Serikali imeendelea kuhamasisha uanzishwaji na uimarishaji wa vikundi na vyama vya ushirika vya msingi vya wavuvi wadogo kwa lengo la kuwapatia mtaji, ujuzi, vifaa pamoja na dhana za uvuvi katika maeneo ya mwambao wa bahari ya hindi , maziwa, mabwawa na mito ili kuzalisha ajira na kipato.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Nyasa, Mhe. Eng. Stella Manyanya ambaye alitaka kufahamu mikakati ya Serikali katika kuhakikisha mikopo inatolewa kwa mtu mmoja mmoja aliye tayari, kuliko kutoa kupitia vikundi jambo ambalo linachelewesha ukuaji wa sekta ya uvuvi.
Mhe. Ulega alisema kuwa katika kutekeleza ilani kwa mwaka wa fedha 2020/2021 serikali iliadhimia kuhamasisha wavuvi na wakuzaji viumbe maji kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili kuwa na sauti ya pamoja ikiwa ni rahisi kutatua changamoto zinazowakabili kwa pamoja na kuwa na usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi.
Aidha Serikali iliwezesha vyama vya ushirika kwa kuvipatia elimu, dhana na vifaa bora vya uvuvi kama vile injini za boti, pamoja na kuviunganisha na taasisi za fedha ili kupata mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa lengo la kufanya shughuli zao kwa tija.
"Mhe. Naibu Spika kutokana na ilani ya chama cha mapinduzi Serikali itaendelea kuvihamasisha na kuviendeleza vyama vya ushirika, aidha mtu mmoja mmoja anayo fursa ya kuomba injini za boti kupitia taasisi za kifedha nchini.” Alisema Mhe. Ulega
Ulega aliongezea kuwa Serikali imejipanga vyema katika kuhakikisha wavuvi wote nchini wanapata suluhu ya changamoto zinazo wakabili wakiwemo wavuvi wa ziwa Nyasa na ndio maana imejipanga pia kwenda kuhakikisha inajenga soko la kisasa katika eneo la mwambao wa ziwa Nyasa.
Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Mwamtum Zodo, ambaye alitaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuwakwamua wavuvi wa pembezoni mwa bahari ya hindi, kwa mikoa ya Tanga, Dar- es- salaam, Pwani, Lindi na Mtwara katika kushiriki kwenye uchumi wa bluu, Mhe. Ulega alisema Serikali ya awamu ya sita inayo ongozwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, inayo mkakati madhubuti ya kuhakikisha inawasaidia wavuvi wa ukanda wa Pwani hasa kuendana na uchumi wa bluu kwa kuongeza uzalishaji kwa wavuvi kwa kuweka miamba ya kuvutia samaki na kutengeneza katika ukanda wote wa pwani
“Tutahakikisha kwamba tunatengeneza vichanja vya kukaushia samaki ili kusaidia kutopoteza mazao ya uvuvi wanayo zalisha, kwa kuoza na kuaribika, tunataka tuhakikishe samaki wote wanaozalishwa kwenye ukanda wa pwani hawaaribiki kwa sababu tutawaongezea thamani kwa kuwakausha lakini vilevile tutakwenda kuongeza uzalishaji wa barafu na kuwa na “cold rooms” za kutosha katika ukanda mzima wa pwani ili kuweza kuutumia vyema uchumi wa bluu na kuongeza kipato cha mvuvi mmoja mmoja na hatimae kuongeza kipato cha Serikali yetu. Alisema Ulega.
Hata hivyo ametoa wito kwa wabunge wote kuhimiza wavuvi na wakuzaji viumbe maji wa maeneo yao kujiunga kwenye vyama vya ushirika vya wavuvi kama chachu ya kuwaletea maendeleo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni