Wananchi wanaojishughulisha na uvuvi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika wameunga mkono hatua ya serikali ya kupumzisha shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika ili kulipa nafasi ziwa kuongeza kiwango chake cha uzalishaji wa samaki.
Wananchi hao waliunga mkono
hatua hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi vizimba vya kufugia samaki, boti za
kisasa za uvuvi na doria na pia kupata elimu na uelewa kuhusu upumzishaji wa
shughuli za Uvuvi Ziwa Tanganyika iliyofanyika katika Mwalo wa Katonga, mkoani
Kigoma Mei 9, 2024.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wawakilishi wa wananchi, akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Kilumbe
Ng’enda alisema kuwa muda ambao umepangwa ziwa kupumzishwa ni muafaka kwa
sababu kipindi hicho ni maarufu kwa jina la ‘kilimia’ ambapo ziwa huwa
linajifunga lenyewe na kufanya kupungua kwa Mazao ya samaki.
Aliongeza kwa kueleza kuwa,
kwa muda mrefu sasa wavuvi wamekuwa wakitumia vifaa vyao na mafuta kwenda mbali
bila mafanikio yoyote kwa sababu samaki wamepungua sana ziwani, hivyo
kupumzisha ziwa kutasaidia samaki kuongezeka na hivyo wavuvi wataweza kupata
mavuno mengi zaidi baada ya ziwa kufunguliwa.
Naye, Mbunge wa Kigoma
Kusini, Mhe. Nashon Bidyanguze alisema kuwa mwanzoni walikuwa wanapinga
kufungwa kwa ziwa kwa sababu wananchi walikuwa hawana elimu ya kufungwa kwa
ziwa lakini sasa hawawezi kuendelea kupinga kwa sababu tayari serikali
imepeleka boti na vizimba kwa ajili ya wananchi kutumia kufuga samaki katika
kipindi ambacho ziwa litakuwa limefungwa.
Wakati akikabidhi boti na vizimba kwa wanufaika wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Tanganyika, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Boti na Vizimba hivyo ili wananchi watumie kufugia samaki kama njia mbadala ya kujipatia kipato katika kipindi ambacho ziwa litakuwa limepumzishwa.
Aidha, Waziri Ulega
amewataka wanufaika wa boti hizo na wengine wote wanaoendesha shughuli za Uvuvi
Ziwa Tanganyika na Nyasa kutumia zana hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, huku
akiwaelekeza maafisa uvuvi wa ukanda wa ziwa Tanganyika kutotumia kipindi hicho
kuwasumbua wavuvi hususani wavuvi wadogo badala yake waendelee kuwaelimisha ili
waweze kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wote wa zoezi hilo.
Katika hafla hiyo, Waziri
Ulega amekabidhi vizimba 29 kwa vikundi
sita na watu binafsi 16 na Boti 6 kwa ajili ya uvuvi na doria katika mikoa ya
Kigoma, Katavi na Rukwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni