Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), kuongeza uvunaji wa malisho ya mifugo katika vituo vyake vyote nchini ili jamii inayowazunguka iweze kujifunza juu ya ulimaji wa malisho.
Katibu Mkuu Nzunda amebainisha hayo (23.09.2022) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika kituo cha TALIRI kilichopo Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma pamoja na kampasi ya Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA).
Ameongeza kuwa sambamba na jamii inayoishi karibu na vituo vya TALIRI kujifunza juu ya ulimaji wa malisho ya mifugo, jamii hiyo inapaswa pia kujifunza juu ya teknolojia rahisi ya uvunaji wa malisho pamoja na kufahamishwa utaratibu wa ulimaji wa malisho ukiwemo wa undaaji wa mashamba na uvunaji wa mbegu.
Ameiasa sekta binafsi kujikita katika biashara ya malisho ya mifugo kwa kuwekeza kwenye vifaa vya uvunaji wa malisho hususan malisho ya asili ambayo kwa sasa ni biashara yenye faida kubwa ambapo robota moja linauzwa kuanzia Shilingi Elfu Nne pamoja na kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbegu za malisho ambazo zinahitajika kwa wingi.
Aidha, amewataka vijana hususan wasomi kuchangamkia fursa ya ulimaji wa malisho ya mifugo kwa kupata elimu juu ya ulimaji bora wa malisho kupitia TALIRI na hatimaye kuwekeza kulingana na maelekezo watakayopata ili walime kwa faida.
Akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa TALIRI pamoja na LITA amewataka kubadilika na kufanya kazi kutokana na mabadiliko ya mazingira ya sasa na kutofanya kazi kwa mazoea pamoja na kuacha kufanya kazi kwa malalamiko na kusubiri kila kitu kutoka serikalini, badala yake wafanye kazi kutokana na rasilimali inayopatikana kwa wakati huo na kuzidi kuboresha utendaji wao wa kazi.
Akiwa katika ziara hiyo Katibu Mkuu Nzunda ameambatana na Mwenyekiti wa bodi ya TALIRI Prof. Sebastian Chenyambuga, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Prof. Erick Komba, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa pamoja na viongozi wengine wa TALIRI na LITA, ametembelea pia ujenzi wa bweni la wanafunzi la LITA na kuutaka uongozi wa kampasi hiyo kuhakikisha jengo hilo linakamilika ifikapo tarehe 30 Mwezi Oktoba mwaka huu ili lianze kutumika.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda (wa tatu kutoka kulia), akitoa maelekezo kwa uongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), kuongeza uvunaji wa malisho ya mifugo katika vituo vyake vyote nchini ili jamii inayowazunguka iweze kujifunza juu ya ulimaji wa malisho. Bw. Nzunda amebainisha hayo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika kituo cha TALIRI kilichopo Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma pamoja na kampasi ya Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA). (23.09.2022)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda akikagua ng’ombe aina ya Mpwapwa wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma na kuitaka TALIRI kuongeza tija katika uzalishaji wa mifugo bora na kuhakikisha inazifikia jamii ili ziweze kuboresha mifugo yao. (23.09.2022)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda (wa nne kutoka kushoto) akikagua josho la kuogeshea mifugo lililopo Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, ambalo ni josho la kwanza Afrika Mashariki lililojengwa na wajerumani Mwaka 1905. Katibu Mkuu Nzunda ameshuhudia josho hilo alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika taasisi hiyo. (23.09.2022)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda (wa nne kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Sebastian Chenyambuga, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Prof. Erick Komba, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa pamoja na viongozi wa TALIRI na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Kampasi ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, wakati Katibu Mkuu Nzunda alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja na kushuhudia uimara wa josho la kuogeshea mifugo lililojengwa na wajerumani Mwaka 1905. (23.09.2022)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda akizungumza na baadhi ya wafanyakazi (hawapo pichani) wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) pamoja na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, ambapo amewataka kubadilika na kufanya kazi kutokana na mabadiliko ya mazingira ya sasa na kutofanya kazi kwa mazoea pamoja na kuacha kufanya kazi kwa malalamiko na kusubiri kila kitu kutoka serikalini, badala yake wafanye kazi kutokana na rasilimali inayopatikana kwa wakati huo na kuzidi kuboresha utendaji wao wa kazi. (23.09.2022)
Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) pamoja na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda (hayupo pichani) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma ambapo walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali na kutoa ushauri. (23.09.2022)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda (wa kwanza) akitoka kwenye jengo la bweni la wanafunzi wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) ili kushuhudia maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, ambapo ameutaka uongozi wa kampasi hiyo kuhakikisha jingo linakamilika ifikapo tarehe 30 Mwezi Oktoba mwaka huu ili lianze kutumiwa na wanafunzi. (23.09.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni