Na Mbaraka Kambona,
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewahimiza Wadau wa Sekta ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika (AU) kuhakikisha wanakuwa na mpango madhubuti wa pamoja wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali hizo ili mchango wake uwe na manufaa makubwa zaidi kwao.
Aliyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha kurasimisha mpango wa kusimamia rasilimali za Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo unaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 26-28, 2022.
Alisema ni wakati sasa nchi za Afrika kuwa na utaratibu wa pamoja wa kuratibu usimamizi wa uendelezaji wa rasilimali za uvuvi utakaosaidia kulinda ubora, usalama, kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kukuza soko la mazao hayo ndani na nje ya Jumuiya hiyo.
"Nimewasisitiza wadau hawa walioshiriki kikao hiki kuwa ni muhimu kutoka na maazimio yatakayosaidia kuratibu vyema uendelezaji wa rasilimali za uvuvi kuliko ilivyo hivi sasa ambapo kila nchi ina namna yake ya kuendesha shughuli hizo", alisema
Aliongeza kwa kusema kuwa nchi hizo pia ziendelee kuelimisha wananchi wao juu ya uvuvi endelevu kwa kuzingatia Sheria na kanuni zilizopo katika maeneo yao.
Kuhusu changamoto za masoko, Waziri Ndaki alisema ni muhimu wanajumuiya hao kuona namna watakavyo zitafutia majawabu ili mazao ya uvuvi yaweze kupata soko kubwa zaidi katika nchi za nje ikiwemo ulaya na china ili nchi za Afrika ziweze kufaidika zaidi na rasilimali zake.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya kimataifa inayoshughulika na usimamizi wa rasilimali za mifugo (AU-IBAR), Bi. Francisca Gonah(katikati) muda mfupi kabla ya kufungua kikao kazi cha kurasimisha mpango wa usimamizi wa rasilimali za Uvuvi na Ufugaji wa Viumbe Maji kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika unaofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 26-28, 2022. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Uvuvi Tanzania, Bw. Emmanuel Bulayi.
Pichani ni sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha kurasimisha mpango wa usimamizi wa rasilimali za Uvuvi na Ufugaji wa Viumbe Maji utakaotumiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku tatu kuanzia Septemba 26-28, 2022.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na Washiriki wa kikao kazi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika (hawapo pichani) cha kurasimisha mpango wa usimamizi wa rasilimali za Uvuvi na Ufugaji wa Viumbe Maji unaofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 26-28, 2022.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni