Nav bar

Alhamisi, 30 Mei 2024

WATUMISHI WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI WATAKIWA KUWAJIBIKA NA KUWA WAADILIFU

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amewataka watumishi wa wizara hiyo kuwa na uwajibikaji na uadilifu katika makujumu yao ya kuwatumikia wananchi.

Mhe. Mnyeti amebainisha hayo leo (10.05.2024) jijini Dodoma, wakati alipokuwa akihutubia wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kufafanua kuwa ana imani kubwa na watumishi wa wizara hiyo na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwa na uzalendo.

Ameongeza kuwa katika uwajibikaji na uadilifu watumishi wa wizara hiyo wanatakiwa kutojiingiza kwenye matukio ya matumizi mabaya ya ofisi na kuhakikisha wanazidi kuwatumikia wananchi kwa kiwango kikubwa hususan wafugaji na wavuvi ambao wengi wao wanaishi vijijini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza hilo, amesema kikao hicho kimetoka na maazimio tisa ambapo pia wajumbe wameridhia Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2023/2024 na Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2024/2025 kusomwa bungeni.

Aidha, Prof. Shemdoe akijibu hoja mbalimbali kutoka kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la wizara hiyo, amesema uongozi unaendelea kutatua changamoto mbalimbali mahali pa kazi ikiwemo kuongeza vitendea kazi.

Pia, amesema wizara itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi na kuwajengea mazingira bora zaidi ya kufanyia kazi kwa kuwa wamekuwa wakitumia muda mwingi kuwa kazini.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede amewataka watumishi wa wizara hiyo kuwa tayari kuwajibika na kutekeleza bajeti ya wizara mara baada ya kusomwa na kupitishwa bungeni.

Akisoma taarifa ya hoja na maoni ya watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) – Tawi la wizara hiyo Bw. Silas William, ameomba uongozi wa wizara kuangalia kwa ukaribu baadhi ya changamoto zinazowapata watumishi waliopo kazini na ambao wanastaafu ili kuondokana na usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza.

Bw. William amesema watumishi wa wizara wataendelea kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kila siku kwa kuwahudumia wananchi kwa miongozo ya sheria na kanuni za utumishi wa umma ili waweze kufikia malengo ya serikali ya kukuza sekta za mifugo na uvuvi.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi walipata pia fursa ya kuuliza maswali na kuchangia hoja mbalimbali na wote kwa pamoja kukubaliana na maazimio tisa kwa ajili ya kufikia malengo ya baraza hilo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akiwahutubia wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kufafanua kuwa ana imani kubwa na watumishi wa wizara hiyo na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwa na uzalendo. Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma na kukubaliana maazimio tisa likiwemo la kuridhia Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2023/2024 na Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2024/2025 kusomwa bungeni. (10.05.2024)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la wizara hiyo, akifafanua hoja mbalimbali na kutoa taarifa ya maazimio tisa kwenye kikao cha baraza kilichofanyika jijini Dodoma. (10.05.2024)

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede amewataka watumishi wa wizara hiyo kuwa tayari kuwajibika na kutekeleza bajeti ya wizara ya mwaka 2024/2025 mara baada ya kusomwa na kupitishwa bungeni. Dkt. Mhede amebainisha hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la wizara hiyo. (10.05.2024)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni