Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi amekabidhi Gari jipya aina ya HINO litakalokuwa linatumika kusafirisha Chanjo za Mifugo kutoka kituo cha uzalishaji (TVI) kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani na kuzisambaza kwa wateja maeneo mbalimbali hapa nchini.
Akikabidhi gari hilo kwa Mkurugenzi wa Huduma Saidizi siku ya tarehe 28/09/2022 Makao Makuu ya ofisi za Wakala zilizopo Temeke jijini Dar es salaam alisema kuwa, Wakala imefanikiwa kununua gari la kutunza baridi ambalo ni mahususi kwa ajili ya kusafirishia chanjo kutoka kituo cha uzalishaji chanjo kibaha na kuzisambaza kwa wateja wote nchini.
“Gari hili limenunuliwa kutokana na fedha za ruzuku ya maendeleo, nachukua fursa hii kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutenga bajeti ya maendeleo ambayo imetuwezesha kununua chombo hiki cha usafiri ambacho kitasaidia kuwafikishia wafugaji chanjo kwa wakati.” Alisema Dkt. Bitanyi
Dkt Bitanyi aliongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2022 wakala imetenga bajeti ya kununua gari jingine kama hilo litakalotumika kwa ajili ya kusafirisha chanjo maeneno mbalimbali nchini kwa kusaidiana na gari lililopo.
“Nalikabidhi gari hili kwa Mkurugenzi wa Huduma saidizi ambaye ndie msimamizi wa shughuli za Wakala, na natoa rai kwa watakaokabidhiwa gari hili kulitunza kwa kuhakikisha linafanyiwa marekebisho (Services) kwa wakati ili liendelee kuwepo na kufanya kazi kwa ufanisi na kutokwamisha shughuli za usafirishaji na usambazaji wa chanjo.” Alisema Dkt. Bitanyi
Akipokea Gari hilo Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania Ndg Henry S. Mwaijega, amemshukuru Mtendaji mkuu kwa kuwakabidhi gari la usafirishaji wa chanjo kwani litasaidia katika kuboresha na kupanua huduma zinazotolewa na Wakala, vilevile ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa.
“Tuzingatie yale yote yaliyoagizwa na Mtendaji Mkuu kwani Serikali imeamua kutenga fedha kununua chombo hiki ili kurahisisha utekelezaji wa shughuli za usafirishaji chanjo, na kila atakaepewa dhamana ya kulitumia ahakikishe analitunza ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli zilizokusudiwa” alisema Ndg. Mwaijega.
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania-TVLA ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi inayojishughurisha na Uchunguzi wa Magonjwa ya Wanyama, Uzalishaji wa Chanjo za Mifugo, Uhakiki wa Ubora wa Vyakula vya Mifugo, Uhakiki wa ubora wa viuatilifu vya Mifugo, Utafiti wa magonjwa ya Wanyama pamoja na Huduma za ushauri.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Gari jipya aina ya HINO litakalokuwa linatumika kusafirisha Chanjo za Mifugo kutoka kituo cha uzalishaji (TVI) kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani na kuzisambaza kwa wateja maeneo mbalimbali hapa nchini leo tarehe 28/09/2022 Makao Makuu ya ofisi za Wakala zilizopo Temeke jijini Dar es salaam kulia kwake ni Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala Ndg Henry S. Mwaijega.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi akipata maelezo ya namna ya kulitumia Gari jipya la kusafirisha Chanjo za Mifugo kutoka kwa dereva wa gari Ndg. Salim Mbalazi leo tarehe 28/09/2022 Makao Makuu ya ofisi za Wakala zilizopo Temeke jijini Dar es salaam ambapo gari hilo litakuwa linasafirisha chanjo kutoka kituo cha uzalishaji (TVI) kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani na kuzisambaza kwa wateja maeneo mbalimbali hapa nchini ajili ya kutumika
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni