Nav bar

Ijumaa, 26 Agosti 2022

WAZIRI NDAKI ATAKA AGIZO LA RAIS SAMIA JUU YA MAENEO YA WAFUGAJI KUTEKELEZWA

Na. Edward Kondela

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amezitaka halmashauri na mamlaka za serikali za mikoa kuhakikisha zinatekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji ili kukuza sekta hiyo na kuepusha migogoro ya matumizi bora ya ardhi.


Waziri Ndaki amebainisha hayo (19.08.2022) alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro na kuzungumza na wakulima na wafugaji katika vijiji vya Tanga na Njiwa, ambapo amesema serikali ina nia nzuri ya kuendeleza Sekta ya Mifugo na kuzitaka halmashauri hizo na mamlaka za serikali za mikoa kutekeleza agizo hilo huku akiwataka wafugaji kutolisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.


Ameongeza kuwa serikali pia imeelekeza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kuanzia ngazi ya kijiji ambayo hayajasajiliwa, yanatakiwa kutambuliwa rasmi na kusajiliwa pamoja na kulindwa na kuhakikisha yanatumika kama ilivyopangwa kwa ajili ya kulishia mifugo pekee pamoja na kuwataka wafugaji kutoingiza mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi na mapori tengefu.


 “Halmashauri na mamlaka za serikali za mikoa zinapaswa kuyalinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji, kama yapo maeneo yaliyotengwa na kijiji au kata kwa ajili ya malisho hayo maeneo yasajiliwe rasmi kuzuia migogoro.” Amesema Mhe Ndaki.


Aidha amewaarifu wafugaji kuwa kufuatia taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wizara inatoa tahadhari kwa wafugaji za taarifa zinazoonesha kumekuwepo na vipindi virefu vya ukavu vilivyojitokeza katika kipindi cha Mwezi Machi na Aprili mwaka 2022 hali ambayo inatishia upungufu wa malisho ya mifugo pamoja na maji.  


Amesema kufuatia hali hiyo wafugaji wategemee ukame hivyo wawe na tahadhari ya kuvuna mifugo na kubakiza ile inayoweza kutunzwa vizuri kutokana na kiasi cha malisho alichonacho mfugaji pamoja na maji.


“Tuchukue tahadhari ya kuvuna mifugo yetu tusije kukutana na ukame halafu tukaanza kulalamika mifugo imeanza kuwa dhaifu au kufa huku tulikuwa tukijua ni vizuri ukapunguza kwa kuvuna mifugo yako na kubaki na ile itakayotosheleza malisho uliyonayo pamoja na maji.” Amesema Mhe. Ndaki


Katika ziara hiyo ya kikazi ya siku moja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Mathayo Maselle amezungumzia skimu ya umwagiliaji iliyopo Kijiji cha Njiwa na Itete ambayo imetengwa maalum kwa ajili ya kilimo imekuwa na changamoto ya wafugaji kuingiza mifugo yao katika eneo hilo jambo ambalo limekuwa likisababisha migogoro.


Hata hivyo kufuatia changamoto hiyo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameutaka uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na wakulima na wafugaji kutengeneza mfereji utakaosafirisha maji kutoka kwenye skimu hiyo hadi eneo lingine watakalolitenga kwa ajili ya kunyweshea mifugo maji badala ya mifugo hiyo kupita kwenye mashamba ya wakulima kwenda kunywa maji.


Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria ziara ya Mhe. Waziri Ndaki wametoa maoni kadhaa yakiwemo ya utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji kutokana na matumizi bora ya ardhi pamoja na kuomba uwepo wa mpaka maalum wa skimu ya umwagiliaji ya vijiji vya Itete na Njiwa ili wakulima waweze kufanya shughuli zao hali kadhalika wafugaji wapate huduma ya maji ya mifugo yao bila kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro na kuzungumza na wakulima na wafugaji ambapo amesema baadhi ya kero serikali inaendelea kuzifanyia kazi ili kuhakikisha inaondoa migogoro kati yao na kuwahamasisha wafugaji kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika Jumanne ijayo Tarehe 23 Mwezi Agosti.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza na wakuu wa idara na vitengo wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro, kabla ya kuwatembelea baadhi ya wakulima na wafugaji wa wilaya hiyo, ambapo katika kikao hicho amepokea taarifa ya maendeleo ya sekta za mifugo na uvuvi na kutaka zoezi la uwekaji hereni za kieletroniki kwa mifugo lifanyike kwa amri kama sheria inavyotamka na siyo hiari. (19.08.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), (kushoto) akipokewa na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro Mhe. Mathayo Maselle (kushoto kwake), mara baada ya Waziri Ndaki kufika katika ofisi za wilaya hiyo kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja kwa kukutana na wakulima na wafugaji. (19.08.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), akizungumza na baadhi ya wakulima na wafugaji waliohudhuria mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Tanga kilichopo Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro ambapo Waziri Ndaki amezitaka halmashauri na mamlaka za serikali za mikoa kutekeleza agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kutenga maeneo kwa ajili ya malisho ya mifugo pamoja na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ambayo hayajatambuliwa, yatambuliwe rasmi na kusajiliwa ili kuepusha migogoro ya matumizi bora ya ardhi. (19.08.2022)

Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro Mhe. Mathayo Maselle, akizungumza kwenye kikao cha hadhara katika Kijiji cha Njiwa, ambapo mgeni rasmi ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), katika mkutano huo Mhe. Maselle ameelezea uwepo wa mgogoro wa matumizi ya skimu ya umwagiliaji iliyopo katika vijiji vya Njiwa na Itete ambapo Waziri Ndaki ameutaka uongozi wa wilaya hiyo kushirikiana na wakulima na wafugaji kutengeneza mfereji wa kusafirisha maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo kwenye eneo watakalotenga ili kuepusha migogoro. (19.08.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), akizungumza na baadhi ya wakulima na wafugaji waliohudhuria mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Njiwa kilichopo Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro, ambapo amewaarifu wafugaji kuwa kufuatia taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wizara inatoa tahadhari kwa wafugaji za taarifa zinazoonesha kumekuwepo na vipindi virefu vya ukavu vilivyojitokeza katika kipindi cha Mwezi Machi na Aprili mwaka 2022 hali ambayo inatishia upungufu wa malisho ya mifugo pamoja na maji hivyo wafugaji wategemee ukame na kuwaasa kuvuna mifugo na kubakiza ile inayoweza kutunzwa vizuri kutokana kiasi cha malisho alichonacho mfugaji pamoja na maji.(19.08.2022)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni