Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amekabidhi vipande vya kamba za manila 700,000 kwa wakulima wa mwani katika Kijiji cha Songosongo, wilayani Kilwa, mkoa wa Lindi.
Akizungumza na wananchi wa
Songosongo jana (19/10/2020) Dkt. Tamatamah amesema serikali kupitia Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) imetoa kamba hizo ili kuwawezesha wakulima wa
mwani kwani kamba ilikuwa ni moja ya changamoto waliyokuwa wakikabiliana nayo.
Kamba hizi za manila (ambazo
kila moja ina urefu wa mita 10) katika kilimo cha mwani, hufungwa katika
vigingi na hutumika kwa ajili ya kuoteshea mwani ambapo mwani hufungwa katika
kamba hizo zinazosaidia pia mwani kutochukuliwa na maji ya bahari pale panapokuwepo
na wimbi.
Dkt. Tamatamah amesema
duniani kote kwa sasa mwani unalimwa kibiashara, hivyo mwani ni moja ya zao linalopewa
kipaumbele katika wizara. Katika kilimo cha mwani wakulima wanakutana na changamoto
mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa mitaji na masoko.
“Wizara kupitia sekta ya
uvuvi imeanza kutoa kamba ambazo ni moja ya pembejeo muhimu kwa wakulima wa
mwani ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha wakulima hao kwa kuwapunguzia sehemu ya
gharama za uzalishaji ili baadae waweze kusimama wenyewe,” alisema Dkt. Tamatamah.
Pia amesema kuwa kama
wakulima watalima vizuri katika kamba moja ya mita kumi katika bamvua nne (miezi
miwili) wanaweza kupata kati ya kilo 8-10, na kamba hizo walizopewa zinaweza kutumika
kwa mwaka mzima. Lengo la wizara ni kusambaza kamba hizi kwa wakulima wa mwani
maeneo yote Tanzania Bara.
Dkt. Tamatamah amesema kuwa
ipo changamoto ya soko la mwani hasa kwenye bei kwani kwa sasa asilimia 90 ya
mwani inauzwa nje ikiwa ghafi na ni asilimia 10 tu ndio inayotumika hapa
nchini.
Hivyo wizara kwa sasa inawahamasisha
wakulima kujiunga katika vikundi na kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili
waweze kukopesheka na waweze kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata mwani ili
kuuongezea thamani. Hii itasaidia kupunguza kiasi cha asilimia ya mwani
inayokwenda nje ya nji ikiwa ghafi na kusaidia kuongeza ajira.
Aidha, Katibu Mkuu Tamatamah
amesema zao la mwani linazo faida kubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza kipato
katika jamii za maeneo ya pwani hasa kwa akina mama, inaodoa umaskini lakini
pia linaingiza fedha za kigeni.
Naye mkulima wa mwani, Bi.
Mbimbisa Omary amemshukuru Katibu Mkuu Tamatamah kwa kuwaletea vitendea kazi
kwa ajili ya kilimo cha mwani. Bi. Mbimbisa amesema kilimo cha mwani kinawasaidia
mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuwasomesha Watoto, kununua chakula pamoja na
ujenzi wa nyumba.
Bi. Jaka Farahani ambaye ni
mkulima wa mwani amesema changamoto ya masoko inawasumbua sana hasa pale wanunuzi
wanaowategemea wasiponunua hivyo ameiomba wizara kuwasaidia kutatua changamoto
hiyo. Lakini pia amemuomba Katibu Mkuu kuendelea kuwapelekea kamba nyingi zaidi
kwa kuwa eneo la kulima ni kubwa na wakulima wapo wengi.
Mkurugenzi wa Idara ya
Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla amesema wizara kupitia idara yake
inaendelea kuhamasisha kampuni kuendelea kuchukua leseni kwa ajili ya kununua
mwani na mpaka sasa zipo kampuni 7. Lengo la kuwa na kampuni nyingi ni kuongeza
ushindani hivyo kampuni zinahamasishwa kujisajili ili zitambulike na ziweze
kufanya biashara ya mwani.
Zao la mwani hapa nchini
Tanzania lilianza kulimwa miaka ya 1980 na lilianzishwa katika kisiwa cha
Zanzibar. Baada ya kufanikiwa katika kipindi cha majaribio, miaka ya 1990 mpaka
2000 Tanzania hususani Zanzibar ilikuwa ni nchi ya kwanza duniani kwa
uzalishaji wa mwani. Lakini kutokana na changamoto mbalimbali kwa sasa Tanzania
ni nchi ya tatu kwa uzalishaji wa mwani ambapo nchi ya kwanza ni Ufilipino
ikifuatiwa na Indonesia.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akiongozana na baadhi ya wakulima wa
mwani baada ya kumaliza kutembelea moja ya shamba katika kijiji cha Songosongo,
wilayani Kilwa. (19.10.2020)
Bi. Mbimbisa Omary ambaye ni
mkulima wa mwani akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wakulima wa mwani wa
kijiji cha Songosongo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt.
Rashid Tamatamah (aliyevaa tisheti nyeusi) kutokana na wakulima hao kupatiwa
kamba 700,000 na Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Sekta ya Uvuvi. (19.10.2020)
Bi. Mbimbisa Omary ambaye ni mkulima wa mwani akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wakulima wa mwani wa kijiji cha Songosongo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (aliyevaa tisheti nyeusi) kutokana na wakulima hao kupatiwa kamba 700,000 na Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Sekta ya Uvuvi. (19.10.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na wakulima wa mwani pamoja
na wananchi wa kijiji cha Songosongo wilayani Kilwa (hawapo pichani) wakati
alipokwenda kukabidhi kamba kwa wakulima hao. (19.10.2020)
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha
Songosongo waliofika kwenye mkutano kumsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah wakati alipotembelea Kijiji hicho kwa
ajili ya kugawa kamba kwa wakulima wa mwani. (19.10.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akimkabidhi kamba kwa ajili ya
wakulima wa mwani Mwenyekiti wa kijiji cha Songosongo, Bw. Swaluya Sadi (kushoto).
Dkt. Tamatamah amekabidhi jumla ya kamba 700,000 zoezi lililofanyika katika
kijiji cha Songosongo, wilayani Kilwa. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya
Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla. (19/10/2020)
Mkurugenzi wa Idara ya
Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla, akizungumza na baadhi ya akina
mama wakulima wa mwani, baada ya zoezi la Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Sekta ya Uvuvi) kukabidhi kamba 700,000 kwa wakulima hao katika kijiji cha
Songosongo, wilayani Kilwa. (19.10.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni