Nav bar

Ijumaa, 25 Novemba 2022

SERIKALI YAPONGEZA SEKTA BINAFSI KWA KUKUZA SEKTA YA UVUVI

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imelipongeza Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF) kwa kuviwezesha vikundi saba vya ujasiriamali vya uvuvi kwa jumla ya Shilingi Milioni Thelathini na Tano, pikipiki nne, boti tatu na injini zake, pamoja na makoti 30 ya kujiokoa (life jackets) kwa halmashauri mbili za Wilaya za Kilwa Mkoani Lindi na Kibiti Mkoani Pwani.


Shukrani hizo zimetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji, Bw. Anthony Dadu wakati wa maadhimisho ya siku ya mvuvi duniani yanayokwenda sambamba na Mwaka wa Kimataifa wa Wavuvi Wadogo na Wakuzaji Viumbe Maji 2022 (International Year of Artisanal Fisheries and Aquaculture (IYAFA) yaliyofanyika katika kijiji cha Somanga Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi.


Amesema hatua hiyo itaongeza chachu ya usimamizi bora wa rasilimali za uvuvi utakaopelekea upatikanaji kwa wingi wa mazao ya uvuvi yenye ubora na hivyo kuwezesha jamii kupata lishe bora na kuongeza kipato ikizingatiwa mafanikio katika usimamizi wa rasilimali za uvuvi yanategemea sana vitendea kazi imara.


"Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mkurugenzi Mkazi wa WWF Dkt. Amani Ngusaru kwa kuendelea kuwajali na kuwawezesha wananchi wetu katika kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na hivyo kuleta tija katika maisha yao" alisema Bw. Dadu katika taarifa hiyo.


Aidha amewataka viongozi wa vijiji ambao watanufaika na zana hizo ikiwemo Nyamatungutungu, Marendego, Njia nne, Somanga Kusini, Somanga Kaskazini, Songosongo, Pombwe, Jaja, Kiomboni, Msala, Dongo, Kilindoni, Chunguruma, na Ndagoni kutimiza wajibu wao mkubwa wa kushirikiana kuvitunza vitendea kazi hivyo ili vinufaishe taifa na familia zao.


Hali kadhalika aliwataka wakurugenzi wa halmashauri zote kuhakikisha wanapata taarifa za mara kwa mara juu ya matumizi sahihi na yaliyokusudiwa kupitia vifaa hivvyo. 


"Nitoe wito kwa halmashauri husika kuona umuhimu wa kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni (BMU) katika halmashauri zenu zinanufaika na vifaa hivi pale wanapohitaji kuvitumia katika maeneo yao." Alisema Bw. Dadu


Aidha amewakumbusha kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha Sheria ya Uvuvi na Kanuni zake zinazingatiwa hali itakayosababisha waendelee kunufaika na fursa nyingi zilizopo katika sekta ya uvuvi. 


Akiwasilisha mada kuhusu dhima ya siku ya mvuvi duniani Mratibu wa Programu ya Bahari na Pwani WWF Dkt. Modesta Medard amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (FAO) inaonesha zaidi ya theluthi mbili ya samaki wote duniani wamevuliwa kupita kiasi au wamevuliwa wote na zaidi ya theluthi moja wako katika hali ya kupungua.


Amesema sababu ya kupungua huko ni kutokana na kutoweka kwa makazi ya samaki, uchafuzi wa mazingira na ongezeko la joto duniani ambapo siku ya mvuvi duniani inasaidia kutambulisha umuhimu wa sekta ya uvuvi kwa maisha ya binadamu, viumbe maji kwenye mito, maziwa na bahari.


"Samaki wanamchango mkubwa katika uhakika wa chakula duniani ni muhimu kwa lishe bora ya watu wote ulimwenguni hususan kwa jamii zilizopo karibu na mito maziwa na bahari" alisema.

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za ugani wa uvuvi na ukuzaji viumbe maji kutoka waizara ya mifugo na uvuvi, Bw. Anthony Dadu akiongea na Wavuvi wa Kijiji cha somanga wilaya ya kilwa wakati wa maadhimisho ya siku ya mvuvi duniani yaliyofanyika kijijini hapo mkoani Lindi, Novemba 21, 2022

Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na wanyama pori (WWF), Dkt. Amani Ngusaro akieleza vitu walivyoleta kwa ajili ya wavuvi ikiwa ni pamoja na pikipiki nne, boti aina ya faiba tatu na mikopo wakati wa maadhimisho ya siku ya mvuvi duniani yaliyofanyika kwenye kijiji cha somanga mkoani Lindi, Novemba 21, 2022.

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za ugani wa Uvuvi na Ukuzaji viumbe maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Anthony Dadu akikata utepe ishara ya kukabidhi pikipiki kwa wavuvi zilizotolewa na Shirika la kimataifa la uhifadhi wa mazingira na  wanyamapori (WWF)Mkoani Lindi, Novemba 21, 2022.

Moja ya boti zilizotolewa na Shirika la kimataifa la uhifadhi wa mazingira na wanyamapori (WWF) Ili kuwasaidia wavuvi kufanya uvuvi endelevu na wenye tija kwenye kijiji cha Somanga, Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, Novemba 21,2022.

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani wa uvuvi na Ukuzaji viumbe maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Anthony Dadu (kushoto) akifanya usafi kwenye fukwe za bahari na baadhi ya wavuvi ikiwa ni siku ya maadhimisho ya mvuvi duniani yaliyofanyika kwenye kijiji cha Somanga, kilwa Mkoani Lindi, Novemba 21,2022.

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani wa uvuvi na Ukuzaji viumbe maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Anthony Dadu (wa tano kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na vikundi vya vijana wanaojishughulisha na Uvuvi mara baada ya kufanya usafi kwenye fukwe ya bahari kwenye kijiji cha Somanga Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, wa tatu  kulia ni Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara hiyo Bi. Upendo Hamidu. Novemba 21,2022

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni