Na Mbaraka Kambona,
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amewaeleza wanafunzi wa Chuo cha
Serikali za Mitaa- Hombolo kuwa wao ni Viongozi watarajiwa hivyo wanawajibu wa
kuhakikisha watakapokuwa viongozi wanakidhi matarajio ya wale watakaokuja
kuwaongoza.
Prof. Gabriel aliyasema hayo
wakati akiwasilisha mada iliyohusu nafasi ya viongozi wa kuchaguliwa katika
kuleta maendeleo kwa jamii anayoiongoza kwenye hafla ya kuwatunuku zawadi
wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao na wafanyakazi bora wa chuo cha
Hombolo iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma Novemba 25, 2020.
Alisema kuwa katika kipindi
hiki ambacho nchi ya Tanzania imeingia katika uchumi wa kati viongozi
wanawajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba wanakidhi matarajio ya Watanzania.
Prof. Gabriel aliongeza kuwa
nchi nyingi na taasisi zimekuwa zikikwama kufikia malengo tarajiwa kwa sababu
ya kukosa usimamizi mzuri.
“Kuwa na rasilimali ni jambo
moja, lakini kusimamia rasilimali hizo ni jambo la muhimu zaidi, taasisi nyingi
zimekwama kwa kushindwa kusimamia rasilimali zake ikiwemo rasilimali watu,
rasilimali fedha na rasilimali miundombinu,” alisema Prof. Gabriel
Kwa mantiki hiyo aliupongeza
Uongozi wa Chuo cha Hombolo kwa kusimamia agenda ya uongozi huku akisema kuwa
elimu hiyo wanayoitoa kwa wanafunzi wa chuo hicho itawasaidia wanafunzi hapo
mbeleni watakapokuwa viongozi.
Aliendelea kusema kuwa
kiongozi yeyote wa kuchaguliwa au kuteuliwa ili awe kiongozi bora ni muhimu
kuzingatia mambo matatu ambayo ni kufahamu hasa anaowaongoza wanamahitaji gani?
pia Kiongozi atambue kuwa hatakumbukwa kwa cheo chake bali kwa mchango wake kwa
jamii ile anayoiongoza na tatu, awe mtu anayewashirikisha wale anaowaongoza
katika kutatua changamoto zao.
“Washirikishe wale
unaowaongoza na ndipo utakapoweza kutatua changamoto, kiongozi mzuri ni yule
anayeziona changamoto na kuzibadilisha kuwa fursa, na kwa kufanya hivyo ndipo
utaweza kukidhi matarajio ya wale unaowaongoza,”alisisitiza Prof. Gabriel
Katika hafla hiyo ya kumi na
mbili (12) ya chuo hicho, Prof. Elisante Ole Gabriel alikuwa Mtoa mada maalum
na aliwasilisha mada hiyo ya nafasi ya viongozi wa kuchaguliwa na wakuteuliwa
katika kuleta maendeleo kwa jamii ili kuwakumbusha wajibu wao mkubwa kwa jamii.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia), akifurahia jambo
alipokuwa akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli
(kushoto) walipokutana kwenye Hafla ya
Kutunukiwa zawadi wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo cha Serikali za Mitaa-
Hombolo waliofanya vizuri katika masomo.
Prof. Elisante Ole Gabriel alikuwa Mtoa mada maalum katika hafla hiyo
iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma. (25.11.2020)
Sehemu ya Wanafunzi na
Wafanyakazi wa Chuo cha Serikali za Mitaa - Hombolo waliohudhuria hafla ya
kutunukiwa zawadi wafanyakazi na wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo
iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma. (25.11.2020)
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasalimia Wanafunzi na
Wafanyakazi wa Chuo cha Serikali za Mitaa- Hombolo (hawapo pichani) alipokuwa
akitambulishwa katika hafla ya kutunukiwa zawadi wafanyakazi na wanafunzi
waliofanya vizuri katika masomo iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma.
(25.11.2020)
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha mada katika hafla ya
kutunukiwa zawadi Wafanyakazi na Wanafunzi waliofanya vizuri wa Chuo cha
Serikali za Mitaa-Hombolo iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma.
(25.11.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni