Nav bar

Jumatatu, 9 Oktoba 2023

KAMPENI YA TUTUNZANE MVOMERO DAWA YA MIGOGORO YA ARDHI

Kampeni ya upandaji wa Malisho ya mifugo, uchimbaji wa visima na malambo katika mashamba binafsi ya wafugaji, hamasa ya kilimo biashara na rafiki kwa mazingira imelenga kutatua migogoro ya ardhi wilayani Mvomero.

 

Kampeni hii inayokwenda na kauli mbiu, “Mfugaji Mtunze Mkulima, Mkulima Mtunze Mfugaji ili Kulinda Mazingira Yetu” inalenga kuwaelimisha kwanza kuanza kumiliki ardhi kwa ajili ya kupanda malisho ya mifugo yao na kuanza kufuga mifugo inayoendana nae neo la ardhi wanalomiliki ili kuondokana na migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kutokana na wafugaji kuhamahama.

 

Akizungumza wakati wa kuhitimisha jukwaa la maandalizi ya kampeni hiyo ijulikanayo kama Tutunzane Mvomero, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amesema kuwa utekelezaji wa kampeni hiyo unakwenda kutatua tatizo la migogoro ya ardhi iliyopo kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hasa wakulima.

 

Naibu Waziri Mnyeti amesema kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi imekuwa ikijitokeza kutokana na kutokuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji na kwenye maeneo ambayo tayari mipango hiyo usimamizi wake unakuwa hafifu. Hivyo amewasihi viongozi wa Mvomero kuhakikisha vijiji vinakuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuusimamia.

 

Wafugaji wameendelea kuhimizwa kumiliki maeneo kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kufuata sheria na taratibu zilizopo ili wasiingie kwenye migogoro ambayo inaweza kusababisha uvuvnjifu wa amani. Naibu Waziri Mnyeti amewaeleza wafugaji kuwa Wizara kwa sasa imejipanga kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mwananchi hivyo ikiwa kosa linakuwa kwa mfugaji au mkulima basi kila mmoja atachukuliwa hatua kulingana na sheria na taratibu zilizopo.

 

Jukwaa hilo la maandalizi ya kampeni ya tutunzane Mvomero limefanyika likilenga kumaliza migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima na watumiaji wengine wa ardhi inamalizika na kuwafanya wananchi wote kuishi kwa amani na utulivu.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni