Nav bar

Jumatatu, 9 Oktoba 2023

MIFUGO NA UVUVI YATINGA NUSU FAINALI KIBABE!

◾ Kukutana na Katiba na Sheria Oktoba 10 


Timu ya soka ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetinga hatua ya nusu fainali ya Michuano ya SHIMIWI inayoendelea mkoani Iringa baada ya kuifumua timu ya bunge kwa magoli 2-1 kwenye mchezo uliochezwa leo Oktoba 08, 2023 uwanja wa Samora mkoani humo.


Katika mchezo huo uliokuwa wa kasi kwa pande zote mbili timu ya Wizara ya Mifugo iliweka kimiani magoli yake kupitia kwa mlinzi wa pembeni Ignatus Mwasa aliyefunga kwa shuti kali la  mpira wa adhabu dakika ya 06 ya mchezo kabla ya timu ya bunge kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji wao Mnubi Kajobi dakika ya 37 na kufanya timu hizo kwenda mapumziko wakiwa wametoshana nguvu.


Timu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilianza kipindi cha pili kwa kasi kubwa huku ikielekeza mashambulizi ya nguvu upande wa Bunge hali iliyoilazimu timu yote kurudi nyuma kwa ajili ya kuzuia mashambulizi hayo.


Mashambulizi hayo makali ya timu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi yalizaa matunda katika dakika ya 71 baada ya kupata goli la ushindi kupitia kwa kiungo wao Hema Mughenyi aliyekuwa nyota wa mchezo wa leo na mwiba kwa timu ya Bunge ambapo alipachika bao hilo kwa mpira wa kona uliozama moja kwa moja wavuni.


Timu ya soka ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatinga hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kushiriki michuano hiyo ambapo msimu uliopita iliondolewa kwa matuta na timu ya Ujenzi katika hatua ya robo fainali.


Timu hiyo sasa itacheza na timu ya SHERIA kwenye hatua ya nusu fainali mchezo utakaopigwa Oktoba 10 kwenye uwanja wa Samora.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni