Nav bar

Jumapili, 11 Oktoba 2020

SEKTA YA UVUVI INATOA ASILIMIA 30 YA PROTINI KWENYE LISHE - DKT. TAMATAMAH

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amewataka wafugaji na wavuvi nchini kuacha kufanya kazi zao kwa mazoea na badala yake watumie njia za kisasa na kitaalam katika utekelezaji wa shughuli hizo.

 

Dkt. Tamatamah aliyasema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa za Sekta za Mifugo na Uvuvi wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula duniani uliofanyika leo (10.10.2020) mkoani Njombe.

 

Katika taarifa yake Dkt. Tamatamah alisema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatambua umuhimu wa lishe bora kwa wananchi hususan wazee na watoto hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa nyama na samaki ni vyakula vinavyotoa protini kwa wingi zaidi ukilinganisha na vyakula vingine.

 

"Mhe. Mgeni rasmi sekta ya uvuvi inachangia asilimia 30 ya protini inayotokana na wanyama huku ikichangia ajira kwa Watanzania takribani Milioni 4.5 katika shughuli mbalimbali za sekta hiyo" Alisema Dkt.Tamatamah.

 

Aidha aliongeza kuwa uzalishaji wa samaki kwa upande wa maji ya asili umefikia kiasi cha takribani tani 497,567 huku kwa upande wa uzalishaji viumbe maji ukifikia kiasi cha takribani tani 18,716.36.

 

Kwa upande wa Mifugo Dkt. Tamatamah alisema kuwa sekta hiyo imechangia ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia lishe bora, ajira, kipato cha mtu mmoja mmoja na fedha za kigeni ambapo kwa mwaka 2019/20 ilichangia pato la taifa kwa asilimia 7.4 na kukua kwa asilimia 5 ikilinganishwa na asilimia 4.9 kwa mwaka 2018/19.

 

"Nihitimishe taarifa yangu kwa kutoa rai kwa wananchi kuongeza ulaji wa bidhaa zitokanazo na mifugo na uvuvi ili kufikia kiwango kilichosimikwa na shirika la chakula la duniani (FAO)" Alimalizia Dkt. Tamatamah.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akiwasilisha taarifa ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani uliofanyika Mkoani Njombe. (10.10.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt.Rashid Tamatamah (kulia) akifafanua jambo kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mgeni rasmi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba (kushoto) alipotembelea banda la wizara hiyo kwenye  uzinduzi  wa Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula duniani. (10.10.2020)

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Dkt. Elifatio Towo (kulia) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba (kushoto) alipotembelea banda la taasisi hiyo kwenye Uzinduzi wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani. Katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt.Rashid Tamatamah. (10.10.2020). 

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Mhe. Andrea Tsere (wa pili kutoka kulia) akielezea jambo mbele ya Mgeni rasmi – Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba (kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt.Rashid Tamatamah (wa tatu kutoka kulia) walipofika kwenye banda la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwenye Uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani. (10.10.2020).


 




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni