Nav bar

Ijumaa, 6 Oktoba 2023

WAZIRI ULEGA ATAJA FAIDA LUKUKI ZILIZOPATIKANA KUTOKANA NA MKUTANO WA AGRF 2023

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kufuatia Jukwaa la Mkutano wa Mifumo ya Chakula Barani Afrika (AGRF), Sekta ya Mifugo na Uvuvi hapa nchini zimenufaika kwa kupata fursa mbalimbali za kibiashara, uwekezaji, mitaji na masoko.


Waziri Ulega alibainisha hayo leo Oktoba 2, 2023 wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuwaelezea  mafanikio yaliyopatikana kutokana uwepo wa Mkutano wa Mifumo ya Chakula Barani Afrika (AGRF) uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 5 hadi 8, 2023.


Alisema kupitia mkutano huo  Tanzania  ilipata fursa ya kuonesha programu bunifu ya BBT ambayo ni programu ya kielelezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kupelekea kupata ahadi ya kuungwa mkono kwa Kiasi cha Dola za Marekani milioni 500 zilitolewa na wahisani kwa ajili ya kufadhili programu hiyo.


Vilevile, alisema, Benki ya CRDB imetoa ahadi ya kiasi cha Dola Milioni 50 kama mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kusaidia Vijana waliopo katika sekta za Mifugo na Uvuvi kupata mitaji.


Halikadhalika, aliendelea kufafanua kuwa, uwepo wa mkutano huo, ulivutia wadau takriban 5,400 kutoka nchi 90, ambao walipata fursa mbalimbali za kujadili mageuzi ambayo yataunda mustakabali wa bara la Afrika.


Awali, Waziri Ulega alitumia fursa hiyo kutoa shukrani  za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake wenye mtazamo wa mbali wenye dhamira ya kuinua sekta za uzalishaji zikiwemo sekta za mifugo na uvuvi.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni