Nav bar

Alhamisi, 19 Septemba 2024

TANGA YAJIPANGA KUONGEZA UZALISHAJI WA SAMAKI

Na Edward Kondela

Mkoa wa Tanga unajikita kuongeza kiwango cha uzalishaji wa samaki na mazao mengine ya baharini, ili kuzinufaisha jamii zake kupitia shughuli hizo zinazohusiana na Uchumi wa Buluu.

Mkuu wa Mkoa huo, Mhe Balozi Dkt. Batilda Burian, ameyasema hayo (18.09.2024) kwenye mkutano ulioandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa ajili ya kujadili masuala ya uhifadhi wa bahari kwa vizazi na maendeleo ya sekta hiyo Mkoani Tanga.

Amesema uvuvi ni moja ya sekta muhimu mkoani humo, hususan kwenye wilaya za Tanga, Pangani, Mkinga na Muheza ambapo takwimu zinaonesha kuwepo jumla ya wavuvi 13,336 na vyombo vya uvuvi vilivyosajiliwa 1,922. 

Mhe Balozi Dkt. Burian ametoa mfano kuwa, mwaka 2023/2024 samaki waliouzwa mkoani humo walikuwa na thamani ya Shilingi Bilioni 47.208, zilizowezesha ukusanyaji ushuru uliofikia takriban Shilingi Milioni 951.7 huku wakulima wa mwani wakifikia 5,300.

Ameongeza kuwa uzalishaji wa zao hilo la baharini umefikia tani 3,000 kwa thamani ya takribani Shilingi bilioni 5, kiasi kinachotarajiwa kuongezeka kufikia tani tani 5,000.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, amemtaja Mhe Balozi Dkt. Batilda Burian kuwa ni ‘Champion’ wa ulinzi wa rasilimali za bahari na mazao yake, kutokana na jitihada mbalimbali anazozifanya katika sekta hiyo Mkoani Tanga.

Amebainisha kuwa mkuu huyo wa mkoa amekuwa akifanya kampeni mbalimbali za kuhakikisha rasilimali za bahari hususan samaki wanazaliana kwa wingi kwa kupiga marufuku na kusimamia matukio ambayo yanaashiria uvunjifu wa sheria katika Sekta ya Uvuvi.

Aidha, amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kutoa elimu na kuhakikisha wadau wa sekta hiyo wanaendelea kufanya shughuli kwa misingi ya sheria, kanuni na taratibu za nchi lengo likiwa kuhakikisha ukuaji wa pato la taifa kupitia Sekta ya Uvuvi.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh ametoa wito kwa Sekretarieti za Mikoa kusimamia halmashauri kutekeleza sheria, kanuni na miongozo ya uvuvi, kupitia sera, sheria na kanuni za uvuvi, kuandaa miongozo ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi na mazingira yake, kupanga na kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya uvuvi.

Amesema endapo hayo yatasimamiwa vyema rasilimali za uvuvi zitakuwa na tija kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla na kuifanya Sekta ya Uvuvi kuwa endelevu na kubadili mtazamo juu ya jamii ya wavuvi na wote wanaojishughulisha na mazao ya uvuvi.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wametoa maoni yao juu ya kuendeleza rasilimali za uvuvi wakitaka elimu zaidi kutolewa kwa wadau wa uvuvi ya namna ya kutunza rasilimali za uvuvi na mazao ya uvuvi kwa ujumla na kuendelezwa kwa kampeni mbalimbali za kudhibiti uvuvi haramu.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede (kulia kwake) na baadhi ya viongozi kutoka katika wizara hiyo na ofisi ya mkuu wa mkoa huo, baada ya Mhe. Balozi Dkt. Burian kutembelewa ofisini kwake na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Mhede, kabla ya kushiriki mkutano wakujadili namna ya kukuza rasilimali za uvuvi na kudhibiti uvuvi haramu, kilichohusisha baadhi ya viongozi na wadau wa Sekta ya Uvuvi Mkoa wa Tanga. (18.09.2024)











Hakuna maoni:

Chapisha Maoni