Baraza la Veterinari Tanzania limekifungia kituo cha huduma ya afya ya wanyama cha Sendeu kilichopo Wilayani Longido, Mkoani Arusha kwa kubainika kutokuwa na wataalam waliosajiliwa na Baraza hilo.
Baraza limefikia hatua hiyo
mkoani humo Novemba 22, 2020 kufuatia ukaguzi unaoendelea kufanywa katika mikoa
mbalimbali nchini na wakaguzi wa baraza hilo ikiwa ni sehemu ya majukumu yao ya
kila siku.
Msajili wa Baraza Veterinari
Tanzania, Dkt. Bedan Masuruli alieleza kuhusu uamuzi huo wa baraza ofisini
kwake, jijini Dodoma Novemba 23, 2020.
Dkt. Masuruli alisema kuwa
uamuzi huo wa baraza umefikiwa baada ya kujiridhisha kuwa kituo hicho cha afya
ya wanyama kinaendesha shughuli zake kinyume cha taratibu.
Aliongeza kuwa wakaguzi wa
baraza walipoenda kufanya ukaguzi katika kituo hicho walibaini mapungufu hayo
ambayo kimsingi ni kinyume cha taratibu na ni hatari kwa afya ya wanyama.
Aidha, Dkt. Masuruli aliwahimiza wamiliki wote
wa vituo vya afya ya mifugo kuhakikisha kuwa vituo hivyo vinasimamiwa
kikamilifu na huduma zinazotolewa na wataalam wa mifugo waliosajiliwa na baraza
la veterinari Tanzania.
Dkt. Masuruli amevisisitiza
vituo vingine vyote nchini kuzingatia taratibu zote za kutoa huduma, na baraza
halitasita kuchukua hatua kwa vituo vyote vitakavyoshindwa kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu za utoaji huduma ya afya ya wanyama.
Awali msajili wa Baraza hilo
alisema walifanya ukaguzi kwenye mikoa ya Tanga, Shinyanga, Simiyu na Ruvuma na
kubaini changamoto za ukiukwaji wa maadili ya utoaji huduma ya afya ya wanyama
na kupelekea kulipishwa faini na
wengine kufungiwa kutoa huduma ya afya ya wanyama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni