasisitiza ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na TAMISEMI ikiwa ni pamoja na kufuata taratibu za kupeana taarifa katika utekelezaji wa shighuli mbalimbali za sekta ya Uvuvi nchini.
Mgeni
rasmi,Kaimu Mkurugenzi, idara ya utafiti, Mafunzo na Ugani (DRTE) Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Erastus Mosha akisoma hotuba ya ufunguzi wa warsha
ya wadau wa sekta ya uvuvi ya uwasilishwaji wa matokeo ya utafiti wa mchango wa
uvuvi mdogo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi.Warsha hiyo inayofanyika
(20-21.5.2021) kwenye hoteli ya Edema mjini Morogoro imehusisha wadau
mbalimbali wakiwemo wavuvi, wakusanya takwimu, watafiti na watumishi kutoka
sekta ya Uvuvi.
Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha
Maandalizi ya Mpango wa Utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa Kuendeleza Sekta ya
Uvuvi Mdogo nchini, Alhaj Yahya Mgawe akitoa maelezo ya awali kuhusu suala la
Uvuvi mdogo nchini kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha ya wadau
wa sekta ya uvuvi ya uwasilishwaji wa matokeo ya utafiti wa mchango wa uvuvi
mdogo inayofanyika kwenye Hoteli ya Edema iliyopo mjini Morogoro
(20-21.5.2021).Utafiti huo umefanywa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa
ufadhili wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).
Bw. Yusuph Semuguruka kutoka Idara ya Uratibu
wa Sekta Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) akitoa
salamu za ofisi hiyo kabla ya kukaribishwa kwa Mgeni rasmi kufungua warsha ya
wadau wa sekta ya uvuvi ya uwasilishwaji wa matokeo ya utafiti wa mchango wa
uvuvi mdogo inayofanyika kwenye Hoteli ya Edema iliyopo mjini Morogoro
(20-21.5.2021) ambapo alisisitiza ushirikiano kati ya Wizara na TAMISEMI katika
utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Uvuvi nchini.Utafiti huo umefanywa na
Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa ufadhili wa Shirika la Chakula na Kilimo
Duniani (FAO).
Baadhi ya watafiti Dkt. Paul Onyango kutoka
Chuo Kikuu cha Dar es salaam (kulia) ambaye ndio kiongozi wa timu ya watafiti
na Bi. Fatma Sobbo wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati
wa ufunguzi wa warsha ya wadau wa sekta ya uvuvi ya uwasilishwaji wa matokeo ya
utafiti wa mchango wa uvuvi mdogo inayofanyika kwenye Hoteli ya Edema iliyopo
mjini Morogoro (20-21.5.2021). Utafiti huo umefanywa na Chuo Kikuu cha Dar es
salaam kwa ufadhili wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).
Mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi, idara ya utafiti,
Mafunzo na Ugani (DRTE) Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Erastus Mosha
kwenye picha ya pamoja (waliokaa,katikati) mara baada ya ufunguzi wa warsha ya
wadau wa sekta ya uvuvi ya uwasilishwaji wa matokeo ya utafiti wa mchango wa
uvuvi mdogo inayofanyika kwenye Hoteli ya Edema iliyopo mjini Morogoro
(20-21.5.2021). Utafiti huo umefanywa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa
ufadhili wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) ambapo utafiti huo umependekeza
serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) kuwa na bajeti maalum ya
utafiti, kuwa na wakusanya takwimu wenye weledi pamoja na utoaji wa elimu kwa
wavuvi ikilenga kuwaelimisha umuhimu wa kutoa takwimu sahihi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni