Na. Martha Mbena
Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya Kimataifa tayari imeanza kufanya utaratibu wa kuwezesha upatikanaji wa chanjo za kutosha ili Mbwa na paka wengi wapate Chanjo dhidi ya kichaa Cha Mbwa.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Mifugo Ndug. Abdul Mhinte alipokuwa anafunga kilele Cha maadhimisho ya siku ya Kichaa Cha Mbwa Duniani yaliyofanyika Kitaifa Katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza Septemba 28.2024.
Mhinte amesema katika jitihada za kutokomeza ugonjwa huo Serikali inaratibu upatikanaji wa chanjo za kutosha kwa ajili ya kuchanja Mbwa na paka ambapo kwa kuchanja zaidi ya idadi ya 70% ya Mbwa na Paka kwa miaka mitano mfululizo tunaweza kutokomeza kabisa ugonjwa huo Nchini.
"Pamoja na hatari kubwa ya ugonjwa huu, ni kwamba unaweza kuzuilika kwa asilimia mia Moja na tunaweza kutokomeza iwapo tutaweza kuwachanja Mbwa na Paka wetu na kuwatunza vizuri", amesema Mhinte.
Aidha, Septemba 28 kila mwaka ni siku ya kichaa cha Mbwa duniani ambapo kutokana na takwimu za Wizara ya Afya Tanzania, watu 1,500 hufariki kwa ugonjwa wa kichaa cha Mbwa kila mwaka huku watu 60,000 hufariki kila mwaka kwa ugonjwa huo duniani.
Pia Mhinte amesema lengo la siku hiyo ni kuongeza ufahamu kwa wananchi juu ya ugonjwa huo na kujua namna ya kujikinga.
"Tunajua Mbwa na Paka ni wanyama muhimu katika maisha yetu lakini wanyama hawa kama hawatatunzwa vizuri pamoja na kuwakinga dhidi ya magonjwa wanageuka kuwa hatari kwa mwanadamu",amesema Mhinte.
Pia, amesema mwanadamu anaweza kupata ugonjwa huo kwa kung'atwa na Mbwa au Paka na kwa njia ya mate ya mnyama alieathirika na ugonjwa huo na kuweza kuambukizwa kwa mwanadamu.
Mh. Naibu katibu Mkuu amesema lengo la umoja wa mataifa ni kuhakikisha ugonjwa unatokomezwa duniani kote ifikapo 2030 kwa kutumia kauli mbiu ya "Breaking Rabies Boundaries" kama hamasa ya kutokomeza kabisa ugonjwa wa kichaa cha mbwa duniani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuchagua kufanya maadhimisho hayo Wilayani hapo.
Mhe. Samizi amesema ni jukumu la kila mmiliki wa Mbwa kumtunza Mbwa wake kwa kumpatia chakula, dawa na Chanjo zote na kumpenda Mbwa huyo ili kuhakikisha Mbwa wahazuruli mitaani.
Kauli mbiu ya kutokomeza kichaa cha mbwa inakuja na jitihada za kuondoa vikwazo vya kuwezesha mbinu za kutokomeza ugonjwa huo zikiwemo matumizi ya teknologia katika kutokomeza ugonjwa, kuongeza uelewa kwa wananchi kupitia kampeni mbalimbali na kuunganisha wadau.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni