Nav bar

Ijumaa, 25 Novemba 2022

UGAWAJI WA MADUME BORA YA NG’OMBE NI UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MABADILIKO WA SEKTA YA MIFUGO - NDAKI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema ugawaji wa madume ya bora ya ng’ombe ni utekelezaji wa mpango wa mabadiliko wa Sekta ya Mifugo.

 

Waziri Ndaki ameyasema hayo leo (24.11.2022) wilayani Chamwino Mkoani Dodoma wakati alipokuwa anagawa madume bora 50 ya ng’ombe aina ya boran ambapo kila mmoja ana uwezo wa kupanda majike 25 kwa mwaka, kwa vikundi vya wafugaji kwa lengo la kwenda kuboresha mifugo yao ambayo mingi ni ya asili.

 

“Mifugo mingi iliyopo hapa nchini ni ya asili na uzalishaji wake wa nyama na maziwa kwa mfugo ni ndogo, hivyo kwa kuanza kuboresha mifugo kwa kutumia madume haya pamoja na njia ya uhimilishaji kutasaidia wafugaji kuwa na mifugo michache ambayo itakuwa na uzalishaji mkubwa wa nyama na maziwa,” Alisema

 

Ng’ombe wa asili huzalisha nyama kilo 80 -120 kwa ng’ombe wakati baada ya kuboreshwa kwa kosaafu mfugaji anaweza kupata kilo 150 – 200 kwa ng’ombe. Lakini pia kwenye upande wa maziwa ng’ombe hawa walioboreshwa kosaafu huwa na uwezo wa kutoa kati ya lita 5 – 10 za maziwa na hivyo kumfanya mfugaji apate tija zaidi tofauti na mfugaji wa ng’ombe wa asili.

 

Wafugaji wametakiwa kuyatunza madume hayo kwa kufuata taratibu zote wanazoelekezwa na wataalam wa mifugo.  Lakini pia Waziri Ndaki amevitaka vikundi ambavyo vimepatiwa madume hayo kuyatumia kwa kushirikiana na wafugaji wengine ili kuhakikisha tija inapatikana kwa wafugaji ndani ya Wilaya ya Chamwino.

 

Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza amesema Wizara inaendelea kutekeleza mpango wa mabadiliko wa sekta hiyo ambapo licha ya kazi ya uboreshaji wa kosaafu inayoendelea, wafugaji wanaendelea kupatiwa elimu kuhusu malisho ya mifugo.

 

Wizara inaendelea kuanzisha mashamba darasa ya malisho ya mifugo kwa lengo la kutoa elimu ya kilimo cha malisho na namna ya kuyatunza malisho hayo pamoja na nyanda za malisho ili malisho hayo yaweze kuwasaidia wakati wa kiangazi kikali.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Gift Msuya amesema kuwa uongozi wa Wilaya utakwenda kusimamia utekelezaji wa mpango wa mabadiliko wa sekta ya mifugo kwa kuhakikisha madume hayo yaliyogawiwa kwenye vikundi yanatunzwa na kutumika ili kuboresha kosaafu.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Sekta ya Mifugo, Bw. Stephen Michael amesema kuwa takribani asilimia 97 ya ng’ombe waliopo nchini ni wa asili hivyo katika kutekeleza mpango wa mabadiliko wa sekta, Wizara imepanga kununua mitamba 1,160,000 ambayo itapelekwa kwenye mashamba ya serikali. Hivyo kutokana na uzalishaji wake wafugaji wataweza kupata ng’ombe bora hapa nchini badala ya kutegemea kuagiza kutoka nje.

 

Aidha, Wizara inaendelea na zoezi la uhimilishaji mifugo ambapo tayari imeshapanga kuhimilisha takribani ng’ombe 373,000 katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwenye maeneo ambayo hawatapata madume hayo.

 

Mwakilishi wa taasisi ya PASS Trust, Langelika Kalebi amesema kuwa taasisi hiyo ni mwezeshaji ikichochea maendeleo kwenye kilimo (mifugo, uvuvi, mazao, na mazao ya porini). Taasisi hiyo ipo nchi nzima ikichochea maendeleo kwenye upatikanaji wa mitaji na elimu, hivyo wanaongezea dhamana katika kurahisisha upatikanaji wa mitaji kwa mtu mmoja, vikundi, vyama vya ushirika.

 

Naye mwenyekiti wa wafugaji Wilaya ya Chamwino, Bw. John Kochocho ameishukuru serikali kupitia Sekta ya Mifugo kwa kuwapelekea wafugaji madume hayo ya ng’ombe yatakayokwenda kuboresha kosaafu na hivyo kuwafanya wazalishe kwa tija na kibiashara.

 

Serikali ya awamu ya sita ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanikiwa kununua jumla ya madume bora ya ng’ombe wa nyama 366 aina ya Boran kama sehemu ya jitihada za kuendelea kuboresha tija ya ng’ombe tulionao nchini.


Baadhi ya Wafugaji na Viongozi wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati wa hafla ya kugawa Madume bora 50 ya ng’ombe aina ya boran kwa Vikundi vya wafugaji katika wilayani Chamwino Mkoani Dodoma. (24.11.2022)


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wafugaji pamoja na viongozi wakati wa hafla ya kugawa madume bora 50 ya ng’ombe aina ya boran kwa Vikundi vya wafugaji katika wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma ambapo aliwataka wafugaji hao kuhakikisha wanayatunza madume hayo ili lengo la serikali la kuboresha kosaafu liweze kutimia na wafugaji waweze kuwa na mifugo michache yenye tija. (24.11.2022)


Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza akiuelezea mpango wa mabadiliko wa Sekta ya Mifugo wakati wa hafla ya kugawa Madume bora 50 ya ng’ombe aina ya boran kwa Vikundi vya wafugaji katika wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, ambapo amesema Wizara imepanga kuanzisha mashamba darasa ya kilimo cha malisho kwa lengo la kuwaelimisha wafugaji juu ya kilimo hicho, utunzaji wa malisho na nyanda za malisho ili waweze kukabiliana na tatizo la malisho wakati wa kiangazi kikali. (24.11.2022)


Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko (WMUV), Bw. Stephen Michael akiwaeleza wafugaji kuhusu mpango wa Wizara wa kuhimilisha ng’ombe 373,000 katika mwaka wa fedha 2022/2023, hivyo kwa wafugaji ambao hawatafikiwa na madume bora watapatiwa huduma ya uhimilishaji. Amewaeleza hayo wakati wa hafla ya kugawa Madume bora 50 ya ng’ombe aina ya boran kwa Vikundi vya wafugaji katika wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma. (24.11.2022)


Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Gift Msuya akitoa salam za wilaya ameishukuru Wizara kwa kuamua kupeleka madume bora 50 ya ng’ombe katika wilaya hiyo na kwamba uongozi wa wilaya utakuwa ukifanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha tija ya uwepo wa madume hayo inaonekana kama ilivyokusudiwa na serikali. Mhe. Msuya ameyasema hayo wakati wa hafla ya kugawa Madume bora 50 ya ng’ombe aina ya boran kwa Vikundi vya wafugaji katika wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma. (24.11.2022)


Meneja wa Taasisi ya PASS Trust kutoka Mwanza, Bi. Langelika Kalebi akizungumza na wafugaji wakati wa hafla ya kugawa Madume bora 50 ya ng’ombe aina ya boran kwa Vikundi vya wafugaji katika wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma. (24.11.2022)


Mwenyekiti wa Wafugaji Wilaya ya Chamwino, Bw. John Kochocho akitoa neno la shukrani kwa Sekta ya Mifugo mara baada ya kukabidhi Madume ya Ng’ombe wakati wa hafla ya kugawa Madume bora 50 ya ng’ombe aina ya boran kwa Vikundi vya wafugaji katika wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma. (24.11.2022)


Baadhi ya Wafugaji na Viongozi wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati wa hafla ya kugawa Madume bora 50 ya ng’ombe aina ya boran kwa Vikundi vya wafugaji katika wilayani Chamwino Mkoani Dodoma. (24.11.2022)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni