Kampuni ya Kahama Fresh inayomiliki Kiwanda cha kusindika maziwa na Shamba la mifugo imeunga mkono Programu ya BBT kwa kutoa ng'ombe wa maziwa (mitamba) watano (5) kwa kikundi cha vijana 17 ili kuwawezesha kujishughulisha na uzalishaji wa maziwa na kujiongezea kipato.
Tukio hilo limefanyika katika shamba la mifugo la kampuni hiyo lililopo wilayani Karagwe, Mkoani Kagera leo Oktoba 5, 2023.
Akizungumza wakati wa kukabidhi ng'ombe hao kwa vijana, Waziri Ulega alimpongeza Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Bw. Josam Ntangeki kwa kuunga mkono Programu ya BBT kwa vitendo.
"Nampongeza Ndugu Josam kwa kuunga mkono Programu hii ya BBT kwa kuwakopesha ng'ombe wa maziwa vijana wetu kupitia mpango wa Kopa Ng'ombe Lipa Maziwa ili kuwawezesha vijana wetu kuzalisha maziwa kwa wingi na kuyapeleka katika viwanda vya uchakataji wa maziwa kikiwemocha Kahama Fresh", alisema Mhe. Ulega
Aliongeza kwa kusema kuwa programu hiyo ya BBT haiwezi kuendeshwa na Serikali peke yake bila ya wadau wa maendeleo, hivyo Kampuni ya Kahama Fresh wameunga mkono Programu hiyo kwa vitendo huku akisema kitendo hicho kitatoa hamasa kwa wadau wengine kujitokeza.
Aidha, Waziri Ulega aliwakikishia wadau wote kuwa wataendelea kushirikiana nao ili programu hiyo ya kielelezo ya BBT ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan iweze kushamiri na vijana wengi waweze kupata fursa za kujiajiri.
Halikadhalika, Waziri Ulega amewahimiza wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kuunga mkono Programu hiyo ili kwa pamoja waweze kushirikiana katika kuleta mabadiliko ya kweli katika sekta za uzalishaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Bw. Josam Ntangeki ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapa fursa ya kuendesha shughuli zao huku akisema kuwa wametoa mitamba hiyo ili kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwawezesha vijana kupata fursa mbalimbali za kujiajiri kupitia sekta za uzalishaji.
Kahama imetoa ng'ombe hao kupitia programu Kopa Ng'ombe Lipa Maziwa unaotekelezwa na Shirika la kimataifa la Heifer International kupitia mradi wa kuboresha sekta ya maziwa (TI3P) kwa Kanda ya Ziwa na Zanzibar ambao unaofadhiliwa na Taasisi ya Bill and Melinda Gates (BMGF) kupitia Benki ya Maendeleo ya kilimo nchini (TADB).
Tukio hilo la utoaji ng'ombe watano kwa vijana ni sehemu ya uzinduzi wa mpango wa ukopeshaji ng'ombe Mia Sita (600) watakaotolewa na TADB kupitia programu ya Kopa Ng'ombe Lipa Maziwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni