Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa mafunzo rejea kwa maafisa ugani kutoka mikoa ya Singida na Dodoma ili kuwawezesha wagani hao kwenda kutoa elimu kwa wafugaji.
Akifungua mafunzo hayo kwa
niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Mkurugenzi wa Idara ya
Utafiti, Mafunzo na Ugani, Dkt. Angello Mwilawa amesema wizara imekua
ikitekeleza mikakati muhimu katika sekta ya mifugo ili kuweza kumsaidia mfugaji
kufuga kisasa na kibiashara.
Mikakati hiyo ni pamoja na
Uboreshaji wa Koosafu za mifugo nchini, Udhibiti wa magonjwa, Upatikanaji wa
uhakika wa malisho na maji katika maeneo yaliyo na mifugo, Kuboresha uzalishaji
ulio wa kibiashara na ustawishaji wa ndege wafugwao, Kutafuta ufumbuzi wa
kudumu wa migogoro ya ardhi, Kuhamasisha na kuanzisha vyama vya ushirika vya
wafugaji na Kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na mifugo pamoja na mazao
yake.
Dkt. Mwilawa amesema katika
kutekeleza mikakati hiyo wizara imekua ikipata changamoto nyingi ambazo ni
ukosefu wa maarifa kwa wafugaji na ndio maana wizara imeamua kutoa mafunzo rejea
kwa maafisa ugani ili waweze kwenda kuwaelimisha wafugaji walioko katika mikoa
yao.
Katika kutekeleza mikakati
hiyo maafisa ugani wametakiwa kwenda kushirikiana na sekta na wadau wengine
waliopo katika maeneo yao ili kuhakikisha wafugaji wanapata elimu hii na kuweza
kufuga kwa tija.
Naye mmoja wa washiriki wa
mafunzo hayo na Mshauri wa mifugo kutoka
sekretarieti ya mkoa wa Singida, Dkt. David Mluma ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi na
Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kutoa mafunzo
rejea kwa kuwapatia ujuzi katika sekta ya mifugo.
Dkt. Mluma amesema mafunzo
haya yamekuja muda mzuri kwani serikali kwa sasa inaendelea kuhamasisha
wafugaji kuboresha koosafu za mifugo ili wafugaji waweze kuzalisha kwa tija.
Lakini pia wamekumbushwa suala la udhibiti wa magonjwa ambalo usimamizi wake
unasaidia mazao ya mifugo kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Afisa Mifugo kutoka
Halmashauri ya Kondoa Mji, Semeni Mwakasege amesema mafunzo haya yamemsaidia
kutambua sheria mbalimbali ambazo hapo awali hakudhani kama zinawahusu, hivyo
ameahidi kwenda kuwaelimisha wataalamu wenzake pamoja na viongozi wa
halmashauri ili wote kwa pamoja waweze kuzisimamia.
Pia ametoa wito kwa washiriki
wenzake kuhakikisha kila mmoja anakwenda kutoa elimu waliyoipata kwa wataalam
wenzao na wafugaji. Vilevile ameiomba wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya
Rais – TAMISEMI kuongeza wigo wa mafunzo haya ili wataalam wengi wa mifugo
waweze kupata mafunzo haya ambayo yatasaidia kusambaza elimu hii kwa wafugaji
wengi zaidi.
Mafunzo haya yametolewa kwa
maafisa ugani 20 kutoka mikoa ya Singida na Dodoma na yamefanyika katika ukumbi
wa chuo cha Mipango jijini Dodoma. Katika mafunzo hayo washiriki wameweza
kupitishwa katika mada za Sheria Kanuni na Miongozo ya sekta ya mifugo,
Udhibiti wa Magonjwa na matumizi ya dawa na viwatilifu, Sumukuvu, Madhara na
namna ya kudhibiti, Mashamba darasa ya malisho na ustawishaji wa matunzo ya
nyanda za malisho pamoja na uboreshaji wa koosafu za mifugo kwa ufugaji
endelevu na tija.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni