Serikali kupitia Wizara ya
Mifugo na Uvuvi imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 10.5 kwa ajili ya mitaji ya
miradi ya vijana ili kuwainua kiuchumi.
Naibu Waziri Ofisi ya
Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi amebainisha
hayo (24.05.2024) jijini Mwanza, wakati wa kuhitimisha mafunzo kwa vitendo ya
uvuvi na ukuzaji viumbe maji awamu ya pili kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo
Bora (BBT – LIFE) ambayo imewejenga katika kujiajiri kupitia Sekta ya Uvuvi.
Mhe. Katambi amempongeza
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) pamoja na viongozi wengine
wa wizara kwa kusimamia vyema maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza ajira kwa vijana kupitia sekta za
mifugo na uvuvi.
Ameongeza kuwa ni wakati
sasa kwa vijana kutumia vyema fursa zitokanazo na sekta hizo ili kujipatia
ajira na utajiri pamoja na kufuga kisasa na kuuza mazao ya mifugo na uvuvi
yakiwa katika ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema zaidi ya vijana 300
wamenufaika kupitia mafunzo hayo ya miezi mitatu kupitia vituo mbalimbali.
Prof. Shemdoe ameongeza
kuwa lango la mafunzo hayo ni kuwezesha vijana kuwa wajisiriamali na wawekezaji
kwenye shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji kwa kuwajengea ujuzi
utakaowawezesha kubuni miradi na kuanzisha vikundi au kampuni ili waweze
kujiajiri na kutoa fursa za ajira kwa wenzao.
Amebainisha kuwa awamu ya
pili ya wigo wa mafunzo hayo imeongezeka tofauti ya awamu ya kwanza ambapo
yalipokelewa maombi zaidi ya 1,200 ambapo inaashiria vijana wana ari ya
kujiunga katika mafunzo hayo ya vitendo ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi na
Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) zinahitaji kuweka
nguvu zaidi katika kuwawezesha vijana kujiajiri.
Kwa upande wake mmoja wa
wanufaika wa BBT – LIFE akisoma risala kwa niaba ya vijana wenzake Bw. Muhsin
Mussa amesema katika mafunzo hayo wamejifunza namna ya utunzaji wa fedha,
kuunda na kusajili vikundi, maandiko ya miradi na namna ya kuiendesha pamoja na
mafunzo ya vitendo kwa vijana wa Tanzania Bara na Visiwani.
Aidha, amesema mafunzo hayo
wanaamini yataenda kupunguza wingi wa vijana wasio na ajira ambapo sasa
wataweza kujishughulisha na uvuvi pamoja na ukuzaji viumbe maji kibiashara.
Naibu Waziri Ofisi ya
Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi (mwenye tai
nyekundu) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe
(kulia kwake) wakiangalia moja ya vizimba vya kufugia samaki, wakati wa
kuhitimisha mafunzo kwa vitendo ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji awamu ya pili
jijini Mwanza kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE).
(24.05.2024)
Naibu Waziri Ofisi ya
Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi (mwenye tai
nyekundu) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe
(kulia kwake) wakiangalia moja ya vizimba vyenye uwezo wa kufuga samaki
takriban 100 na kisichogharimu zaidi ya Shilingi Laki Moja kwa ajili ya
matengenezo yake, wakati wa kuhitimisha mafunzo kwa vitendo ya uvuvi na ukuzaji
viumbe maji awamu ya pili jijini Mwanza kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo
Bora (BBT – LIFE). (24.05.2024)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni