Na Mbaraka Kambona, Singida.
Serikali kupitia Wizara ya
Mifugo na Uvuvi ipo katika mchakato wa kukamilisha Mpango kabambe wa miaka 15
ijayo kuanzia 2021 utakaosimamia sekta ya Uvuvi na kutoa dira ya kulinda
rasilimali za uvuvi ili sekta hiyo iweze kutoa mchango mkubwa na endelevu
katika pato la taifa.
Hilo limefahamika wakati
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akifungua
Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Uvuvi wa kupitia, kujadili na kuidhinisha masuala
ya kipaumbele yanayopaswa kuingizwa katika Mpango huo Kabambe unaofanyika
Mkoani Singida Novemba 26-28, 2020.
Dkt. Tamatamah alisema kuwa
lengo la Serikali ni kuona sekta ya Uvuvi inaendelea kutoa mchango mkubwa
katika pato la taifa zaidi ya ilivyosasa na ndio maana inaanda Mpango huo ili
usimamizi wa rasilimali za uvuvi uwe imara.
“Ni mategemeo yetu kuwa
mpango huu utatoa hamasa kwa sekta ya uvuvi katika kulinda usalama wa chakula
kuanzia ngazi ya kaya na taifa, vilevile tunatarajia utuingize katika uchumi wa
viwanda na uchumi wa bluu,” alisema Dkt.Tamatamah
Alisema kuwa pamoja na juhudu
za Wizara za kusimamia maendeleo ya Sekta ya Uvuvi nchini, Sekta hiyo imeendele
kukabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo kwa ujumla zimekuwa zikiathiri
ukuaji na uendelevu wa sekta hiyo.
Aliendelea kueleza kuwa ili
kukabiliana na changamoto hizo, Wizara imekuwa ikitekeleza mipango, mikakati na
programu mbalimbali zinazolenga kuendeleza sekta ya uvuvi nchini, miongoni mwa
mipango hiyo ni Mpango huo Kabambe wa Uvuvi unaotarajiwa kuanza kutumika mwaka
2021.
Mratibu wa Masuala ya Uvuvi
kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), ambao wanafadhili maandalizi
ya mpango huo, Dkt. Oliver Mkumbo alisema shirika hilo limeamua kufadhili
mpango huo ikiwa ni sehemu ya malengo yao ya kuhakikisha dunia inaondokana na
njaa, umasikini na kuimarisha usalama wa chakula ili ifikapo mwaka 2030
pasiwepo na mtu atakayekuwa na njaa.
Aidha, wadau wa Sekta ya
Uvuvi hawakusita kuonesha matumaini yao na mpango huo huku wakisema kuwa
ukikamilika utajibu changamoto nyingi ambazo zimeendelea kukabili sekta hiyo.
Kiongozi wa Wavuvi Mkoani
Kigoma, Francis John alisema kuwa mpango huo ambao utasimamia rasilimali za
uvuvi utawasaidia kuimarisha biashara yao ya dagaa kutoka ziwa Tanganyika kwani
mpango huo utawahakikishia uwepo wa dagaa wengi ambapo wataweza kuwa na mzigo
wa uhakika wa kusafirisha kwenda kuuza dagaa wao katika nchi za Marekani,
Astralia, Kanada, Uingereza na Denmark.
Naye, Raphael John, mdau wa
sekta hiyo ya Uvuvi alisema kuwa moja ya
mambo yatayokwenda kuimarishwa kupitia mpango huo ni ufugaji na ukuzaji wa
viumbe maji jambo ambalo anasema litasaidia kupunguza utegemezi wa kupata mazao
ya uvuvi kutoka maji ya asili pekee.
“Katika nchi nyingi
zilizoendelea, ufugaji na ukuzaji wa viumbe maji umepewa kipaumbele sana, ni
muhimu kuimarisha eneo hilo ili tusitegemee tu uvuvi wa mazao ya samaki katika
maji ya asili, ni lazima tuanze sasa kabla rasilimali za asili katika bahari,
mito na maziwa hazijaisha,” alisema John
Mpaka sasa sekta ya uvuvi
inachangia asilimia 1.7 katika pato la Taifa huku ikielezwa kuwa sekta hiyo
inatoa ajira ya moja kwa moja kwa wananchi takriban 202,000 na wananchi wengine
wasiopungua Milioni 4.5 wamaendelea kutegemea kupata kipato chao kupitia sekta
hiyo.
Shirika la Chakula na Kilimo
Duniani (FAO) limetoa Dola za Kimarekani 195,000 kwa ajili ya kufanya mapitio
na kuandaa Mpango huo Kabambe wa sekta ya uvuvi ili sekta hiyo iweze kusimamiwa
vizuri na kuendelea kuleta maendeleo yenye tija nchini.
Uandaaji wa mpango huo ni sehemu ya mipango mingi ambayo serikali imekusudia kuitekeleza, wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 13, 2020 jijini Dodoma, Mhe. Rais, Dkt. John Joseph Magufuli alieleza mipango kadhaa ya kuboresha sekta ya uvuvi ikiwemo ununuzi wa meli nane (8), ujenzi wa Bandari kubwa ya uvuvi itakayotoa ajira elfu thelathini (30,000).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni