Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
leo Mei 13, 2024 amezindua na kushuhudia makabidhiano ya Kituo Atamizi cha
Ufugaji wa Kibiashara kwa Vijana, baina ya Taasisi ya PASS TRUST na Taasisi ya
Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI)kilichopo Kongwa mkoani Dodoma.
Akizungumza baada ya
makabidhiano ya kituo hicho, ambacho kinathamani ya shilingi bilioni 1.63
ikijumuisha uwekezaji wa vifaa na mindombinu, Mheshimiwa Majaliwa ameagiza
uwekezaji utunzwe ili taifa liweze kunufaika kupitia uwezeshwaji wa vijana.
Mheshimiwa Majaliwa amesema
kuwa lengo la mradi huo ni kuwapatia vijana ujuzi kwa vitendo ikiwemo elimu ya
ujenzi wa mabanda, ulishaji, matibabu na usimamizi wa mbuzi lakini pia kutoa
mafunzo ya biashara ili vijana waweze kuwa wajasiriamali na kuendeleza biashara
ya unenepeshaji mbuzi.
Kwa upande wake, Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa hadi kufikia Aprili 2024,
ongezeko la mauzo ya nyama nje ya nchi limefikia takribani shilingi bilioni 100
ambapo nyama ya mbuzi imeendelea kuongoza kwa kuchangia asilimia 70.1 ya mauzo
yote, hivyo kituo hicho cha unenepeshaji wa mbuzi kitaendelea kuchaguza kwenye
biashara ya nyama kupitia shughuli ya unenepeshaji wa mbuzi utakaokuwa
ukifanywa na vijana hao.
Aliongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga
kukifanya Kituo Atamizi cha Ufugaji
kilichopo Kongwa kuwa kituo kikubwa kwa ajili ya ufugaji na unenepeshaji wa
mbuzi nchini.
Kituo hicho kilichokuwa kikisimamiwa na
Taasisi isiyo ya kiserikali ya PASS kimekabidhiwa kwa Serikali na kitakuwa chini
ya uangalizi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni