SERIKALI kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema kuwa inaendelea na majadiliano na Wadau wa sekta ya Mifugo nchini ili kuona namna bora ya kushirikiana na vijana waliopo kwenye Programu ya BBT -LIFE katika kunenepesha Mifugo na kuisafirisha kwenye masoko ya nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo) Dkt. Daniel Mushi wakati wa kikao kati ya menejimenti ya sekta mifugo na wadau kuhusu kuwaunga mkono vijana waliopo kwenye programu ya BBT- LIFE , jijini Dodoma, tarehe 06.10.2023.
Dkt.Mushi amebainisha kuwa wamekutana na Kampuni za ELIA FOOD na TANCHOICE Limited za uchakataji nyama kwa ajili ya kutengeneza muunganiko wa BBT -LIFE na Soko kubwa la nje ya nchi la uuzaji wa mazao ya Mifugo ili kukabiliana na changamoto ya masoko ya mifugo kwa vijana wa BBT-LIFE.
"Tumefikiria kuwa tukiwapata wanunuzi wakubwa wa Mifugo programu yetu ya BBT - LIFE itakuwa imefanikiwa katika kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia fursa hii ya wadau “, Amesema Dk. Mushi.
Pia alisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha Mifugo haisafirishwi nje ya nchi ikiwa hai bali ichakatwe ndani ya nchi ili kuleta ajira kwa vijana hapa nchini na hatimaye kunufaika na rasilimali zilizopo na kuongeza pato la taifa.
Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu huyo,amefafanua kuwa,Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kuanzisha Vituo vingine zaidi vya BBT -LIFE kwa ajili ya Vijana ambao watakuwa wanashirikiana na wadau mbalimbali katika biashara hiyo ya mifugo.
Naye mmoja wa wadau hao Dkt.Sele Luwongo kutoka kampuni ya TANCHOICE Limited ambayo ni machinjio na kiwanda cha kuchakata nyama amesema wao kama sekta binafsi wako tayari kushirikiana na Serikali katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za masoko kwa mifugo ya vijana waliopo kwenye prigramu ya BBT -LIFE .
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni