Nav bar

Jumapili, 28 Agosti 2022

LITA KIKULULA YATAKIWA KUENDELEA KUSAIDIA WANANCHI

Na Mbaraka Kambona, 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki ameipongeza Wakala ya Mafunzo ya Mifugo, Kampasi ya Kikulula (LITA-Kikulula) iliyopo Wilayani Karagwe Mkoani Kagera kwa kazi nzuri ya kuwawezesha wananchi ujuzi wa kufuga kisasa huku akiwataka kuendelea kuwasaidia wananchi kufanya ufugaji wa kisasa, wenye tija zaidi kwao na Taifa kwa ujumla.


Waziri Ndaki alitoa kauli hiyo Agosti 26, 2022 wakati wa ziara yake aliyoifanya katika kampasi hiyo kwa lengo la kukagua shughuli wanazozifanya.


"Napenda kuipongeza Kampasi hii ya LITA Kikulula kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kazi zao, ukijaribu kuangalia rasilimali walizonazo na kile wanachokitoa utaona kwamba ni juhudi kubwa wanafanya ili kuwa na matokeo haya wanayoyapata," alisema


Alisema kuwa kampasi hiyo imeendelea kupata matokea hayo kwa sababu wanafundisha kwa vitendo zaidi kuliko maneno na ndio maana alipokutana na wanafunzi wa katika kampasi hiyo walimueleza Waziri huyo kuwa kutokana na Mafunzo wanayoyapata wapo tayari kujiajiri.


"Ni vizuri muendelee kuwa na muelekeo wa namna hiyo kwa sababu vyuo hivi vilianzishwa kwa lengo la kuzalisha wananchi watakaokuwa wafugaji wa kisasa, wanaofanya ufugaji wa tija, wafugaji ambao watakuwa wanajua kwamba kuwa na Ng'ombe ni utajiri", alisisitiza


Naye Kaimu Mkuu wa Kampasi hiyo ya Kikulula, Bw. Said Mohamed alimueleza Waziri huyo kuwa katika Kampasi hiyo wana programu ya kuwatembelea wafugaji kwa ajili ya kuwasaidia kutatua changamoto za mifugo zinazowakabili na kuwashauri namna bora ya ufugaji ila wanakabiliwa na changamoto ya usafiri kwa ajili ya wanafunzi hao.


Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kihanga, Bw. Rwamhangi Mugasha aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kupeleka Kampasi hiyo Kikulula kwa sababu kupitia Kampasi hiyo  wafugaji wengi wamebadilika, wanafuga kisasa na matunda ya ufugaji wameanza kuyaona.


"Mhe. Waziri naomba nikuambie kuwa wanafunzi hawa wamekuwa msaada mkubwa sana kwa wafugaji wetu hapa Kikulula, hata ile changamoto ya upungufu wa Wataalamu wa Mifugo kwenye Kata yetu kwa kweli haipo, hawa vijana wanasaidia sana, na  wanatembea kwa miguu kuwafikia wafugaji wetu, kwa kweli tunashukuru",  alisema Diwani huyo


Aidha, alisema kuwa katika Kata hiyo kwa sasa kumekuwa na wafugaji wengi wa kisasa na hivyo alimuomba Waziri Ndaki  kuona uwezekano wa kuwa na shamba darasa ili wafugaji waweze kujifunza zaidi ufugaji wa kisasa na waweze kubadilisha maisha yao.

Kaimu Mkuu wa Kampasi ya Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA -Kikulula), Bw. Said Mohamed  akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) mifugo iliyopo katika kampasi hiyo alipotembelea Agosti 26, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni