WAFUGAJI WASHAURIWA KUWEKEZA KATIKA KILIMO CHA MALISHO
Wafugaji wa Ng’ombe wameshauriwa
kujikita katika kilimo cha Malisho ili wawe na uhakika wa malisho bora kwa
ajili ya mifugo yao na kuachana na uchungaji wa kutafuta malisho.
Mtendaji Mkuu wa Shamba la Ndoto,
Hartmut Rottcher aliyasema hayo kwa Wakurugenzi na Mameneja wa Wizara ya Mifugo
na Uvuvi waliotembelea shamba la mfano la Ndoto lililopo Mkoani Iringa Novemba
27, 2020.
Rottcher alisema kilimo cha malisho
yaliyo bora kinasaidia kuwapatia mifugo uhakika wa chakula bora huku akieleza
kuwa mifugo ni muhimu kupewa pumba kwa kiasi na sio kuzidisha kwani
kufanya hivyo hupelekea ng’ombe kupata asidi tumboni na kuuwa bakteria ambao
husaidia kukata kata majani tumboni kwa mnyama.
Alisema kuwa yeye anafanya kilimo
cha malisho kwa kumwagilia na ametenga maeneo katika mashamba yake illi
kusaidia kulisha mifugo kwa mzunguko na kuipatia mifugo mahitaji
wanayotaka na sio kuletewa chakula kwenye maboma yao.
“Njia ya kulisha kwa mzunguko
husaidia kupata muda wa kuondoa magugu na kufanya shamba kuwa safi na malisho
kustawi vizuri kwa wakati na linakuwa na rutuba ya kutosha,” alisema Rottcher
“Kulisha chakula cha kutosha na cha
aina tofauti husaidia mnyama kupata virutubisho vingi vinavyosaidia
kujenga afya ya mifugo,” Aliongeza Rottcher
Aidha, aliwashauri Wakurugenzi na
Mameneja wa mashamba ya Serikali kutoa mifugo kwenda kujitafutia chakula na sio
kuwaletea katika maboma yao kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia mifugo kupata
kile wanachotaka na sio kuwapimia chakula jambo ambalo litawezesha kupata
mifugo iliyo bora yenye nyama nyingi na maziwa ya kutosha yenye viwango.
Akieleza kuhusu ziara yao katika
Shamba hilo, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani Dkt. Kejeri Gillah alisema
lengo ni kujifunza na kubadilishana uzoefu katika kuboresha kosaafu na utunzaji
wa mifugo, ustawishaji wa malisho bora kwa mifugo ya aina mbalimbali na namna
ya uhifadhi wa malisho kwa matumizi ya kipindi cha kiangazi.
“Ni mategemeo yetu kwamba safari hii
itakuwa ya mafanikio makubwa sana kwetu na tutaweza kuboresha mifugo yetu na
kustawisha malisho ya mifugo kama tutafuata yale yote tutakayoelekezawa”
alisema Dkt. Gillah
Ziara hiyo iliratibiwa na Idara ya
Utafiti, Mafunzo na Ugani, ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za
Ugani, Dkt. Kejeri Gillah, wengine walishiriki katika ziara hiyo ni Mameneja
kutoka Shamba la kitulo, Sao hill, Langwira, Vikuge, Mkurugenzi wa Taasisi ya
Utafiti wa Mifugo (TALIRI) Uyole na meneja wa Ranchi ya Kalambo.
Afisa Utafiti Mifugo Mkuu
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Felista Kimario akitoa neno la shukrani
kwa Mtendaji Mkuu wa shamba la Ndoto, Bw. Hartmut Rottcher (hayupo pichani) kwa
kutumia muda wake kuwatembeza kwenye shamba hilo na kuwaelimisha mambo
mbalimbali katika upandaji wa malisho, namna ya kutunza na kulisha Mifugo.
(27.11.2020)
Mtendaji Mkuu wa shamba la
Ndoto, Bw. Hartmut Rottcher (wa pili kutoka kulia) akiwatembeza watumishi wa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliofika shambani hapo kujionea na kujifunza namna ya ustawishaji wa
malisho, uboreshaji wa kosaafu na utunzaji Mifugo. (27.11.2020)
Kaimu Mkurugenzi kutoka
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Uyole Mbeya, Dkt. Edwin Peter Chang'a (katikati)
akiuliza swali kwa Mtendaji Mkuu wa shamba la Miombo, Bw. Rex Fey (wa pili
kushoto) wakati wa safari yao ya Mafunzo Mkoani Iringa. (27.11.2020)
Mtendaji Mkuu wa shamba la
Ndoto mkoani Iringa, Bw. Hartmut Rottcher akiwaeleza watumishi wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi aina ya nyasi za malisho zilizopo shambani hapo na namna
anavyofanya kilimo cha malisho ya Mifugo. (27.11.2020)
Watumishi kutoka katika
mashamba mbalimbali ya Mifugo yaliyopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi
wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa shamba la Miombo, Bw. Rey Fey (kushoto) wakati
akizungumzia kuhusu mbegu, malisho na namna bora ya kulisha Mifugo kwenye
shamba la Ndoto lililopo mkoani Iringa. (27.11.2020)
Kaimu Mkurugenzi Ugani Mifugo
kutoka WMUV, Dkt. Kejeri Gillah akieleza lengo la safari yao ya Mafunzo wakati
walipotembelea shamba la Ndoto mkoani Iringa, kuwa ni kubadilishana uzoefu
katika uboreshaji wa kosaafu, utunzaji Mifugo, uhifadhi bora wa malisho,
Udhibiti wa Magonjwa na matumizi ya madawa. (27.11.2020)
Kaimu Mkurugenzi Ugani Mifugo
kutoka WMUV, Dkt. Kejeri Gillah akieleza lengo la safari yao ya Mafunzo wakati
walipotembelea shamba la Ndoto mkoani Iringa, kuwa ni kubadilishana uzoefu
katika uboreshaji wa kosaafu, utunzaji Mifugo, uhifadhi bora wa malisho,
Udhibiti wa Magonjwa na matumizi ya madawa. (27.11.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni