Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amewataka wadau wote wanaosimamia ustawi na haki za
wanyama kukemea vikali vitendo vitakavyosababisha kutoweka kwa Punda ili
wanyama hao waendelee kuwasaidia wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii
na kiuchumi.
Mhe. Mnyeti ametoa rai hiyo
Mei 17, 2024 alipokuwa akifunga Maadhimisho ya siku ya Punda Afrika Mashariki
ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Dodoma yakitanguliwa na shughuli mbalimbali
ikiwemo mijadala iliyolenga kuchukua hatua mbalimbali za kunusuru kutoweka kwa
mnyama huyo.
“Punda wamekuwa wakifanya
kazi kubwa na muhimu sana katika sekta za kiuchumi ambapo katika shughuli za usafiri hivi sasa wamekuwa
wakitumika mpaka kubeba vifaa vya ujenzi na siku za hivi karibuni tumeshuhudia
wakibeba madini katika migodi mbalimali nchini” Ameongeza Mhe. Mnyeti.
Aidha Mhe. Mnyeti
amebainisha kuwa kutokana na umuhimu wa ngozi na viungo vingine vya mnyama huyo
ongezeko la uchinjaji wa wanyama hao lilikuwa kubwa hali iliyosababisha tishio
la kutoweka kwao Afrika na ulimwenguni kwa ujumla.
“Serikali imechukua hatua
mbalimbali ili kudhibiti kutoweka kwa wanyama hawa ikiwa ni pamoja na kusitisha
shughuli za uchinjaji wake na biashara ya ngozi zake zilizokuwa zikiendeshwa
kwa leseni ya muda ya kampuni ya Fan-Hu kutoka China na kama tungekiacha
kiwanda hiki kiendelee kufanya kazi kwa miaka miwili basi kusingekuwa na punda
hata mmoja hapa nchini” Amesisitiza Mhe. Mnyeti.
Kwa upande wake Mtaalam wa
Mifugo na mmoja wa watetezi wa haki za Punda Dkt. Bedarn Masuruli ameipongeza
Serikali kwa hatua zake mbalimbali za kuhakikisha mnyama huyo hatoweki huku pia
akitoa rai kwa Serikali kuwazingatia wanyama hao katika Sera na Mipango
inayohusiana na Mifugo.
“Wadau wamepongeza hatua ya
Serikali kuungana na Taasisi zilizo chini ya Umoja wa Afrika kuandaa mkutano wa
kwanza wa Afrika kuhusu Punda uliozaa
azimio la Dar Es Salaam ambalo linasema “Punda Afrika Sasa na katika Siku
zijazo” Amesema Dkt. Masuruli.
Kwa upande wake Mkurugenzi
msaidizi wa Huduma za ukaguzi na ustawi wa wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na
Uvuvi Dkt. Anette Kitambi ameitaka jamii kushirikiana na Serikali kuwalinda
Punda kwani mfumo wa uzazi ni tofauti na
wanyama wengine ambapo anaweza kuzaa mara moja au asizae kabisa na muda wake wa
kubeba mimba huwa ni kati ya miezi 12 hadi 14.
“Na maajabu mengine ya
punda kama akiona mazingira sio rafiki anaweza kuahirisha kuzaa hivyo ni mnyama
mwenye sifa za tofauti kabisa ukiinganisha na wengine na ndio maana kutokana na
umuhimu huo kati ya wanyama wote ni yeye tu ndo aliandaliwa siku yake kitaifa”
Amebainisha Dkt. Kitambi.
Maadhimisho ya Siku ya
Punda duniani hufanyika Mei 08 ya kila mwaka na kwa Afrika Mashariki huwa ni
Mei 17 huku Serikali, wataalam na wadau mbalimbali wakitumia siku hiyo kujadili
hatma ya mnyama huyo na ustawi wake kwa ujumla.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (katikati) akikata keki kuashiria miaka 90 ya
Shirika la kutetea haki za wanyama linaloitwa "BROOKE" wakati wa
Maadhimisho ya Siku ya Punda Afrika Mashariki Mei 17, 2024 jijini Dodoma,
Wanaoshuhudia Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe na
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za ukaguzi na ustawi wa wanyama Dkt. Anette
Kitambi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za wanyama (ASPA)
Bw. Livingstone Masija wakati wa maadhimisho ya Afrika Mashariki ya siku ya Punda yaliyofanyika jijini Dodoma Mei
17, 2024.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na
wataalam na wadau mbalimbali wa kutetea haki za mnyama Punda wakati wa
Maadhimisho ya Siku ya mnyama huyo Afrika Mashariki yaliyofanyika Mei 17, 2024
jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni