Serikali kupitia Wizara ya
Mifugo na Uvuvi leo Mei 22, 2024 imeanza kutoa mafunzo ya siku 3 kwa Wakaguzi
wa mifugo na mazao yake waliopo kwenye vituo mbalimbali vya ukaguzi ikiwa ni
pamoja na vile vilivyopo kwenye mipaka yote nchini zoezi litakalofanyika mkoani
Morogoro.
Akifungua Mafunzo hayo
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege amewataka
wataalam hao mbali na kutumia vema taaluma zao, wazingatie weledi na watende
haki wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuomba
ushauri pale wanapopata changamoto.
“Tunapokuwa kule kwenye
vituo vyetu vya ukaguzi tunapaswa kujua sisi ndio sura ya Wizara kwa hiyo
tunavyowapokea wageni, tunavyoongea nao na tunavyotoa huduma zetu kuna athari
kubwa sana kwa viongozi wetu wanaotusimamia hivyo tunaweza kuwachafua au
kuwajengea sifa njema” Ameongeza Dkt. Lutege.
Aidha Dkt. Lutege ametoa
angalizo kwa vijana hao kuacha kutanguliza mbele maslahi yao wakati
wakitekeleza majukumu vituoni ili kuendelea kujenga dhana ya uaminifu na uadilifu
jambo litakalolinda taswira ya Wizara na Serikali kwa ujumla.
“Akifika Mteja umemkamata,
unatakiwa kumueleza makossa yake kwa moyo mweupe kabisa na kwa lugha stahiki
bila kutumia nguvu au lugha chafu kisha na yeye umpe nafasi akueleze sababu
zake na baada ya hapo upime kwa taaluma yako uone kama alichofanya ni kosa la
kukusudia au la ndipo ufanye maamuzi” Amesisitiza Dkt. Lutege.
Kwa Upande wake Mratibu
wa Mradi wa Mfumo wa Usalama wa Wanyama,
Mimea na Chakula ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia, Habari na
Mawasiliano kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Baltazar Kibola amesema kuwa
mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wataalam hao kufahamu kuhusu Afya ya wanyama na mazao yake kabla hawajatoa vibali
kupitia mfumo wa utoaji vibali vya Mifugo na Mzao yake kielektroniki (MIMIS).
Naye Mratibu wa Mradi huo
kutoka Shirika la “TradeMark Africa” ambao ndio wafadhili wakuu wa Mafunzo hayo
Bi. Kezia Mbwambo ameeleza kuwa Shirika lake liliona umuhimu wa wataalam hao
kujengewa uwezo kuhusu masuala ya usalama wa mifugo na mazao yake ili kulinda
afya za Mifugo na watumiaji wa mifugo hiyo kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya
wataalam wenzake, Afisa Mfawidhi wa kituo cha Ukaguzi wa Mifugo na Mazao yake
Wilaya ya Temeke Bi. Mwajuma Chaurembo amelishukuru Shirika hilo kwa kuwajengea
uwezo kupitia mafunzo hayo ambapo ameahidi kufanyia kazi kwa vitendo yote
watakayojifunza kwa siku zote tatu.
Mafunzo hayo yanafuatia
mafunzo ya awali yaliyodhaminiwa na Shirika la “TradeMark Afrika” na kuratibiwa
na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Kitego chake cha Teknolojia, Habari na Mawasiliano ambayo
yalihusu mfumo wa utoaji wa Vibali vya Mifugo na Mazao yake kielektroniki
(MIMIS).
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma
za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege (kulia) akifungua mafunzo ya wakaguzi wa
Mifugo na Mazao yake vituoni na mipakani Mei 22, 2024 mkoani Morogoro. Katikati
ni Mratibu wa Mradi unaosimamia Mafunzo hayo kutoka Shirika la "Trade
Africa" Bi. Kezia Mbwambo na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Bw. Baltazar Kibola.
Pichani ni wakaguzi wa
Mifugo na Mazao yake vituoni na mipakani wakiwa kwenye Mafunzo yanayohusu afya
ya wanyama na mazao yake Mei 22, 2024 mkoani Morogoro.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma
za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege (wa nne kutoka kulia mbele) na baadhi ya
Viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwa kwenye picha ya
pamoja na wakaguzi wa Mifugo na mazao yake vituoni na mipakani mara baada ya
kufungua mafunzo kwa wakaguzi hao Mei 22, 2024 mkoani Morogoro.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni