Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya kutafsiri ndoto
halisi ya wingi wa mifugo nchini katika kubadilisha mfumo wa maisha kwa
watanzania kupitia sekta hiyo.
Akizungumza (21.05.2024)
wakati wa hafla fupi ya kuwaonesha vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji
mifugo kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), inayosimamiwa
na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, vitalu watakavyopatiwa kwa ajili ya ufugaji
katika Ranchi za Kagoma na Kitengule zinazosimamaiwa na Kampuni ya Ranchi za
Taifa (NARCO), Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. Julius Laizer amesema Mhe. Rais
ameweza kuirasimisha rasmi biashara ya mazao ya mifugo kwa kuwa Sekta ya Mifugo
ni muhimu katika maisha ya binadamu.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa
wa Kagera, Mhe. Laizer amesema ni vigumu kutenganisha biashara yoyote inayohusu
chakula cha binadamu isifanikiwe, hivyo kuwataka vijana wa BBT – LIFE kusimamia
vyema ndoto na maono ya Mhe. Rais kwa kuwa wapo sehemu sahihi katika kujifunza
na kufuga mifugo kibiashara.
Kwa upande wake Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi amesema
wizara inawaangalia vijana hao kama waleta mapinduzi kwenye Sekta ya Mifugo
hivyo imeamua kuwaunganisha na baadhi ya benki zilizopo nchini kupata fursa za
mikopo.
Ameongeza kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alianzisha programu hiyo kwa kwa kuitambua Sekta ya Mifugo kama sekta rasmi na kuwaingiza vijana kwenye ufugaji na uvuvi wa kibiashara na kwamba kila mwaka takriban vijana 1,600 wanahitimu kwenye vyuo mbalimbali vya mifugo hivyo serikali imeona haiwezi kuwaacha bila ajira bali wajifunze ufugaji kibiashara.
Aidha, amesema Mhe. Rais
katika diplomasia ya kiuchumi amekuwa akizunguka nchi mbalimbali kutafuta
masoko ya mazao ya mifugo na uvuvi ambapo kwa sasa nchi inahitaji wawekezaji
wakubwa katika sekta hizo ili kuvipatia viwanda vilivyopo nchini mifugo kwa
ajili ya kuchakatwa na kuhudumia masoko ya kimataifa, ambapo pia vijana wa BBT
- LIFE wanatakiwa kuwa wawekezaji wakubwa katika Sekta ya Mifugo.
Pia, Kaimu Mkurugenzi Mkuu
wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Bw. Bwire Mujarubi amesema kwa mujibu wa
mwongozo kampuni hiyo imepewa majukumu ya kutenga vitalu kwa vijana wa BBT -
LIFE, kupanga vijana hao kwenye vitalu, kuwapatia mikataba wafugaji katika ranchi
za NARCO na kuwa miongoni mwa wateja wa mifugo kutoka kwa vijana wa BBT - LIFE
watakaopatiwa vitalu katika ranchi hizo.
Amesema licha ya awamu ya
kwanza ya BBT - LIFE kuelekea mwishoni ifikapo Tarehe 30 Mwezi Juni mwaka huu,
NARCO itaendelea kuwalea vijana hao 161 ambapo kila mmoja atapatiwa hekari 10
bila kulipa gharama za upangaji katika kipindi cha miaka mitano kwenye ranchi
za Kagoma hekta 311 na Kitengule hekta 2,000 zilizopo Wilaya ya Karagwe Mkoani
Kagera.
Kwa upande wake Mtendaji
Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Dkt. Pius Mwambene amesema
kwa kipindi cha miaka miwili ambacho vijana wa BBT – LIFE wamekuwa wakipata
mafunzo katika wakala hiyo wamepata uzoefu mkubwa wa kuandaa miundombinu ya
mifugo pamoja na biashara ya mifugo.
Ameongeza kuwa vijana hao
wakianza rasmi ufugaji hawataangaika na kwamba watakuwa wakishirikiana na
wawekezaji wakubwa waliopo kwenye ranchi za NARCO, huku akibainisha kuwa wakati
wa mafunzo vijana hao wamekuwa wakiuza mifugo ndani ya nchi pamoja na nchi za jirani.
Pia, amesema amesema lengo
la programu hiyo ni kukuza ufugaji wa mifugo wenye tija kwa kuandaa vijana kuwa
wawekezaji wakubwa kwenye sekta hiyo na kwamba programu hiyo kwa sasa
itapelekwa kwenye ngazi za serikali za mikoa ili kuwanufaisha vijana wengi
zaidi.
Mmoja wa vijana
wanaonufaika na programu ya BBT - LIFE Bw. Posper Mugalula amesema wanashukuru
kwa kupata fursa ya kushiriki mafunzo ya unenepeshaji mifugo hususan ng’ombe
baada ya kumaliza elimu ya vyuo na wapo tayari kuingia rasmi katika ufugaji wa
kisasa baada ya kupatiwa vitalu kwenye ranchi za NARCO.
Amewaomba vijana wenzake kushirikiana ili kufikia malengo ambayo serikali imekusudia na kuwa chachu ya vijana wengine kujiunga na mafunzo kwa awamu ya pili na kufuga kibiashara kwa kuwa Sekta ya Mifugo ina soko kubwa ndani na nje ya nchi.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi
imekuwa ikiendesha mafunzo ya unenepeshaji mifugo katika vituo vya Wakala ya
Mifugo nchini (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kupitia
Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE) ili kufikia maono ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha
vijana kufanya ufugaji wenye tija katika sekta za mifugo na uvuvi.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa
wa Kagera, wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika Ranchi ya Kagoma iliyopo
Wilaya ya Karagwe mkoani humo ya kuwaonesha vijana wanaohitimu mafunzo ya
unenepeshaji mifugo kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE),
baadhi ya maeneo watakayopatiwa kwa ajili ya vitalu vya kufugia mifugo, Mkuu wa
Wilaya ya Karagwe Mhe. Julius Laizer amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya kutafsiri ndoto
halisi ya wingi wa mifugo nchini katika kubadilisha mfumo wa maisha kwa
watanzania kupitia sekta hiyo. (21.05.2024)
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi akizungumza na kuwaonesha baadhi ya
vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo awamu ya kwanza kupitia
Programu ya Jenga kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), vitalu watakavyogaiwa kufanya
ufugaji katika Ranchi za Kagoma na Kitengule ambazo ziko chini ya Kampuni ya
Ranchi za Taifa (NARCO) katika Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, ambapo katika
kipindi cha miaka mitano hawatatozwa malipo ya upangaji katika ranchi hizo.
(21.05.2024)
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi (mwenye kofia nyeusi) akizungumza
na baadhi ya wadau na vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo awamu
ya kwanza kupitia Programu ya Jenga kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), wakati
vijana hao wakioneshwa vitalu watakavyogaiwa kufanya ufugaji katika Ranchi za
Kagoma na Kitengule ambazo ziko chini ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO)
katika Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, ambapo jumla ya vijana 161 watapatiwa
vitalu ambapo kila mmoja atapatiwa hekari 10. (21.05.2024)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni