Nav bar

Alhamisi, 30 Mei 2024

WAVUVI WATAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUKABILIANA NA UPOTEVU WA MAZAO YA UVUVI


Naibu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Edwin Mhede amewataka wadau wa uvuvi kuhakikisha wanatumia teknolojia za kisasa ambazo ni rahisi zitakazowezesha kukabiliana na changamoto ya upotevu wa mazao ya Uvuvi.

Ameyasema hayo Mei 28, 2024 wakati akifungua mkutano wa Uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech Superhighway ambao utachukua takribani miaka 7 (2024-2030) wenye lengo la kusaidia juhudi za Serikali katika kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi.

Mkutano huo ambao umezikutanisha nchi nne Afrika, Dkt. Edwin Mhede amesema wamejielekeza kuhakikisha wanufaika wa mradi huo wanakuwa ni wavuvi wenyewe.

Pia amesema eneo ambalo wanalifanyia kazi kwa kushirikiana na Worldfish pamoja na Taasisi za ndani  ni kuhakikisha wanakabiliana na changamoto za upotevu wa mazao ya uvuvi, pamoja na uharibifu mbalimbali unaojitokeza kwenye mnyororo wa thamani wakati watu wakivua, wakisafirisha, wakiuza na kununua samaki.

"Katika kutathimini fikra mpya za nini kifanyike zaidi ya hiki, tumejielekeza kuyagusa matatizo ya wavuvi na kujielekeza katika kufanya hivyo kuhakikisha kwamba mradi huu wanaofaidika ni wavuvi wenyewe"

"Ni matumaini yangu baada ya siku kadhaa tutakuja kuwa na kitu kikubwa sana kuweza kutusaidia kuyafikia maisha ya wengi ambayo ndiyo maelekezo lakini pia ndiyo maono ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunaenda kuyakuta mahitaji ya watu na tunayafanyia kazi" amesema

Dkt. Mhede amesema changamoto nyingine zinazowakabili wavuvi hao, ni pamoja na uduni wa Teknolojia , upatikanaji masoko, upatikanaji wa mitaji ya kifedha na maarifa lakini pia miundombinu

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh, amesema Afrika ikiwemo Tanzania kunatatizo kubwa la upotevu wa mazao ya uvuvi ambapo inakisiwa kati ya asilimia 30-40 ya upotevu wa mazao hayo yanatokana na mabadiliko ya tabianchi

"Katika kipindi cha mvua inakua ni changamoto kubwa kwa wavuvi wetu hasa wale ambao wanachataka na wanasafirisha mfano, wavuvi wa dagaa wanavua na kuchakata, wanahitaji pia teknolojia mpya kwa ajili ya kusafirisha mazao yao ya uvuvi" amesema Prof. Sheikh.

Prof. Sheikh amesema Serikali ya awamu ya sita imeendelea na jitihada za kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wa mazao hivyo amewaomba wadau mbalimbali kuweka mbinu bora ambazo zitawasaidia wavuvi kuweza kuhifadhi mazao yao ambayo yatakubalika ndani na nje ya nchi.

Naye Kiongozi wa Mawasiliano ya Kimataifa wa Taasisi ya WorldFish, Rajita Majumdar amesema kuwa zaidi ya tani 21.3 za samaki zimepotea kutokana na changamoto ya uhifadhi wa mazao hayo baada ya kuvuliwa ambapo wameona ni vyema kuja nchini kuungana na  Serikali na wavuvi kwa lengo la kupunguza upotevu huo ambao unafifisha uchumi.

"Nadhani inahitajika matumizi ya teknolojia nafuu inayoweza kufikiwa ili kuongeza umahiri katika kushughulikia mnyororo wa usambazaji wa chakula ambapo itasaidia kuondokana na uharibifu mkubwa"amesema

Aditya Parmar ambaye ametoka kwenye Taasisi ya WorldFish, amesema mradi huo umejikita katika  vipengele vinne ambavyo ni  usambazaji wa samaki, uuzaji, utunzaji, uhifadhi na usafirishaji ambapo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutunza thamani ya ubora wa chakula kwa lengo la kuhakikisha lishe bora kwa jamii ya Pwani.

"Tunataka kuona jumuiya ya Pwani jinsi gani inaweza kuongeza mapato, tunataka kushirikisha wanawake na vijana kutekeleza mradi huu ambao tunatarajia utabadilisha maisha yao baada ya miaka michache ijayo "amesema

Mkutano huo unafuatiwa na mkutano ambao utafanyika Tarehe 5-7 mwezi Juni  mwaka huu katika ukumbi wa Mikutano Mlimani city Jijini Dar es Salaam ambao unazungumzia mahsusi wavuvi wadogo wanaochangia kwa asilimia 95.


Naibu katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akiongea wakati wa kufungua mkutano wa  uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech Superhighway ambao utachukua takribani miaka 7  wenye lengo la kusaidia juhudi za serikali katika   upotevu wa mazao ya uvuvi., Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa hotel ya Ramada jijini Dar es Salaam Mei 28,2024

Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohamed Sheikh akiongea wakati wa  uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech Superhighway ambao utachukua takribani miaka 7  wenye lengo la kusaidia juhudi za serikali katika   upotevu wa mazao ya uvuvi., Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa hotel ya Ramada jijini Dar es Salaam Mei 28,2024

Mwakilishi kutoka kwenye Taasisi ya WorldFish Bw. Aditya Parmar akiwasilisha mada wakati wa mkutano wa uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech Superhighway   na kuelezea vipengele vinne ambavyo mradi huo umejikita  ikiwa ni pamoja na  usambazaji wa samaki, uuzaji, utunzaji, uhifadhi na usafirishaji ambapo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutunza thamani ya ubora wa chakula kwa lengo la kuhakikisha lishe bora kwa jamii, Mei 28,2024 jijini Dar es salaam.

Naibu katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Edwin Mhede akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya wadau wa Sekta ya Uvuvi walioudhuria mkutano wa  uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech Superhighway ambao utachukua takribani miaka 7  wenye lengo la kusaidia juhudi za serikali katika   upotevu wa mazao ya uvuvi., Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa hotel ya Ramada jijini Dar es Salaam Mei 28,2024


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni