Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amewasihi wadau kuwekeza kupitia Sekta za Mifugo na Uvuvi wilayani pangani ili kuongeza uzalishaji na tija.
Naibu Waziri Mnyeti ameyasema hay oleo
(03.10.2023) wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Wilaya ya Pangani
Mkoani Tanga ambapo aliwaeleza washiriki kuwa zipo fursa nyingi kupitia sekta
za mifugo na uvuvi.
Wadau wamehimizwa kutumia fursa zilizopo
katika ufugaji wa mifugo na samaki kwa kuhakikisha wanaongeza uzalishaji na
uongezaji wa thamani wa mazao ya mifugo na uvuvi ili kuongeza ajira, kipato na
mchango wa sekta hizo kwenye pato la taifa.
“Niwaombe wadau kuja kuwekeza hapa
pangani kupitia sekta hizi za mifugo na uvuvi kwa kuwa fursa zipo kuanzia
kwenye kuongeza uzalishaji na uongezaji wa thamani wa mazao ya mifugo na uvuvi,
hivyo kupitia kongamano hili ni vema tukazitumia fursa hizi kwa ajili ya kuleta
maendeleo yetu, ya wanapangani na taifa kwa ujumla,’ alisema
Naibu Waziri Mnyeti pia amewasihi
wafugaji kufuga mifugo iliyobora ambayo inakuwa na thamani kubwa badala ya kuwa
na ng’ombe wengi ambao tija yake ni ndogo na hivyo kusababisha migogoro ya
ardhi. Amewashauri wafugaji kuanza kubadilisha mifugo yao kwa kutumia njia ya
uhimilishaji pamoja na kupunguza ng’ombe wengi ambao tija yake ni ndogo na
kununua ng’ombe ambao ni wakubwa na wanauwezo wa kutoa maziwa mengi.
Aidha, amewasihi wadau kutumia fursa ya
uwepo wa bandari wilayani Pangani kwa shughuli za uvuvi kwa kuzingatia sheria
kwani bila hivyo serikali itaendelea kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka. Naibu
Waziri Mnyeti amesema kwa sasa serikali imejipanga kuwashughulikia wauzaji wa
nyavu zisizokidhi vigezo kwa kuwa wao ndio wanaowauzia wavuvi.
Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara,
Mhe. Exaud Kihale amesema serikali imeweka mazingira wezeshi ya kuhakikisha
wadau hawakwamishwi pale wanapokuwa na lengo la kuwekeza hapa nchini. Hivyo
amewasihi wadau kupitia kongamano hilo kwenda kuwekeza wilayani pangani kwa
kuwa fursa zilizopo ni nyingi kupitia sekta mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mhe. Zainab
Issa amesema wilaya imejipanga kupokea wawekezaji na kwamba suala la umeme upo
katika vijiji vyote, mradi wa maji unaendelea kukamilishwa kwenye maeneo ambayo
yanachangamoto na kwa upande wa barabara mkandarasi anaendelea na kazi. Hivyo
wawekezaji walio na nia wamekaribishwa kuwekeza wilayani Pangani. Lakini pia
ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuangalia uwezekano wa kujenga bandari ya
mifugo wilayani humo ili mifugo na mazao yake yawe yanasafirishwa kupitia
bandari hiyo.
Kongamano hilo ambalo lilikuwa na lengo
la kutangaza fursa mbalimbali zilizopo wilayani pangani liliwashirikisha wadau
kutoka sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na wizara za kisekta na taasisi ambapo
wawakilishi walipata fursa ya kuelezea nini taasisi zao zinafanya ili kuweka
mazingira sahihi ya biashara na uwekezaji.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.
Alexander Mnyeti akizungumza na wadau walioshiriki kwenye uzinduzi wa Kampeni
ya Upandaji wa Malisho, Uchimbaji wa Visima na Malambo katika Mashamba Binafsi
ya Wafugaji, Hamasa ya Kilimo Biashara na Rafiki kwa Mazingira
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni