Nav bar

Jumapili, 11 Oktoba 2020

PROF. GABRIEL: OGESHENI MIFUGO YENU ILI KUIKINGA NA MAGONJWA

Wafugaji hapa nchini wametakiwa kuogesha mifugo yao ili kuikinga na magonjwa yaenezwayo na kupe.

 

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel jana tarehe 10.10.2020 wakati akizindua awamu ya tatu ya kampeni ya uogeshaji mifugo iliyofanyika katika Kijiji cha Bahi Sokoni, wilayani Bahi, mkoani Dodoma.

 

Prof. Gabriel amesema lengo kuu la kampeni hizi ni kuhamasisha wafugaji wote nchini kuunga mkono juhudi za serikali katika kuongeza tija ya ufugaji kwa kuwa na mifugo yenye afya njema, mifugo isiyo na magonjwa ambayo itazalisha mazao zaidi na yenye ubora wa kiwango cha kitaifa na kimatifa.

 

“Lengo la uogeshaji ni kudhibiti magonjwa yaenezwayo na kupe hususani Ndigana kali (East Coast Fever – ECF), Ndigana Baridi (Anaplasmosis), Mkojo Mwekundu (Babesiosis) na Maji Moyo (Heart Water) ambayo yamekuwa yakiathiri mifugo na kusababisha hasara kubwa kwa mfugaji,” alisema Peof. Gabriel.

 

Magonjwa yaenezwayo na kupe yasipodhibitiwa ipasavyo huchangia asilimia 72 ya vifo vyote vya ng’ombe hapa nchini. Kati ya magonjwa hayo, ugonjwa wa Ndigana Kali huchangia vifo kwa kiwango kikubwa cha asilimia 44. Hasara inayotokana na magonjwa yaenezwayo na kupe inakadiriwa kuwa ni dola za kimarekani milioni 64.7 kwa mwaka sawa na takribani shilingi bilioni 145. Hasara nyingine ni pamoja na kupunguza uzalishaji wa maziwa, kupungua kwa nyama kutokana na kukonda, kushuka thamani ya Ngozi, kupoteza wanayama kazi na udumavu wa ndama.

 

Prof. Gabriel amesema serikali imenunua dawa za kuogesha mifugo aina ya Paranex, Paratop na Amitrax kiasi cha lita 15,579 zenye thamani ya shilingi 592,822,375 ambazo zinatosheleza majosho 1,983 katika halmashauri 162 na matarajio ni kifikia jumla ya michovyo 405,000,000 ya mifugo yote itakayoogeshwa.

 

Kupitia kampeni hizi, serikali imekuwa ikitoa dawa zenye ruzuku na bei elekezo za kuogeshea mifugo ambapo kwa ng’ombe ni shilingi 50, mbuzi na kondoo shilingi 10 kwa mchovyo mmoja, wafugaji wamehamasika sana kuogesha mifugo yao.

 

Pia serikali kuu, halmashauri na wadau wengine wamejenga majosho 101, kukarabati majosho 578 pamoja na kuunda kamati 1,036 zinazosimamia shughuli za uogeshaji wa mifugo katika ngazi ya josho. Vilevile imeunda timu 12 ambazo huzunguka nchi nzima kwa ajili ya kuhamasisha shughuli za uogeshaji mifugo na ufuatiliaji wa miundombinu ya mifugo.

 

Katika kudhibiti magonjwa yaenezwayo na kupe, serikali imetunga Kanuni ya Uogeshaji na Matumizi ya Viuatilifu vya Mifugo (Acaricide Applications and Management Regulations, 2019). Kanuni hii inamlazimisha mfugaji kuogesha mifugo yake mara mbili kwa mwezi na serikali itasimamia zoezi la uogeshaji kwa ujumla.

 

Katika uzinduzi huo, Prof. Gabriel alitoa maelekezo kwa wafugaji wote nchini kuhakikisha wanaogesha mifugo yao ili kuikinga na magonjwa, halmashauri zote nchini kusimamia kanuni ya uogeshaji ili wafugaji waifuate maana majosho yapo na dawa zimeshatolewa, halmashauri zote nchini kwa kushirikiana na wafugaji na wadau ziendelee kukarabati majosho yake na miundombinu mingine ya mifugo na halmashauri kuhamasisha wafugaji kuunda vi vitakavyosimamia uendeshaji endelevu wa majosho ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti benki kwa ajili ya kuhifadhi fedha zinazokusanywa wakati wa uogeshaji mifugo.

 

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma R. Mganga amesema mifugo katika wilaya ya Bahi imekuwa ikichangia zaidi ya asilimia 55 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa mwaka. Lakini mifugo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya magonjwa kama Ndigana Kali, Ndigana Baridi, Ugonjwa wa Mapafu ya ng’ombe na mbuzi na kideri cha kuku. Halmashauri imekuwa ikidhibiti magonjwa haya kwa kuogesha na kunyunyizia mifugo viuatilifu, kutoa chanjo na kutoa ushauri wa kitaalam kupitia maafisa ugani waliopo katika kata na vijiji.

 

Nao wafugaji walioleta mifugo yao kwa ajili ya kuiogesha katika uzinduzi wa kampeni hiyo ya awamu ya tatu wilayani Bahi wameishukuru serikali kwa kufufua majosho na kujenga mengine mapya pamoja na kutoa ruzuku ya madawa ya kuogeshea mifugo kwani kwa kufanya hivyo wanaimani mifugo yao hatakufa tena kutokana na magonjwa yanayosababishwa na kupe.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga amesema kuwa awamu ya kwanza ya kampeni hii ilizinduliwa tarehe 16/12/2018 wilayani Chato na awamu ya pili uzinduzi wake ulifanyika tarehe 29/10/2019 katika halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi.

 

Prof. Nonga amesema katika kampeni awamu ya kwanza na awamu ya pili serikali ilinunua jumla ya lita 21,373.06 za dawa zenye thamani ya 740,714,750 kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuogesha mifugo yao. Katika awamu zote mbili kumekuwa na jumla ya michovyo 254,375,555 ya mifugo yote ikiwemo ng’ombe 176,320,815, mbuzi 58,012,461, kondoo 20,039,594 na punda 2,685.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (mwenye koti jeupe katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kampeni ya Uogeshaji Mifugo Kitaifa awamu ya tatu katika kijiji cha Bahi Sokoni, wilayani Bahi, mkoani Dodoma. (10.10.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwahutubia wananchi wa wilaya ya Bahi (hawapo pichani) kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Uogeshaji Mifugo Kitaifa uliofanyika katika kijiji cha Bahi Sokoni, wilayani Bahi, mkoani Dodoma. (10.10.2020)

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo (WMUV), Prof. Hezron Nonga akitoa taarifa fupi ya Kampeni ya Kitaifa ya Uogeshaji Mifugo hapa nchini kwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya Kampeni hiyo uliofanyika katika kijiji cha Bahi Sokoni, wilayani Bahi, mkoani Dodoma. (10.10.2020)

Katibu Mkuu Wizara Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyemshika ng'ombe) akishirikiana na wafugaji katika zoezi la uzinduzi wa kuogesha Mifugo Kitaifa awamu ya tatu lililofanyika katika kijiji cha Bahi Sokoni, wilayani Bahi, mkoani Dodoma. (10.10.2020)

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatima Mganga (mwenye kilembe) akipokea madawa ya ruzuku ya kuogeshea Mifugo kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel kwa niaba ya wakurugenzi wa Halmashauri zote hapa nchini wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Uogeshaji Mifugo Kitaifa awamu ya tatu uliofanyika katika kijiji cha Bahi Sokoni, wilayani Bahi, mkoani Dodoma. (10.10.2020)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni