Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza mchakato wa kufanya Utafiti wa kina juu ya chanzo cha tope maji yatokayo katika ardhi ndani ya mnada wa Mhunze Wilayani Kishapu ikiwa ni njia mojawapo ya kujua athari zinazoweza kujitokeza kutokana na uwepo wa hali hiyo katika eneo la ujenzi ambao unaendelea katika Mnada huo ili kuweza kutafuta suluhisho. Hii ni kufuatia hali hii kuleta taharuki kwa wafugaji na wauzaji wa mifugo kwenye mnada huo.
Akizungumza, leo Mei 29,
2024 Wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga wakati akienda kukagua hali ya eneo la
mnada wa Mhunze, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof.
Daniel Mushi amesema Wizara imeamua kufanya Utafiti wa kina ili kujiridhisha
kama hali ya mnada wa Mhunze ni salama na kukabiliana na uwepo wa tope kwa
ajili ya kuhakikisha usalama wa watu na mifugo kwenye mnada huo.
"Leo tumekuja na
wataalam kutoka Taasisi ya madini Tanzania kwa ajili ya kupima kilichotokea na
kutupa taarifa, ambapo mpaka sasa wameshafanya uchunguzi wa awali na
wametueleza kisayansi ni kitu gani kina sababisha matope haya na kutuhakikishia
kwamba mradi wa ujenzi wa ukuta unaozunguka eneo hili na maboresho mengine
yanaweza kuendelea", amesema Prof. Mushi.
Aidha, Prof. Mushi alisema
Wataalamu watakapofanya uchunguzi wa kina wataeleza namna ya kukabiliana na
suala hili ili yasijitokeze madhara na wataalamu wameihakikishia Wizara kuwa
hakuna madhara yanayoweza kusababisha maafa katika mnada huo wa Mhunze.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude amesema mbali na utafiti huo lakini pia
yapo marekebisho na maboresho yanayotarajiwa kufanywa kwenye eneo hilo la mnada
na maeneo ya pembezoni ili kujihakikishia usalama wa wananchi na mifugo.
Vilevile Mhe. Mkude
ameishukuru sana Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuja kwa wakati na watafiti ili
kufanya utafiti baada ya kusikia jambo
hili la kufurika kwa tope katika mnada wa Mhunze.
Akitoa ufafanuzi juu ya
suala hilo la kufurika kwa tope katika mnada wa Mhunze, Mjiolojia kutoka
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa madini Tanzania, Bw. Sudian Chilagwile
amesema, sababu iliyofanya waitwe na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuja kufanya
uchunguzi kwenye eneo la mnada wa Mhunze ni uwepo wa chemchem ya maji tope na udongo uliojaa
matope ukitoka chini ya ardhi.
Bw. Chilagwile, ameweka bayana kuwa wao kama watafiti watafanya kazi ya Utafiti katika eneo hilo la mnada ili kubaini chanzo, japo utafiti wa awali wa kisayansi unaonyesha sababu ya yote ni uwepo wa mvua nyingi ambazo zimeleta athari katika miamba iliyopo aridhini ambayo imesababisha uwepo wa tope hilo, na kubainisha kuwa jambo hili haliwezi kuathiri shughuli za mnada huo kuendelea, ila watatoa ushauri kwa Wizara na wakandarasi juu ya ukarabati wa eneo hilo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Prof. Daniel Mushi, akizungumza katika kikao kifupi na Mkuu wa
Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude (hayupo pichani), baada ya kufika Ofisi ya
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, kwa ajili ya kujitambulisha na kuelezea nia na
dhumuni la kufika kwake na ujio wake na Timu ya maafisa toka Wizara ya Mifugo
na Uvuvi pamoja na wanajiolojia kwa ajili ya kufanya Utafiti juu ya uwepo wa
tope maji katika mnada wa Mhunze, kikao kimefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya ya Kishapu, leo Mei 29, 2024, Shinyanga.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Prof. Daniel Mushi (katikati), akimuahidi Mkuu wa Wilaya ya
Kishapu, Mhe. Joseph Mkude (kushoto), kushirikiana nae bega kwa bega katika
kutatua changamoto iliyopo na kufuata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa watafiti,
wakati alipofika katika mnada wa Mhunze Wilayani Kishapu kujionea hali ilivyo,
leo Mei 29, 2024, Shinyanga.
Pichani ni sehemu eneo la
mnada wa Mhunze lililo athiriwa na tope maji, Wilayani Kishapu - Shinyanga
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni