Naibu Katibu Mkuu Sekta ya
Uvuvi Dkt. Edwin Mhede amewataka wadau wa uvuvi kuhakikisha wanatumia
teknolojia za kisasa ambazo ni rahisi zitakazowezesha kukabiliana na changamoto
ya upotevu wa mazao ya Uvuvi.
Ameyasema hayo Mei 28, 2024
wakati akifungua mkutano wa Uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech
Superhighway ambao utachukua takribani miaka 7 (2024-2030) wenye lengo la
kusaidia juhudi za Serikali katika kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi.
Mkutano huo ambao
umezikutanisha nchi nne Afrika, Dkt. Edwin Mhede amesema wamejielekeza
kuhakikisha wanufaika wa mradi huo wanakuwa ni wavuvi wenyewe.
Pia amesema eneo ambalo
wanalifanyia kazi kwa kushirikiana na Worldfish pamoja na Taasisi za ndani ni kuhakikisha wanakabiliana na changamoto za
upotevu wa mazao ya uvuvi, pamoja na uharibifu mbalimbali unaojitokeza kwenye
mnyororo wa thamani wakati watu wakivua, wakisafirisha, wakiuza na kununua
samaki.
"Katika kutathimini
fikra mpya za nini kifanyike zaidi ya hiki, tumejielekeza kuyagusa matatizo ya
wavuvi na kujielekeza katika kufanya hivyo kuhakikisha kwamba mradi huu
wanaofaidika ni wavuvi wenyewe"
"Ni matumaini yangu
baada ya siku kadhaa tutakuja kuwa na kitu kikubwa sana kuweza kutusaidia
kuyafikia maisha ya wengi ambayo ndiyo maelekezo lakini pia ndiyo maono ya Rais
wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunaenda kuyakuta mahitaji ya watu na
tunayafanyia kazi" amesema
Dkt. Mhede amesema
changamoto nyingine zinazowakabili wavuvi hao, ni pamoja na uduni wa Teknolojia
, upatikanaji masoko, upatikanaji wa mitaji ya kifedha na maarifa lakini pia
miundombinu
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh, amesema Afrika
ikiwemo Tanzania kunatatizo kubwa la upotevu wa mazao ya uvuvi ambapo inakisiwa
kati ya asilimia 30-40 ya upotevu wa mazao hayo yanatokana na mabadiliko ya
tabianchi
"Katika kipindi cha
mvua inakua ni changamoto kubwa kwa wavuvi wetu hasa wale ambao wanachataka na
wanasafirisha mfano, wavuvi wa dagaa wanavua na kuchakata, wanahitaji pia
teknolojia mpya kwa ajili ya kusafirisha mazao yao ya uvuvi" amesema Prof.
Sheikh.
Prof. Sheikh amesema
Serikali ya awamu ya sita imeendelea na jitihada za kuhakikisha wanaongeza
uzalishaji wa mazao hivyo amewaomba wadau mbalimbali kuweka mbinu bora ambazo
zitawasaidia wavuvi kuweza kuhifadhi mazao yao ambayo yatakubalika ndani na nje
ya nchi.
Naye Kiongozi wa
Mawasiliano ya Kimataifa wa Taasisi ya WorldFish, Rajita Majumdar amesema kuwa
zaidi ya tani 21.3 za samaki zimepotea kutokana na changamoto ya uhifadhi wa
mazao hayo baada ya kuvuliwa ambapo wameona ni vyema kuja nchini kuungana
na Serikali na wavuvi kwa lengo la
kupunguza upotevu huo ambao unafifisha uchumi.
"Nadhani inahitajika
matumizi ya teknolojia nafuu inayoweza kufikiwa ili kuongeza umahiri katika
kushughulikia mnyororo wa usambazaji wa chakula ambapo itasaidia kuondokana na
uharibifu mkubwa"amesema
Aditya Parmar ambaye
ametoka kwenye Taasisi ya WorldFish, amesema mradi huo umejikita katika vipengele vinne ambavyo ni usambazaji wa samaki, uuzaji, utunzaji,
uhifadhi na usafirishaji ambapo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutunza thamani ya
ubora wa chakula kwa lengo la kuhakikisha lishe bora kwa jamii ya Pwani.
"Tunataka kuona
jumuiya ya Pwani jinsi gani inaweza kuongeza mapato, tunataka kushirikisha
wanawake na vijana kutekeleza mradi huu ambao tunatarajia utabadilisha maisha
yao baada ya miaka michache ijayo "amesema
Mkutano huo unafuatiwa na
mkutano ambao utafanyika Tarehe 5-7 mwezi Juni
mwaka huu katika ukumbi wa Mikutano Mlimani city Jijini Dar es Salaam
ambao unazungumzia mahsusi wavuvi wadogo wanaochangia kwa asilimia 95.
Naibu katibu Mkuu Sekta ya
Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akiongea wakati wa kufungua mkutano wa uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech
Superhighway ambao utachukua takribani miaka 7
wenye lengo la kusaidia juhudi za serikali katika upotevu wa mazao ya uvuvi., Mkutano huo
umefanyika kwenye ukumbi wa hotel ya Ramada jijini Dar es Salaam Mei 28,2024
Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohamed Sheikh akiongea wakati wa uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech
Superhighway ambao utachukua takribani miaka 7
wenye lengo la kusaidia juhudi za serikali katika upotevu wa mazao ya uvuvi., Mkutano huo
umefanyika kwenye ukumbi wa hotel ya Ramada jijini Dar es Salaam Mei 28,2024
Mwakilishi kutoka kwenye
Taasisi ya WorldFish Bw. Aditya Parmar akiwasilisha mada wakati wa mkutano wa
uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech Superhighway na kuelezea vipengele vinne ambavyo mradi
huo umejikita ikiwa ni pamoja na usambazaji wa samaki, uuzaji, utunzaji,
uhifadhi na usafirishaji ambapo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutunza thamani ya
ubora wa chakula kwa lengo la kuhakikisha lishe bora kwa jamii, Mei 28,2024
jijini Dar es salaam.
Naibu katibu Mkuu Sekta ya
Uvuvi Dkt. Edwin Mhede akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya wadau wa Sekta
ya Uvuvi walioudhuria mkutano wa
uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech Superhighway ambao utachukua
takribani miaka 7 wenye lengo la
kusaidia juhudi za serikali katika
upotevu wa mazao ya uvuvi., Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa
hotel ya Ramada jijini Dar es Salaam Mei 28,2024