Bodi ya Maziwa yasisitiza ushirikiano na sekta binafsi katika kuongeza usindikaji wa maziwa nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Msajili wa
Bodi ya Maziwa, Bw. Noely Byamungu wakati wa kikao kazi cha kubainisha maeneo
ya ushirikishwaji na Sekta Binafsi kilichofanyika jana (20.11.2020) jijini Dar
es Salaam.
Kikao kazi hicho kililenga
kupitia Mpango Mkakati wa miaka mitano 2020/21-2025/26 wa Bodi ya Maziwa na
kubainisha namna ya bora ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika utekelezaji
wa majukumu ya Bodi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Wakurugenzi
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Makampuni ya Wasindikaji
Maziwa ya UHT nchini kutoka kampuni ya Asas Dairies, Tanga Fresh, Milkcom na
Azam Dairies, Wabia wa maendeleo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania
(TADB) na Mradi wa Wasindikaji wa Maziwa Tanzania (TMPP).
Bw. Byamungu alisema kuwa
lengo la Bodi ya Maziwa ni kuwezesha viwanda kuongeza uwezo wa kusindika maziwa
ambao kwa sasa usindikaji wa maziwa katika viwanda hivyo ni asilimia 23.52.
Aidha, Msajili amesema kuwa
Bodi ya Maziwa ipo tayari kuunga mkono jitihada za wadau wa Tasnia ya Maziwa
kufikia malengo yao ya kuzalisha maziwa kwa kiwango kilichosimikwa.
Bw. Byamungu alisema kuwa
kikao hicho kitaleta mtazamo wa muda mrefu wa Tasnia ya maziwa katika
usindikaji na kutoa ramani ya kuongezeka kwa ushirikishwaji wa wadau,
mawasiliano na ushirikiano miongoni mwa sekta binafsi, wabia wa maendeleo na
wadau wengine kwenye sekta.
"Bodi ya Maziwa iko
tayari na ina nia njema ya kufanya kazi pamoja nanyi kufikia malengo ya kuwa sekta
endelevu katika uzalishaji, usindikaji na masoko ya maziwa na bidhaa zake
nchini" Alisema Bw. Byamungu.
Nae Mkurugenzi wa Mradi wa
Wasindikaji Tanzania, Bw. Mark Tsoxo amesema wapo tayari kuisaidia Bodi ya
Maziwa kutekeleza majukumu yake ya kuongeza usindikaji wa maziwa nchini ili
kuimarisha mnyororo mzima wa thamani. Pia ameiomba Bodi ya Maziwa kuendelea
kushirikiana na Sekta Binafsi kwa Ukaribu ili kufikia azma iyo.
Tasnia ya Maziwa ina mchango
mkubwa katika kuhakikisha usalama wa chakula na kupunguza umaskini.
Washiriki wa kikao cha
"Stakeholder Engagement Towards Sustainable Dairy Industry in
Tanzania" wakiwa kwenye picha ya pamoja katika kikao kilichofanyika jijini
Dar es Salaam. (20.11.2020)
Kaimu Msajili wa Bodi ya
Maziwa, Bw. Noel Byamungu (wa kwanza kushoto) akisikiliza kwa makini mada
zinazowasilishwa na mdau (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha kuimarisha
mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali kilichofanyika jijini Dar. Es
Salaam. Kulia ni mwakilishi kutoka Azam Dairies, Bw. Yunus Ibrahim.
(20.11.2020)
Mhandisi kutoka Wizara ya
Viwanda na Biashara, Bw. Emmanuel Zakayo (kushoto) akifuatiwa na Mchumi Mkuu
kutoka Wizara ya Viwanda, Bi. Genoveva Kilabuko na Mchumi kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Bw. Francis Makusaro wakati wa kikao kazi cha kuimarisha
mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali kilichofanyika jijini Dar. Es
Salaam. (20.11.2020)
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe (WMUV), Bw. Gabriel Bura akisikiliza kwa makini mada zinazowasilishwa wakati wa kikao kazi cha kuimarisha mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali kilichofanyika jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)
Mkurugenzi Mtendaji wa
Kiwanda cha Tanga Fresh, Bw. Innocent Mushi akisikiliza mada zinazowasilishwa
wakati wa kikao cha kuimarisha mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali
kilichofanyika jijini Dar. Es Salaam. (20.11.2020)
Baadhi ya Wasindikaji wa
Maziwa wakiwa kwenye kikao cha kuimarisha mahusiano kati ya Sekta Binafsi na
Serikali kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mwakilishi
kutoka Milkcom Dairies, Bw. Abubakar Faraji, akifuatiwa na Abdul Ally kutoka ASAS
Dairies na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi mtendaji kutoka Tangafresh, Innocent
Mushi. (20.11.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni