Na Mbaraka Kambona,
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi una fursa nyingi za kiuchumi hivyo ni muhimu vijana kufundishwa namna ya kutumia fursa hizo kujiajiri ili kujiongezea kipato.
Naibu Waziri Ulega alitoa kauli hiyo wakati akiongea na Uongozi wa Shirikisho la Kimataifa linaloshughulika na programu ya uendelezaji wa pwani na uvuvi wa bahari (IUCN) walipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam Septemba 28, 2022.
Alisema kuwa katika ukanda wa pwani wa bahari kuanzia Moa mpaka Msimbati kuna fursa nyingi za ukuzaji viumbe maji ikiwemo ukulima wa mwani, ufugaji majongoo bahari na kaa na tayari kuna jitihada mbalimbali zimeshaanza kuchukuliwa na serikali kuhakikisha fursa hizo za uchumi wa buluu zinawasaidia wananchi hususan vijana na kinamama.
“Sasa hivi tuna shilingi bilioni tatu (3) za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajli ya ukulima wa mwani, zitatumika kununulia vifaa vya kulimia mwani ikiwemo Kamba, Taitai na Mbegu,”alisema
Aliongeza kwa kuwataka wadau hao kushirikiana na serikali kikamilifu kuwapatia ujuzi stahiki vijana ili waweze kutumia fursa hizo zilizopo katika ukanda wa pwani kujiongezea fursa za ajira na kipato.
“Leo IUCN mmekuja na hili jambo la kumuunga mkono Mhe. Rais Samia la kutengeneza fursa za ajira kupitia uchumi wa buluu, tafadhali, tuwafundishe hawa watu wetu wafuge,”alihimiza
Aidha, Mhe. Ulega aliwataka viongozi hao wa IUCN kuandaa mpango utakaoonesha namna watakavyoshirikiana na serikali katika kuwasaidia vijana kujiajiri kupitia fursa za uchumi wa buluu zilizopo nchini.
Kwa upande wake, Meneja wa Programu, Shirikisho la Kimataifa linaloshughulika na programu ya uendelezaji wa pwani na uvuvi wa bahari (IUCN), Dkt. Elinasi Monga alisema kuwa wao wapo tayari kushirikiana na serikali katika kuwezesha vijana kutumia fursa za uchumi wa buluu ili kujiajiri na kwa sasa wameshaanza kuwezesha baadhi ya vijana mkoani Tanga.
Halikadhalika alisema kuwa maelekezo aliyoyatoa Waziri Ulega watayafanyia kazi huku akiongeza kuwa ushirikiano wao na serikali utasaidia kufikia malengo waliyokusudia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni