Nav bar

Ijumaa, 25 Novemba 2022

MAABARA ZA TVLA SASA ZAFANYA KAZI KIDIGITALI

Na Mbaraka Kambona,


Wakala ya Maabara ya Mifugo Tanzania (TVLA) imewezeshwa vifaa vya kisasa katika maabara zake ambapo sasa wamekuwa na  uwezo wa kutambua kwa haraka vimelea vya magonjwa ya mifugo ndani ya dakika 15 tofauti na hapo awali ambapo ilikuwa inawachukua kati ya masaa 24 hadi 36.


Hayo yamefahamika  leo Novemba 21, 2022, jijini Dar es Salaam wakati  Mwakilishi kutoka Taasisi ya American Society for Microbiology, Dkt. Wes Kim akimkabidhi  Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Prof. Hezron Nonga nyaraka za vifaa vya maabara ambavyo vimegharimu zaidi ya Shilingi za Kitanzania Milioni 600.


Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Prof. Nonga alisema kuwa lengo la kuboresha maabara hizo ni kuzijengea uwezo hasa kwenye kubaini uwepo wa vimelea ambavyo vimepelekea matumizi makubwa ya dawa za antibayotiki kwenye mifugo hasa kuku.


“Kutokana na mazingira tuliyonayo Tanzania, uwepo wa vimelea haukwepeki kutokana na joto, mvua na hali ya unyevunyevu, na vimekuwa kikwazo kwenye uzalishaji na uzalianaji wa mifugo yetu, hivyo basi tunapokuwa na maabara zilizoboreshwa zaidi inakuwa ni rahisi kubaini aina ya kimelea na kuweza kujua aina ya dawa ambayo inaweza kutumika kutibu na kumsaidia mfugaji kufuga kwa tija na kuepukana na maradhi,”alisema Prof. Nonga


Aliongeza kwa kusema kuwa ili kuweza kupambana vyema na vimelea hivyo ni muhimu wadau wa mifugo wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye sekta ya mifugo ili iweze kuwa na tija zaidi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.


Naye, Mtendaji Mkuu, Wakala ya Maabara ya Mifugo (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi alisema msaada huo walioupata kutoka kwa taasisi ya Fleming Fund kupitia taasisi ya American Society for Microbiology umesaidia kuwawezesha kufanya kazi zao kwa haraka zaidi.


“Kabla ya kupata vifaa hivi ilikuwa inatuchukua masaa zaidi ya 24 kutambua vimelea vya magonjwa ya mifugo lakini baada ya kupata msaada huu sasa tunaweza kutambua vimelea ndani ya dakika 15 tu,”alifafanua Dkt. Bitanyi


Aliongeza kuwa teknolojia hiyo ya kisasa waliyoipata inafanya maabara zao ziendane na teknolojia iliyopo duniani ambayo inawawezesha pia kutambua aina ya kimelea na ukoo wake.


Kwa upande wa Mwakilishi kutoka Taasisi ya American Society for Microbiology, Dkt. Wes Kim alisema kuwa wataendelea kutoa ushirikiano kwa serikali katika kupambana na vimelea vya magonjwa ya  mifugo ili kuweka msingi mzuri wa afya ya mifugo na usalama wa chakula kwa jamii.  


Aidha, taasisi hiyo pia iko mbioni kuzisaidia maabara nyingine zilizo chini ya TVLA ikiwemo ya Iringa ambayo hivi karibuni nayo itakabidhiwa vifaa kwa lengo hilo hilo la  kuboresha utendaji wa maabara nchini.


Wakala ya Maabara ya Mifugo(TVLA) ni Wakala ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi yenye vituo 11 vilivyopo katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Mwanza, Arusha, Tabora, Mtwara, Sumbawanga, Simiyu, Kigoma na Tanga.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Hezron Nonga(Kushoto) akipeana mkono na Mwakilishi wa Taasisi ya American Society for Microbiology, Dkt. Wes Kim muda mfupi baada ya kusaini nyaraka za makabidhiano ya vifaa vya maabara vilivyokabidhiwa kwa Wakala ya Maabara ya Mifugo Tanzania (TVLA) katika hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 21, 2022.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Hezron Nonga(Kushoto) na Mwakilishi wa Taasisi ya American Society for Microbiology, Dkt. Wes Kim(kulia) wakisaini nyaraka za makabidhiano ya vifaa vya maabara vilivyokabidhiwa kwa Wakala ya Maabara ya Mifugo Tanzania (TVLA) katika hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika jijini Dar es Salaam  Novemba 21, 2022. Wa kwanza kushoto aliyesimama ni Mkurugenzi Mtendaji wa TVLA, Dkt. Stella Bitanyi. Kulia ni Afisa kutoka taasisi ya American Society for Microbiology, Ade Olarewaju.

Mkuu wa Maabara ya Bakteliorojia kutoka Wakala ya Maabara ya Mifugo Tanzania (TVLA), Godwin Minga (kushoto) akitoa maelezo kwa Mwakilishi wa  Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Hezron Nonga(Kulia) na mgeni wake, Mwakilishi wa Taasisi ya American Society for Microbiology, Dkt. Wes Kim kuhusu mashine inayotumika kutambua vimelea vya magonjwa ya mifugo inavyofanya kazi walipotembelea maabara hiyo iliyopo  jijini Dar es Salaam Novemba 21, 2022.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Hezron Nonga(wa Sita kutoka Kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na  Mwakilishi wa Taasisi ya American Society for Microbiology, Dkt. Wes Kim (wa tano kutoka kushoto) walipotembelea moja ya maabara za  Wakala ya Maabara ya Mifugo Tanzania (TVLA) iliyopo jijini Dar es Salaam Novemba 21, 2022. Wengine katika picha ni Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wakala ya Maabara ya Mifugo, na Maafisa kutoka taasisi ya American Society for Microbiology.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni