Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania imepanga kutoa huduma ya Chanjo pamoja na upimaji wa magonjwa ya mifugo bure kwa maeneo yatakayobainishwa kwenye vituo vya 11 vilivyopo Tanzania nzima kuanzia tarehe 21/11/2022 hadi tarehe 25/11/2022 ikiwa ni maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza na vyombo vya habari Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania-TVLA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Dkt.Qwari Bura kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi siku ya tarehe 20/11/2022 mtaa wa Bomani Mkoani Iringa kwa ajili ya kuutambulisha Umma alisema kwamba wakala imepanga kuwafikia wafugaji na kurudisha kile ilichokipata kwa jamii ikiwa ni Maadhimisho ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012.
Dkt. Bura alisema kwamba wakala ilizinduliwa rasmi tarehe 11 Julai, 2012 na Katibu Mkuu Kiongozi na hadi kufikia mwaka huu 2022 Wakala imetimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake kutokana na kuunganishwa kwa iliyokuwa Maabara Kuu ya Mifugo (CVL), Vituo vya Kanda vya Uchunguzi na Utambuzi wa Magonjwa ya Mifugo (VICs), Taasisi ya Utafiti wa Ndorobo (TTRI) Tanga na Kituo cha Utafiti wa Ndorobo (TTRC) Kigoma.
“Shughuri zitakazofanywa kwenye maadhimisho hayo ni pamoja na Uchanjaji wa Mifugo Bure kwa maeneo yatakayobainishwa, Kufanya upimaji wa magonjwa ya Mifugo Bure kwa maeneo yatakayobainishwa, Kutoa Elimu kuhusiana na huduma zinazotolewa na TVLA, Utoaji wa Elimu ya Mifugo, Kutembelea vituo vya watoto yatima na kutoa misaada pamoja na Kufanya Ufunguzi wa Jengo Jipya la Maabara na Ofisi Kituo cha Iringa.” Alisema Dkt. Bura
Dkt. Bura aliongeza kuwa kwa upande wa Kituo cha Iringa kinachohudumia mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Ruvuma, wamepanga Kutembelea wafugaji wa kuku wa asili na kufanya mikutano na wafugaji kwa lengo la kutoa Elimu hususan huduma za upimaji wa mgaonjwa na chanjo. Kufanya upimaji wa magonjwa ya Mifugo Bure kwenye kituo chetu cha zamani kilichopo mtaa wa Boma Manispaa ya Iringa.
Zingine ni uchanjaji wa kuku Bure kwenye kata zitakazotembelewa, Kutoa chanjo ya Ugonjwa wa MDONDO wa kuku kwa wafugaji, kufanya Ufunguzi wa Jengo Jipya la Maabara na Ofisi Kituo cha Iringa pamoja na kuzindua tovuti mpya ya TVLA, Mfumo wa Usajili na Utoaji wa Vibali wa Viuatilifu vya Wanyama pamoja na uzinduzi wa namba ya mawasiliano ya Huduma kwa Mteja.
“Wakala inajivunia mafanikio makubwa iliyoyapata toka kuanzishwa kwake kwani imeongeza mapato yake ya ndani kutoka Shilingi Milioni 220 mwaka 2013/2014 hadi kufikia Shilingi bilioni 3.1 mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 1,409, Uzalishaji na usambazaji wa chanjo kutoka chanjo moja (1) ya Mdondo Mwaka 2013/2014 na hadi chanjo 7 mwaka 2022, Kusogeza huduma za uchunguzi na utambuzi wa magonjwa karibu na wananchi.”
“Mafanikio mengine ni Uboreshaji wa maabara ya kupima ubora wa vyakula vya mifugo, Kushiriki katika utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja, kupata ithibati ya kimataifa (accreditation) katika vipimo 10 vya kimaabara na Kujenga uwezo katika kusajili na kutoa vibali vya viuatilifu vya wanyama.” Alisema Dkt. Bura
Aina 7 za chanjo zinazozalishwa na TVLA ni pamoja na Chanjo stahimilivu joto ya kukinga kuku dhidi ya ugonjwa wa Mdondo, Chanjo ya ugonjwa wa Kimeta, Chanjo ya ugonjwa wa Chambavu, Chanjo ya Homa ya Mapafu ya Ng’ombe, Chanjo ya ugonjwa wa Kutupa Mimba, Chanjo mchanganyiko wa Kimeta na Chambavu pamoja na Chanjo ya Homa ya Mapafu ya Mbuzi.
Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania-TVLA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Dkt.Qwari Bura akitoa taarifa kwa vyombo vya habari (havipo pichani) siku ya tarehe 20/11/2022 kuhusiana maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Wakala na shuguli zitakazofanyika kuanzia tarehe 21/11/2022 hadi tarehe 25/11/2022 kwa lengo kuwafikia wafugaji na kurudisha kile ilichokipata kwa jamii kwenye vituo vyake vyote 11 vilivyopo Tanzania nzima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni