◾ Ni baada ya kutoa suluhu dhidi ya MSD
Timu ya soka kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanikiwa kufuzu hatua ya 16 bora ya Michuano ya SHIMIWI inayoendelea mkoani Iringa baada ya kutoka suluhu na timu ya MSD kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa mkwawa 2 leo Oktoba 03, 2023.
Mchezo huo uliokuwa na upinzani mkali kutokana na kila timu kuhitaji pointi 3 muhimu ili iweze kufuzu hatua hiyo ulishuhudia timu zote zikitengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia jambo lililoufanya kuwa mgumu zaidi hasa kwa upande wa MSD ambao kwa namna yoyote walihitaji kushinda mchezo wa leo.
Upinzani mkali uliokuwepo baina ya timu hizo mbili ulishuhudia mlinzi wa kati Abdallah Bajwala kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kiungo Omary Kibaranga kutoka MSD wakitolewa nje kwa kadi nyekundu ambapo Bajwala alioneshwa kadi hiyo baada ya kuunawa mpira huku akiwa mchezaji wa mwisho kwenye lango lao na Kibaranga aliadhibiwa mara baada ya kumsukuma mwamuzi baada ya kutoridhika uamuzi wake.
Kwa matokeo hayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetangulia kwenye hatua ya 16 bora ikiwa imefikisha pointi 6 huku ikisubiri timu ya pili kati ya Mawasiliano na TAKUKURU ambao wanakutana leo na kila mmoja akiwa na pointi 4.
Kama yoyote kati ya timu hizo itaibuka na ushindi itafikisha pointi 7 na kuongoza kundi huku Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakishika nafasi ya pili na kama watatoa sare ya aina yoyote timu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi itasalia kinara wa kundi hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni