Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Zachariyya Kera amewataka watumishi wa umma kujijengea tabia ya kusoma katiba na sheria za kiutumishi ili kuzifahamu sheria na haki zao za msingi.
Akiongea wakati alipotembelea
ofisi za Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) (20.10.2020) zilizopo Mkoani Pwani,
akiambatana na baadhi ya viongozi waandamizi wa wizara hiyo sekta ya mifugo,
Bw. Kera ametoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwataka wafanyakazi kujua haki zao za msingi na
kufuatilia kwa wakati.
"Watumishi waelimishwe
kuhusu haki zao na wapate stahiki zao kwa wakati na kujijengea tabia ya kusoma
sheria na taratibu za kiutumishi ili wasipitwe na mambo mengi." alisema
Bw. Kera.
Katika ziara hiyo ya baadhi
ya viongozi waandamizi wa Wizara ya Mifugo na uvuvi sekta ya mifugo, walipata
pia fursa ya kutembelea kituo cha uhimilishaji kanda ya mashariki (kibaha)
kilichopo Mkoani humo na Shamba la Malisho Vikuge kujifunza shughuli mbalimbali
zinazofanywa na kituo pamoja na shamba hilo.
Meneja wa Taasisi ya Chanjo
Tanzania (TVI), Dkt. Stella Bitanyi amesema chanjo ni muhimu sana kwa mifugo
kwani huboresha afya za mifugo na mfugo ukiwa na afya nzuri hata afya ya
binadamu huimarika pale atumiapo, chanjo zinaongeza pato la taifa kwani
huzalishwa na kuuzwa.
Aidha, Dkt. Bitanyi ametumia
nafasi hiyo kuwaeleza watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi changamoto
zinazowakabili ikiwa ni pamoja na upungufu wa vifaa vya kisasa vya kufanyia
kazi kwani wanatumia teknolojia ya chini sana katika utendaji wao wa kazi.
Hata hivyo ameshauri kuwe na
utaratibu wa kutoa elimu kwa wataalam ya namna ya kutumia Chanjo kwani wengi
hukosea na kuchanja maeneo yasiyostahili.
"Elimu ya uchanjaji
inahitajika kwa wingi kwa wataalam wetu kwani wanachanja shingoni badala ya
kuchanja nyuma ya kwapa kwenye ngozi." Alisisitiza Dkt. Stella.
Mkuu wa kituo cha uhimilishaji kanda ya
Mashariki (Kibaha), Bw. Anzigary Kasanga Balaka ameeleza kazi wanazofanya ikiwa
ni pamoja na kuzalisha mbegu bora za madume na kuuza, kutoa ushauri kwa
wafugaji na kuboresha mifugo yao kwa uhimilishaji, kuratibu Mafunzo ya
uhimilishaji na kuuza vitendea kazi vya uhimilishaji kama mitungi ya gesi.
Aidha, Viongozi wa TVI, Kituo
cha Uhimilishaji na Shamba la Malisho Vikuge waliishukuru serikali ya awamu ya
tano kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuendelea kuona umuhimu wa shughuli
wanazofanya na kuwatembelea kujionea mazingira ya watumishi wao na changamoto
wanazopitia katika maeneo yao ya kazi na kuzitafutia ufumbizi.
Mkurugenzi wa Utawala na
Rasilimali Watu (WMUV), Bw. Zachariyya Kera (kulia) akitoa ufafanuzi wa hatua
na namna mtumishi anavyopandishwa cheo kwa watumishi wa Taasisi ya Chanjo
Tanzania (TVI) walipotembelea kituo hicho wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani.
(20/10/2020)
Mkurugenzi wa Manunuzi na
Ugavi (WMUV), Bw. Emanuel Mayage akipata ufafanuzi wa namna ya kutengeneza
chanjo mbalimbali kutoka kwa Meneja wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), Dkt.
Stella Bitanyi walipotembelea Taasisi hiyo mkoani Pwani. (20.10.2020)
Meneja wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), Dkt. Stella Bitanyi akitoa taarifa ya Taasisi hiyo kwa watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) juu ya namna wanavyofanya kazi na mafanikio waliyopata hadi sasa walipotembelea Taasisi hiyo mkoani Pwani. (20.10.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni