◾ Meneja SAO-HILL atoa motisha ya Maji na Maziwa kwa wachezaji
Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kwa upande wa sekta za Mifugo na Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Mhina na Bw. Emmanuel Kayuni wametembelea kambi ya timu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi inayoshiriki michuano ya SHIMIWI iliyopo kwenye viunga vya chuo kikuu cha Mkwawa mkoani Iringa leo Oktoba 04, 2023 ambapo mbali na kutoa pongezi kwa timu hiyo kufanya vizuri kwenye michezo mbalimbali wamewasilisha salamu kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kwa upande wa sekta ya Uvuvi Bw. Emmanuel Kayuni amevitaka vikosi vyote vya Wizara hiyo kuhakikisha vinashinda kwenye michezo yake yote iliyosalia na kupunguza matokeo ya sare ambayo timu ya mpira wa miguu imeyapata kwenye baadhi ya mechi zake.
“Lakini jambo la pili naomba tusiendekeze sana haya mambo ya kupewa ushindi wa mezani, tunataka kucheza na yoyote tuliyepangiwa naye na tumfunge ili afahamu umahiri tulionao kwenye upande wa michezo” Ameongeza Bw. Kayuni
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka sekta ya Mifugo Dkt. Charles Mhina ameupongeza uongozi wa kamati ya michezo wa Wizara hiyo kwa kutafuta kambi tulivu yenye madhari ya kuwawezesha wanamichezo kujiandaa vema na mechi mbalimbali za michuano hiyo.
“Katibu Mkuu alipanga kuja ili kuungana nasi leo kwenye sherehe za ufunguzi wa michuano hii lakini kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine ya kikazi ametuagiza mimi na mwenzangu kufika kwenye ufunguzi na kuja kuungana na nyie hapa kambini ili kufahamu kama mna changamoto zozote tuweze kuziwasilisha kwao” Amebainisha Dkt. Mhina.
Akielezea hali ya kambi na ushiriki wa Wizara kwa ujumla kwenye michuano hiyo Mwenyekiti wa kamati ya Michezo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Ally Suru aliwaeleza viongozi hao kuwa wachezaji wote wapo salama kambini na kuwahakikishia kuendelea kufanya vizuri kwenye michezo inayofuata kutokana na maandalizi yanayoendelea kwa upande wa timu zote.
Aidha Bw. Suru aliushukuru uongozi wa Wizara kwa ujumla kwa mchango mkubwa wanaoendelea kuutoa kwa timu zake ambapo aliwaahidi kuendelea kudumisha nidhamu wakati wote wa michuano hiyo kama ambavyo timu hizo zimekuwa zikifanya tangu alipochaguliwa kushika wadhifa huo.
“Lakini pia nitumie fursa hii kutoa shukrani za dhati kwa wakuu wa Taasisi za TVLA ambao wametupa wachezaji 7 na kuwagharamia 6, Deep Sea kutoka Zanzibar ambao tuliwaomba wachezaji 3 walikubali na wote waliwagharamia, LITA ambao tuliwaomba wachezaji 4 wametupa wote na kuwagharamia 2, Bodi ya Nyama ambao tuliwaomba mchezaji mmoja walitupa na kumgharamia na Bodi ya Maziwa ambao tuliwaomba wachezaji 3, wametupa wawili na kumgharamia mmoja” Amesisitiza Bw. Suru.
Naye Meneja wa Shamba la Mifugo la SAO-HILL lililopo Mafinga mkoani Iringa Bw. Noel Byamungu ambaye amewapelekea wachezaji hao katoni za maziwa na maji amebainisha kuwa hatua hiyo imetokana na kuguswa kwake na matokeo mazuri ambayo vikosi mbalimbali vya timu hiyo vimekuwa vikipata na hivyo kuwapa motisha ili wafanye vizuri zaidi.
“Mmekuja kwenye mkoa ambao mimi ni mwenyeji hivyo nikaona ni vizuri nije kuwapa sapoti kidogo na ninatumai mtaendelea kufanya vizuri zaidi kwenye michezo inayofuata.” Amehitimisha Bw. Byamungu.
Michuano hiyo ya SHIMIWI inatarajiwa kuendelea kesho kwa mchezo wa riadha ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kuwa na wawakilishi katika mchezo huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni