Nav bar

Ijumaa, 26 Agosti 2022

SPIKA MSTAAFU MSEKWA APONGEZA UCHUMI WA BULUU WA SERIKALI YA RAIS SAMIA

Na Mbaraka Kambona, Mwanza


Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Pius Msekwa ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuwezesha vijana kufuga samaki ili wanufaike kupitia uchumi wa buluu.


Mzee Msekwa alibainisha hayo alipotembelewa  nyumbani kwake Wilayani Ukerewe na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega wakati wa  ziara yake aliyoifanya Wilayani humo, Mkoani Mwanza Agosti 19, 2022.


Alisema kuwa mambo ambayo yanafanywa na Serikali ya awamu ya sita hususan ya kuwezesha vijana kujiajiri ni mambo ambayo Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere alitamani sana kuyafanya na hivyo kama angekuwa hai mpaka leo angefurahi sana.


"Haya yote uliyoyasema Mwl. Nyerere alitamani kuyafanya wakati wa uhai wake, kama angekuwepo leo angefurahi sana kwa sababu yale yote aliyoyataka kuyafanya Rais Samia anayaendeleza kwa kasi kubwa, hongereni sana",  alisema


Awali, akitoa taarifa ya fupi kuhusu ziara yake Mkoani Mwanza, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alimueleza Spika Mstaafu Mzee Msekwa kuwa  Mhe. Rais Samia ametoka shilingi bilioni 20 kuwawezesha  watanzania hususan vijana kufuga samaki katika vizimba katika Ziwa Viktoria hivyo lengo la ziara yake hiyo ni kuhamasisha vijana na makundi mengine kuchangamkia fursa hiyo adhimu.


Katika hatua nyingine, Waziri Ulega alisema mwaka huu pia Serikali itawakopesha wavuvi nchini kote boti za kisasa zaidi ya 150 ili wavuvi waweze kuboresha shughuli zao na kuongeza uzalishaji wa samaki.


Aliongeza kwa kusema kuwa boti hizo zitafungamanishwa na teknolojia za kisasa zitakazomsaidia mvuvi kurahisisha shughuli za uvuvi.


Waziri Ulega aliendelea kufafanua kuwa Mhe. Rais Samia anataka kuwatoa wavuvi katika uvuvi wa kuwinda na kufanya ufugaji wa kisasa wa uhakika.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni