Nav bar

Jumamosi, 21 Novemba 2020

MRADI WA SWIOFISH WASHIRIKISHA WANANCHI KULINDA RASILIMALI ZA UVUVI NCHINI

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amesema Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi Mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) umewezesha uboreshaji wa miundombinu ya taasisi za wizara hiyo katika kuhakikisha serikali kwa kushirikiana na wananchi inalinda rasilimali za uvuvi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi.

 

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwafahamisha manufaa ya mradi wa SWIOFish, Dkt Tamatamah amesema mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia umewanufaisha pia wavuvi wa Pwani ya Bahari ya hindi, wakulima wa Mwani, wafugaji wa viumbe maji na wachakataji wa mazao ya uvuvi wakiwemo wanawake na jamii inayozunguka maeneo hayo.

 

“Lengo kuu la mradi huu ni kuimarisha usimamizi madhubuti wa uvuvi katika ngazi ya kijamii, kitaifa na kimataifa na malengo mengine ni kujenga uwezo wa nchi katika kusimamia rasilimali za uvuvi, kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika ulinzi wa rasilimali za uvuvi wa Bahari kuu, kuinua uchumi wa jamii ya watu wa Pwani na kuinua pato la taifa kutokana na rasilimali za uvuvi,” Amesema Dkt. Tamatamah.

 

Aidha, Dkt. Tamatamah amesema tangu mradi huo uingie hapa nchini mwezi Juni mwaka 2015 ambapo unatarajia kukamilika mwezi Septemba mwaka 2021 uvuvi haramu wa kutumia baruti na mabomu umedhibitiwa kwa asilimia 100 kutokana na kuimarishwa kwa doria pamoja na kuongezeka kwa uelewa wa jamii ya Pwani kuhusu madhara ya uvuvi haramu.

 

Pia, amesema usajili wa vyombo vya uvuvi umeongezeka hadi kufikia asilimia 58 kutoka asilimia 25 ya awali kabla ya mradi kutokana na usimamizi wa utekelezwaji wa sheria na kanuni za uvuvi. Mradi umewezesha tafiti mbalimbali ambapo matokeo yake yametumika kurekebisha baadhi ya kanuni za uvuvi ambazo zimesaidia kuongezeka kwa samaki wanaovuliwa pamoja na kuongezeka kwa uvuvi wa karibu wa kutumia ndoano kwa maeneo mengi.

 

“Mafanikio mengine ya Mradi wa SWIOFish ni pamoja na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na uvuvi hususan kwenye halmashauri ambapo Halmashauri ya Pangani yameongezeka kutoka milioni 55 mwaka 2016/17 hadi kufikia Milioni 235 mwaka 2018/19,” Amebainisha Dkt. Tamatamah. 

 

Katika kikao hicho na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah ametumia muda huo kuelezea pia namna mradi wa SWIOFish ulivyoimarisha Sekta ya Uvuvi kwa kufadhili mafunzo ya uvuvi endelevu ambayo yamesaidia baadhi ya wavuvi kutekeleza kwa hiari usimamizi wa rasilimali za bahari.

 

Ameongeza kuwa mradi umeanzisha vikundi hamsini vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika Wilaya tano za mfano na kuimarisha utunzaji wa mazingira ya Pwani, viwango vya dagaa pamoja na Mwani vimeandaliwa na kupitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

 

Katibu mkuu huyo pia amesema mradi umewezesha ujenzi wa maabara ya utafiti iliyoko Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaaam, ujenzi wa nyumba tatu za watumishi wa Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), kituo cha Tanga Silikanti kilichopo Kigombe, wilayani Muheza, na ujenzi wa ofisi tano za BMU katika Wilaya za Mkinga (Zingibari), Pangani (Kipumbwi), Chalinze (Saadani), Bagamoyo (Dunda) na Lindi vijijini (Sudi).

 

Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa SWIOFish Tanzania Bara, Bw. Nichrous Mlalila amesema licha ya mafanikio ya mradi changamoto mbalimbali zimekuwa zikijitokeza zikiwemo za ugumu wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za kila siku za BMU, kutokea kwa baadhi ya matukio ya uvuvi haramu wa kutumia nyavu zisizofaa kisheria na upatikanaji wa takwimu sahihi katika mifumo ya ukusanyaji taarifa.

 

Bw. Mlalila amesema hadi sasa asilimia 65 ya shughuli za mradi zimetekelezwa na kukamilika, ambapo asilimia nane (8) zipo katika utekelezaji kwa zaidi ya asilimia 75, asilimai 19 ya shughuli za mradi zinaendelea kutekelezwa kati ya asilimia 25 hadi 75 ya utekelezaji. Asilimia nne (4) zipo katika utekelezaji wa asilimia chini ya 25.

 

Ameongeza kuwa mradi unaonyesha matokeo chanya na upo katika mwelekeo mzuri wa utekelezaji.

 

Akizungumza kwa niaba ya wahariri wa vyombo vya habari waliohudhuria kikao hicho Kaimu Mhariri Mkuu wa gazeti la Habari Leo Bw. Mgaya Kingoba ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Uvuvi kwa kuendelea kuwapatia taarifa mbalimbali na elimu juu ya sekta hiyo ambazo zinawasaidia kutoa taarifa sahihi kwa umma. 

 

Pia, amewaomba wahahriri wenzake kuendelea kuiunga mkono wizara hiyo katika kuhakikisha inatoa taarifa ambazo zitasaidia kulinda rasilimali za uvuvi pamoja na kupambana na uvuvi haramu katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

 

Mradi wa SWIOFish unatekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) na Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) katika maeneo ya Pwani ya Tanzania katika wilaya tano za mfano zikiwemo Mkinga, Tanga Jiji, Pangani, Bagamoyo na Lindi Vijijini. Kwa upande wa Zanzibar, Mradi unatekelezwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo, Maliasili na Uvuvi pamoja na Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA).

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya habari, baada ya kufungua kikao hicho chenye lengo la kuelezea mafanikio ya Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) katika ofisi ndogo za wizara hiyo jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)

Mratibu wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) Tanzania Bara, Bw. Nichrous Mlalila akiwaelezea wahariri wa vyombo vya habari (hawapo pichani) waliohudhuria kikao hicho kilichokuwa na lengo la kuwaelezea wahariri hao mafanikio ya mradi wa SWIOfish. Kikao hicho kimefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini wakipata maelezo na kushuhudia namna serikali inavyofuatilia vyombo vya majini vinavyofanya shughuli za uvuvi maeneo ya bahari kuu, wakati wa kikao cha Sekta ya Uvuvi na wahariri wa vyombo vya habari kilichokuwa na lengo la kuwafahamisha mafanikio ya Mradi wa (SWIOFish). Kikao hicho kimefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wahariri wa vyombo vya habari nchini, na baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya mradi wa SWIOFish, baada ya kufungua kikao cha Sekta ya Uvuvi na wahariri wa vyombo vya habari kuelezea mafanikio ya mradio huo. Kikao hicho kimefanyika katika ofisi ndogo za wizara hiyo jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni