Nav bar

Jumatatu, 9 Oktoba 2023

 MIKOPO NA MAFUNZO YATAJWA KUWA NA TIJA KWA WALENGWA 


 

Na. Edward Kondela

 


Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza, umesema mikopo itakayotolewa na serikali kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa wanawake wanaojihusisha na uvuvi itakuwa na tija kwa kuwa imezingatia utoaji wa mafunzo ya namna ya kutumia mikopo hiyo.


Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Bw. Binuru Shekideli amebainisha hayo (05.10.2023) wakati alipotembelewa ofisini kwake na wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wakufunzi wa vikundi vya kuweka na kukopa ili kumuarifu juu ya mradi wa kusimamia na kuendeleza uvuvi mdogo nchini ambao unatekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na FAO kwa vikundi vya FARAJA na TEGA ZIFE vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.


Bw. Shekideli amesema mikopo hiyo ni dhahiri itavifanya vikundi hivyo hususan vya wanawake wanaojihusha na masuala ya uvuvi kuwa na tija kwa kuwa licha ya kupatiwa mikopo wanapatiwa pia mafunzo na kwamba wapo pia ambao wana mitaji lakini hawana mafunzo, hivyo itakuwa fursa kwao kujifunza zaidi.


Aidha, amesema halmashauri itasimamia maelekezo yatakayotolewa na wataalamu huku akiwapongeza kwa kuweza kuwafikia na kuchagua vikundi viwili vya wanawake vinavyojihusisha na masuala ya uvuvi katika halmashauri hiyo ambavyo vimekuwa sehemu ya vikundi vya mwanzo katika mradi huo kabla ya kufikiwa kwa vikundi vingine nchini.


Nao baadhi ya wanawake kutoka vikundi vya FARAJA na TEGA ZIFE ambavyo vimepatiwa vitendea kazi vya kuendesha shughuli za kuweka na kukopa pamoja na majiko maalum yanayotumia gesi kwa ajili ya kuandalia mazao ya uvuvi wakiwemo dagaa ambao ndiyo wanashughulika nao zaidi, wamesema mafunzo hayo yamekuwa na tija kwao kwa kuwa sasa wamefahamu namna bora ya kutumia vikundi hivyo ili viwe na manufaa kwenye shughuli zao na hatimaye waweze kujiinua kiuchumi, hivyo watakuwa makini zaidi mara watakapopatiwa fedha.


Wizara ya Mifugo na Uvuvi inashirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO katika mradi wa kusimamia na kuendeleza uvuvi mdogo nchini wa namna ya upatikanaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake wanaojihusisha na uvuvi, ambapo kwa sasa mradi huo unaanza kwa kufanyiwa majaribio kwa baadhi ya vikundi vya Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza, Muleba Mkoani Kagera, Mtera Mkoani Iringa na Mkuranga Mkoani Pwani.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni