Nav bar

Ijumaa, 25 Novemba 2022

MBEGU ZA MALISHO ZIPATIKANE KWENYE MADUKA YA PEMBEJEO-ULEGA.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kuhakikisha mbegu za malisho bora ya Mifugo zinapatikana kwenye maduka ya pembejeo za Kilimo na Mifugo ili kuwawezesha wafugaji kuzalisha malisho kwa urahisi zaidi.


Mhe. Ulega ameyasema hayo kwenye hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Faida Maziwa Tanzania uliofanyika jana (22.11.2022) kwenye Viwanja vya Ofisi za Taasisi hiyo kanda ya Mashariki zilizopo jijini Tanga.


"Moja ya jambo ambalo litatupa heshima kubwa sana ni kuhakikisha mbegu za malisho zinauzwa kama zilivyo mbegu za mazao mengine kama mahindi, mpunga na mengineyo kwa sababh tunatumia nguvu kubwa sana kuwahamisha wafugaji kuzalisha malisho bora kwa ajili ya Mifugo yao lakini mbegu za malisho hayo hazipatikani kwa urahisi hivyo ni muhimu sasa zikaanza kupatikana kwenye maduka yote ya pembejeo na hilo ninaagiza lifanyike haraka sana" Amesisitiza Mhe. Ulega.


Mhe. Ulega amebainisha kuwa hatua hiyo ikifikiwa, Nchi itakuwa imepiga hatua kwa vitendo kuelekea kwenye ufugaji wa kisasa na kutoa fursa kwa wazalishaji wa malisho hayo kujikita kikamilifu kwenye biashara ya malisho ambayo imeendelea kukua kwa kasi hivi karibuni.


" Kila mfugaji mwenye nia ya dhati ya kufanya shughuli hiyo ameshakubali kubadilika ili apate tija kwenye ufugaji wake na mojawapo ya mambo anayopaswa kufanya ni kuzalisha malisho yanayokidhi mifugo yake na kinyume na hapo ni aidha atapata hasara kwenye ufugaji wake au ataharibu mazingira" Amesisitiza Mhe.Ulega.


Akizungumzia kuhusiana na Mradi wa Faida Maziwa Tanzania Mhe. Ulega amebainisha kuwa mradi huo kwa kuanzia utalenga zaidi kujenga uwezo kwa wafugaji wa ng'ombe wa maziwa wanawake na vijana wasiopungua elfu 3 kwa kanda ya Mashariki na kufanya tafiti zenye matokeo chanja kwenye vikwazo vilivyopo katika mnyororo wa biashara ya maziwa kuanzia shambani, kiwandani hadi kufika kwa mlaji.


"Lakini pia mradi huu utatafiti juu ya malisho bora yanayoweza kuongeza uzalishaji wa maziwa ndani ya kaya, ng'ombe bora wa maziwa anayefaa kwa kanda ya mashariki kwa kuzingatia hali ya hewa na mabadiliko ya tabia nchi, kuimarisha huduma za ugani na ushirika kwenye Mkoa wa Tanga na kuimarisha miundombinu ya utafiti hasa maabara na mashamba darasa ya ufugaji ng'ombe bora wa maziwa na uzalishaji malisho ya Mifugo" Ameongeza Mhe. Ulega.


Kwa upande wake Balozi wa Ireland nchini Tanzania Bi. Mary O' Neill amesema kuwa mradi huo ni muendelezo wa mahusiano mazuri kati ya nchi yake na Tanzania ambapo amebainisha kuwa wanataka kuhakikisha mradi huo unatengeneza dira na somo endelevu kwa wafugaji wa ng'ombe wa maziwa ili iwasaidie hata mara baada ya mradi huo kukamilika.


"Uzinduzi wa mradi huu ni ishara ya mabadiliko kwenye sekta ya Ufugaji wa ng'ombe wa Maziwa nchini Tanzania na ni matumaini yetu kwa kutekeleza mkakati wa mabadiliko wa sekta ya Mifugo, Wizara itaendelea kuhamasisha ushiriki wa kila mdau aliyepp kwenye mnyororo wa thamani wa ufugaji wa ng'ombe wa maziwa bila kusahau makundi maalum hasa wanawake" Amesema Bi. O'Neill.


Bi. Oneil alitumia sehemu ya uzinduzi wa mradi huo kumkabidhi Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega jumla ya pikipiki 8 zitakazotumiwa na Maafisa ugani wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kutekeleza shuguli zao na gari moja litakalotumiwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kwenye utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kitafiti.


Akizungumzia kusudio la kutekeleza mradi huo katika maeneo mengie nchini, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Prof. Erick Komba amesema kuwa mbali na kufanya utafiti huo katika kanda ya Mashariki, matokeo yake yatasambazwa nchi nzima ili kuongeza tija kwenye kila hatua iliyopo kwenye mnyororo wa thamani wa maziwa nchini.


“Tunatekeleza mradi huu na nchi ya Ireland kwa sababu wao wanafanya vizuri sana kwenye upande wa uzalishaji na biashara ya Maziwa kwa ujumla hivyo naamini tutapeana uzoefu wa kutosha wa kitafiti kuhusu malisho ya mifugo, mbari na namna bora ya kutunza ng’ombe wa maziwa ili wazalishe maziwa kwa wingi” Amemalizia Prof. Komba


Mradi wa Maziwa Faida Tanzania unalenga kuongeza kiwango cha maziwa kwa kuboresha malisho ya ng'ombe wa maziwa na unatekelezwa kwa kipindi cha Miaka 5 ambapo kila mwaka unatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 6.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega na Balozi wa Ireland nchini Tanzania Bi. Mary O’Neill (katikati) wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa pikipiki 8 na gari moja vyote vikikabidhiwa na Bi. O’Neill kwa niaba ya Serikali ya Ireland jana (22.11.2022) ili vitumike  wakati wa utekelezaji wa mradi wa Faida Maziwa Tanzania unaotarajiwa kutekelezwa kwa miaka 5 hapa nchini. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Charles Mhina na kulia ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Bw. Albogasti Kimasa.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akimfafanulia Balozi wa Ireland nchini Tanzania Bi. Mary O’Neill (kushoto) namna mbegu za malisho ya mifugo zinavyopandwa katika mashamba mbalimbali hapa nchini muda mfupi kabla ya uzinduzi wa mradi wa Faida Maziwa Tanzania uliofanyika jana (22.11.2022) kwenye Viwanja vya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kanda ya Mashariki jijini Tanga.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akitoa maelekezo kwa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kuhakikisha mbegu za malisho zinapatikana  kwenye maduka yote ya  pembejeo nchini muda mfupi baada ya kufika kwenye Viwanja vya Taasisi hiyo kanda ya Mashariki jijini Tanga jana (22.11.2023)  ambapo pia alizindua mradi wa Faida Maziwa Tanzania. Kushoto ni Balozi wa Ireland nchini Tanzania Bi. Mary O’Neill na katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Pro. Erick Komba.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Kulia)  na Balozi wa Ireland nchini Tanzania Bi. Mary O’Neill (kushoto) wakiwasha pikipiki muda mfupi baada ya pande hizo kukabidhiana vitendea kazi hivyo vitakavyotumiwa na Maafisa Ugani wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kwenye utekelezaji wa mradi wa Faida Maziwa Tanzania uliozinduliwa rasmi jana (22.11.2022) kwenye hafla iliyofanyika viwanja vya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Kanda ya Mashariki jijini Tanga.

Balozi wa Ireland nchini Tanzania Bi. Mary O’Neill (kushoto) akisalimia na Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini (TDB) Dkt. George Msalya muda mfupi jana (22.11.2022) baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Kanda ya Mashariki jijini Tanga ambako alishiriki uzinduzi wa mradi wa Faida Maziwa Tanzania unaotekelezwa baina ya nchi ya Ireland na Tanzania. Katikati ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Charles Mhina.

Balozi wa Ireland nchini Tanzania Bi. Mary O’Neill (kushoto) akisalimia na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Prof. Erick Komba muda mfupi jana (22.11.2022) baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Kanda ya Mashariki jijini Tanga ambako alishiriki uzinduzi wa mradi wa Faida Maziwa Tanzania unaotekelezwa baina ya nchi ya Ireland na Tanzania. Katikati anayeshuhudia ni Mratibu wa Mradi huo kutoka TALIRI  Dkt. Zabron Nziku.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni